Mkutano wa 18 wa Bunge unatarajiwa kuanza leo mjini Dodoma, lakini hoja nzito ambazo zinatarajia kuibua mijadala mizito ni Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2014 na taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Jumla
ya miswada mitatu itawasilishwa kwenye mkutano huo, lakini tayari kuna
dalili kuwa muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali, ambao unagusa
kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi, unaweza kuibua mjadala mzito bungeni,
kutokana na suala hilo kila linapoibuka wabunge wamekuwa wanagawanyika.
Huu
utakuwa ni mkutano wa kwanza wa Bunge, bila kuwepo kwa vigogo ambao
wameondolewa au kujiuzulu, kutokana na kashfa ya Tegeta Escrow. Vigogo
hao ni Mwanasheria Mkuu wa zamani, Jaji Frederick Werema, aliyekuwa
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa
Madini na Nishati, Profesa Sospeter Muhongo.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na
Uhusiano wa Kimataifa ya Bunge hilo, katika mkutano huo moja ya shughuli
ambazo zitafanywa na Bunge ni kujadili taarifa za CAG zilizowasilishwa
katika Mkutano wa 15.
Miongoni
mwa madudu ambayo Ripoti ya CAG ilibaini serikalini ni malipo ya
mishahara hewa, kupotea kwa stakabadhi kwenye halmashauri, uwindaji
haramu unavyoongezeka na kandarasi tata ndani ya Mamlaka ya Bandari
nchini (TPA).
Wenyeviti
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), watawasilisha ripoti zao na serikali
itajibu taarifa hizo, ambazo ni hesabu za mwaka 2012/13.
Pia,
katika mkutano huo, Kamati za Bunge nazo zitapewa nafasi ya kuwasilisha
taarifa za mwaka za shughuli za Kamati; na zitapangiwa muda wa
kujadiliwa, kwa kadri Spika atakavyoelekeza.
Hali
kadhalika, Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza na kuchambua
Sera mbalimbali zinazohusu masuala ya ardhi, kilimo, mifugo maji na
uwekezaji ili kubaini kasoro zilizomo katika matumizi ya ardhi, itapewa
nafasi ya kuwasilisha taarifa yake, na taarifa hiyo itajadiliwa bungeni
hapo.
Taarifa
hiyo ya Bunge ilisema miongoni mwa shughuli za leo bungeni ni kuapishwa
kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju ambaye amejaza nafasi
ya Jaji Werema.
Taarifa
hiyo ilitaja miswada itakayowasilishwa na kupitishwa katika vikao vya
Bunge ni Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa Mwaka 2014 ambao
utapigiwa kura tu, Muswada wa Muswada wa Sheria ya Takwimu wa mwaka 2013
na Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 2 wa mwaka 2014.
Wakati
huo huo, Jukwaa la Wakristo limetoa tamko ambalo linaishauri Serikali
kuuondoa bungeni Muswada huo wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali kwa
kile linachodai kuwa ni kuepusha kuvunja misingi ya taifa, ambalo halina
ubaguzi na lisilo na dini yoyote.
Muswada
unaopingwa na jukwaa hilo ni ule ambao unapendekeza, pamoja na mambo
mengine, marekebisho ya Sheria ya tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka
1964, ambao unapendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.
Tamko
hilo lilitolewa jijini Dar es Salaam jana kwenye taarifa iliyosainiwa
na viongozi wa Jukwaa hilo, ambao ni Askofu Dk Alex Malasusa wa Jumuiya
ya Kikiristo Tanzania (CCT) , Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Baraza
la Maaskofu Tanzania (TEC) na Askofu Daniel Awet kutoka Umoja wa
Makanisa ya Pentekoste (CPCT) baada ya mkutano uliowakutanisha Januari
20 mwaka huu.
Kwenye
tamko hilo, viongozi hao walieleza kuwa mapendekezo ya kurekebisha
Sheria ya tamko la Sheria za Kiislamu ni mapendekezo makubwa,
yatakayokuwa na athari kubwa na nzito, yakihoji msingi wa dola ya
Tanzania kama dola isiyokuwa ya kidini.
Tamko
hilo lilieleza kuwa kwa sababu hiyo, mapendekezo hayo yanaibua mambo
mazito ya kikatiba, ambayo hayawezi kuamuliwa na muswada huo.
Tamko
hilo lilibainisha kuwa sababu zilizowezesha kufutwa kwa mahakama hizo
mwaka 1963, ilikuwa kujenga umoja wa kitaifa, kuondoa ubaguzi katika
mfumo wa kisheria na utoaji haki sawa, jambo ambalo bado ni halali na
la msingi kwa sasa.
"Kwa
sababu hiyo, kwa heshima kubwa, tunashauri kwamba Serikali iondoe
Muswada huu bungeni ili kuepusha kuvunja misingi ya Taifa hili kama
taifa lisilo la kibaguzi na lisilofungamana na dini. "
Katika
tamko hilo, viongozi hao walisema kuwa, masuala yanayohusu imani za
dini na kujiingiza kwa Serikali katika masuala yanayohusu imani hizo,
yanahitaji mjadala mpana na maridhiano ya kitaifa.
EmoticonEmoticon