Aliyejifanya
Askari Polisi wa Usalama Barabarani, James Hassan (54) amehukumiwa
kifungo cha miaka sita jela baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na
sare za Polisi na kujifanya mtumishi wa jeshi hilo.
Aidha,
adhabu hiyo ilitokana na makosa mawili ambapo mshitakiwa huyo atatakiwa
kutumikia kifungo cha miaka mitatu mitatu kwa kila kosa.
Akisoma
hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassan Juma wa Mahakama ya
Wilaya ya Ilala, alisema kwamba ametoa adhabu hiyo ambayo haitaenda kwa
pamoja, kutokana na mshitakiwa huyo kuwa ni mkosefu mzoefu.
Pia
alisema kwamba mahakama hiyo imemtia hatiani kupitia kwa mashahidi
watatu wa upande wa mashitaka walioithibitishia mahakama bila ya kuacha
shaka.
Kabla
ya hukumu, mshitakiwa huyo alidai kwamba kwa kuwa mahakama imemwona
kuwa ana hatia, yeye hakufanya kosa hilo na hata ikiwezekana mahakama
imuachie huru.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi hayo na badala yake alihukumiwa kifungo hicho.
Wakili wa serikali, Florida Wenuslaus alidai kuwa mshitakiwa apewe adhabu iwe fundisho kwa wengine.
Katika
kumbukumbu za makosa ya nyuma ya mshitakiwa, ilibainika kwamba
mshitakiwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la
unyang’anyi wa kutumia silaha, katika mahakama ya Wilaya ya Isanga,
Dodoma na kufungwa katika gereza la Isanga mkoani humo.
Pia mshitakiwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela kwa kosa la kukutwa na sare za Jeshi la Polisi.
Katika
barua iliyoandikwa na Mkuu wa Gereza la Keko kwenda kwa Hakimu Mfawidhi
wa Mahakama hiyo, iliithibitishia mahakama kwamba mshitakiwa huyo
alikuwa na kesi namba 32 ya mwaka 2004 na kwamba mshitakiwa
alijiandikisha kwa jina la Ally Kinanda.
Pia
barua hiyo ilieleza kuwa Hassan alitoroka akiwa chini ya uangalizi wa
jeshi hilo na kwamba asipatiwe dhamana baada ya kukamatwa na kufikishwa
katika mahakamana hiyo, kwa kuwa mshitakiwa alikana kuhusika na tuhuma
hizo na kueleza kuwa watafuata taratibu zote kuchukua alama za vidole
ili kuthibitisha kabla ya kupatiwa dhamana.
Ilidaiwa
kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo Agosti 14, 2014 maeneo ya
Kinyerezi mnara wa Voda akijifanya kwamba ni askari polisi wa Usalama
barabarani.
EmoticonEmoticon