SERIKALI
imetoa siku 30 kukamatwa kwa watumishi waliosababisha matumizi mabaya
ya fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) III, kwa
kuingiza majina ya watu masikini wasiostahili ili kujipatia fedha za
mradi huo.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
George Simbachawene akizungumza na baadhi ya wakuu wa mikoa, wilaya na
wakurugenzi, jana alisema ni lazima watumishi wa umma waliohusika katika
kuisababishia hasara Serikali wawajibishwe.
Februari
mwaka huu, TASAF ilitekeleza maagizo ya Serikali na kufanya uhakiki wa
kaya masikini ziliopo kwenye mpango wa kupata fedha na kuziondoa zile
zilizokosa sifa na kuziondoa kaya 32,456.
“Katika
msako huo tulibaini, waliokufa ni 7,819, viongozi waliojipachika 2,999,
waliohama sehemu ambapo mpango haujaanza 3,948, wasiojitokeza au
wasiofahamika 9,342 na wasiokuwa na sifa 8, 348,” alisema Simbachawene.
Aidha
alisema kuwa, zoezi hilo ni endelevu na kwamba utaratibu wa kutoa
taarifa za walengwa waliofariki au kuhama unapaswa kufanyika ili fedha
za serikali zisitumike ovyo nje ya malengo yaliyokusudiwa.
Simbachawene
alisema, kuingizwa kaya zisizo na sifa katika mpango huo na kuachwa kwa
kaya ambazo ni maskini zaidi, kumetokana na baadhi ya watumishi wasio
waadilifu ambao pia wamekuwa wakipunguza malipo ya walengwa.
Watu
6.5 milioni, katika kaya maskini na zinazoishi katika mazingira
hatarishi wanatarajiwa kunufaika na mradi wa fedha za TASAF katika awamu
ya sasa.
Hata
hivyo, Simbachawene aliwashauri wakurugenzi wa halmashauri zote nchini
pamoja na wakuu wa wilaya, kutoogopa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu
wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwani suala hilo litaepusha
hasara na mianya ya wizi.
Mhandisi
Evarist Ndikilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, alimuahidi waziri Simbacahwene
kuwa, hawatofumbia macho ubadhirifu katika halmashauri na kusema
watazishauri, kuzikumbusha na hata kuingilia kati pale mambo yanapoenda
ndivyo sivyo katika halmashauri.
EmoticonEmoticon