TANZANITE YAING’ARISHA TANZANIA KATIKA MAONESHO YA VITO BANKOK


 Wanunuzi wa madini wakikagua madini ya vito kutoka kwa mfanyabiashara wa madini wa Tanzania katika banda la Tanzania kwenye maonesho kimataifa ya 56 ya Madini ya vito na usonara yanayofanyika mjini Bankok, Thailand.
 Ofisa kutoka Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA), Bi. Stella akimpatia maelezo mmoja kati ya wanunuzi wa madini ya vito waliofika katika banda la Tanzania kutaka maelezo ya jinsi ya kuweza kununua madini hayo ya vito yanayopatikana Tanzania.
 Picha ya pamoja kati ya ujumbe kutoka Wizara ya Nishati na Madini ya Tanzania na maofisa waandamizi wanaosimamia maonesho ya kimataifa ya Madini ya vito mara baada ya ufunguzi rasmi kufanyika jijini Bangkok, Thailand.
 Wanunuzi wa Madini ya vito waliofika katika banda la Tanzania wakipata maelezo kutoka kwa maofisa wa Wizara ya Nishati na Madini waliopo kwenye banda la Tanzania.
Wanunuzi mbalimbali wa madini ya vito waliofika katika banda la Tanzania wakijadiliana namna ya kununua madini ya vito kutoka kwa Wafanyabiashara wa Tanzania.



Na Mwandishi Wetu, Bangkok
Maonesho ya 56 ya vito na usonara yameanza kwa kishindo jijini Bangkok, Thailand huku Tanzania ikiwa imeng’ara kutokana na madini ya tanzanite kuzalishwa katika nchi ya Tanzania pekee duniani.

Maonesho ya kimataifa ya vito na usonara yameanza rasmi tarehe 10 hadi 14 ambapo hufanyika kila mwaka nchini Thailand na kukutanisha wauzaji na wanunuzi wa madini ya vito na usonara duniani.

Katika maonesho hayo ambapo wachimbaji na wauzaji wa madini wanashiriki ili kujitangaza pamoja na kutafuta masoko ya madini yao kwa sasa na katika siku zijazo ambapo wanunuzi wengi wamejitokeza na kutaka kujua utaratibu wa kuweza kununua madini hususan ya vito mbalimbali yanayopatikana Tanzania.

Wanunuzi hao wengi wamejitokeza kutoka katika nchi za Brazil, Canada, India, Thailand, Hongkong na Marekani ambapo pia wameahidi kushiriki katika maonesho ya kimataifa ya vito ambayo yatafanyika mjini Arusha.
Lengo la Tanzania kushiriki maonesho hayo nchini Thailand ni kutangaza madini ya vito mbalimbali yaliyopo nchini ikiwamo tanzanite ambayo inapatikana Tanzania pekee katika eneo la Mererani wilayani Simanjiro mkoa wa Manyara.

Aidha, ziara hiyo pia inatoa fursa kubwa kwa taifa la Tanzania hususan katika sekta ya Madini kuvutia wanunuzi mbalimbali duniani wanaoshiriki maonesho ya Bangkok kuja pia Tanzania katika maonesho ya kimataifa ya vito yanayofanyika kila mwaka mkoani Arusha kununua madini ya vito na kuufanya mji wa Arusha kuwa kituo kikubwa cha madini ya vito katika bara la Afrika.

Ni dhahiri kwamba maonesho hayo ya vito Bangkok ni jitihada za serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini hususan Idara ya Madini kuwatafutia masoko wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hasa wale wadogo.
Katika maonesho hayo wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hasa ya vito wapata mawasiliano kwa wanunuzi mbalimbali wa kimataifa badala ya kuwatumia madalali ili kuweza kuuza madini yao kwa wanunuzi walengwa na kuuza madini kwa bei nzuri na hatimaye kupata faida maradufu.

Maonesho hayo ya vito yanatoa fursa pia kwa sekta nyingine kujitangaza pamoja na kuitangaza Tanzania duniani mathalan sekta ya utalii ambapo madini ya vito yanakwenda pia na ujumbe wa vivutio vya utalii vilivyopo nchini ikiwamo mbuga za wanyama pamoja na mlima wa Kilimanjaro.
SOURCE:MATUKIO-MICHUZI

Previous
Next Post »