WATU wengi duniani wamekuwa wakitumia dawa za mitishamba kutibu maradhi
mbalimbali, lakini siku za karibu utafiti wa sayansi unaonyesha kuwa mti
wa ‘hibiscus sabdarifa’, unaojulikana kama Rosella umeibua habari mpya
kuwa unaweza kutibu shinikizo la damu.
Ukizungumza
na watu wa makabila, rangi na mataifa mbalimbali, wanasema ukitumia
dawa za mitishamba, unaweza kupata nafuu kwa ugonjwa huo. Dawa za
mitishamba hiyo si maarufu Afrika pekee, kwa sababu ni maarufu zaidi
kwenye vituo vya awali vya afya katika nchi za Ulaya kama Ubelgiji,
Ufaransa, Ujerumani na Uholanzi.
Umaarufu
wa vituo vya kutoa huduma za afya, unaonyesha namna dawa za mitishamba
zinavyokubalika na zinavyotumika katika viwanda vingi vikiwamo vya
vipodozi. Ukweli kuwa dawa hizo zinatumika, kumebainika pia kwa kuongeza
gharama za matumizi ya kila siku katika kutunza afya zao na kuboresha
maisha yao.
Miongoni
mwa vipodozi vinavyotokana na mitishamba ambavyo vinapendwa na
watumiaji wengi ni vile vinavyotumika katika kutengeneza upya ngozi,
kuondoa magamba mwilini na kutumika kama krimu ya kulainisha na
kuboresha ngozi mwilini.
Duniani,
dawa za mitishamba zinatumika zaidi China, India, Japan, Pakistan, Sri
Lanka na Thailand. Nchini China, zaidi ya asilimia 40 ya matumizi ya
dawa nchini humo ni ya mitishamba. Watu wengi wanaoishi mijini hawana
habari juu ya utajiri wa maua na mimea inayowazunguka ambayo Mungu
amewapa na ambayo ina faida kubwa katika maisha yao ya kila siku.
Wanasayansi
wanathibitisha kuwa mmea wa rosella, unaopatikana katika maeneo mengi
nchini, ni tiba muhimu ya shinikizo la damu kuanzia hatua za mwanzo hadi
linapofikia hatua ya kati. Hadi sasa majaribio mengi yamefanyika kwa
kutibu wanyama na binadamu na yameonyesha mafanikio makubwa upande wa
utunzaji na upunguzaji shinikizo la damu. Maji ya miti hiyo yakikamuliwa
yanakuwa na ubora sawa na dawa nyingine za hospitalini zinazotibu
shinikizo la damu.
Mfumo
wa namna ya kutengeneza dawa za kushusha kiwango cha shinikizo la damu
bado unahitaji kufanyiwa utafiti zaidi. Lakini matokeo yaliyopatikana
kutokana na kutibu wanyama, yameonyesha wazi kuwa mmea huo unatoa tiba
salama na haujasababisha madhara kwa wanyama na binadamu.
Pamoja
na kupunguza shinikizo la damu, utengenezaji dawa kutokana na mti huo
pamoja na vikonyo vya majani yanayohifadhi maua ambayo kabla
hayajachanua yanasaidia kupunguza mgandamizo wa damu mwilini.
Dawa
hiyo ina kazi ya kupunguza oksijeni mwilini na inaweza pia kutumika
kuzuia kansa na magonjwa kwenye maini, hasa kwa wanywaji wa pombe. Ni
nzuri kuitumia kwa wagonjwa wa upungufu wa damu kwani imeonyesha wazi
ina uwezo wa kuimarisha nyumba zinamokaa chembechembe nyekundu za damu.
Dawa
hiyo inasaidia kuhuisha upya maisha ya mtu mwenye upungufu wa damu. Kwa
upande wa chakula bora, dawa hiyo ni tajiri wa vitamani C, thiamin,
riboflavin na niacin. Pia ina madini muhimu mwilini ambayo ni calcium,
phosphorus na chuma.
Kwa
miaka mingi, rosella imekuwa ikitumika katika nchi mbalimbali kama
nishati muhimu ya kupikia na chanzo mahususi cha dawa za kutibu maradhi
mbalimbali ya binadamu. Dawa hii ilitumika kwa wingi barani Asia,
Amerika Kusini, Visiwa vya Caribbeani, Ulaya na Asia. Ilitumika katika
kuandaa mishumaa, mafuta na viungo moto na baridi na ilitengeneza mvinyo
mzuri wa kunywa.
Ukichanganya
na chai utajisikia unakunywa kinywaji chenye harufu nzuri inayonukia
kama dawa na kama kirutubisho mwilini. Si ajabu kusikia dawa hiyo baada
ya kunywa inaondoa uchovu, mafua na maradhi ya tumbo hasa ya kujaa gesi.
Taarifa
ya hivi karibuni ya Shirika la Afya Duniani (WHO), inasema, ‘kuzuia
magonjwa sumbufu, ni uwekezaji muhimu.’ changamoto iliyopo kwa taasisi
za magonjwa ya moyo na kupooza, miongoni mwa taasisi nyingine, ni
kutakiwa kuponya maisha ya watu milioni 36 duniani ambao wanaweza kuwa
wamekufa kufikia mwaka 2015.
Kuwa
dawa hiyo inatibu shinikizo la damu ni faraja kwetu sote, kwa sababu
magonjwa ya mifumo ya hewa imetokea kuwa miongoni mwa magonjwa sugu
yanayosumbua afya ya jamii katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo.
Kwa
mujibu wa Profesa Jacob Mtabaji, katika Tanzania, magonjwa ya mifumo ya
hewa yanachangia asilimia 15 ya vifo vya watu wenye umri wa zaidi ya
miaka 30, na hivyo kuufanya ugonjwa huo kusababisha vifo vingi kwenye
kundi hilo.
Hivi
karibuni utafiti umeonyesha kuwa asilimia sita ya vifo hivyo nchini
Tanzania vinatokana na kupooza kwa watu wazima wenye umri kati ya miaka
15 na 64. “Vifo vya kupooza kwa mwaka ni watu 65 kati ya watu 100,000
kwa wanaume, wakati wanawake ni 88 kati ya 100,000, kumbe Uingereza na
Wales ni 10.8 kwa wanaume na wanawake ni 8.6,” anasema Profesa Mtabaji.
Idadi
ya vifo vya kupooza katika Tanzania vinatokana na kutotibiwa kwa
wagonjwa wengi wanaopata maradhi ya shinikizo la damu. Jijini Dar es
Salaam, utafiti unaonyesha kuwa watu wengi wanaoathirika na ugonjwa huo
ni wenye umri mkubwa. Kwani asilimia 21.8 ya wanaume wenye umri wa miaka
50-54 wana shinikizo la damu, wakati asilimia 30.9 ya wanawake wenye
umri wa miaka 50-54 ndiyo wenye ugonjwa huo.
Kundi
la watu wenye umri wa miaka 40 hadi 44, kiwango cha shinikizo la damu
kwa wanaume ni asilimia 6.4 na wanawake 11.5. Wakati kundi la watu wenye
umri wa miaka 30 hadi 34, kiwango cha shinikio la damu ni asilimia 6.4
wanaume na wanawake ni asilimia 5.9. Maendeleo ya utafiti wa miti ya
habiscus sabdariff umekuja wakati muafaka ambako dawa za mitishamba
zinapata umaarufu nchini mwetu kutokana na juhudi za watafiti mbalimbali
walioamua kuinua kiwango cha dawa za mitishamba nchini.
Mti
huo unapatikana Tanzania na unapandwa mkoani Kilimanjaro, Morogoro,
Dodoma na Pwani. Taasisi ya Dawa za Mitishamba katika Chuo Kikuu cha
Sayansi ya Afya Muhimbili (MUCHS), inaitambulisha dawa hiyo kama chanzo
cha kuleta lishe bora na kinywaji chenye kuleta afya.
Kinachotakiwa
ni kuchukua maganda ya miti hiyo na kuchanganya na maji, halafu tikisa
na utapata kinywaji kizuri cha kuburudisha. Mti huu ni miongoni mwa
mimea ambayo ipo kwenye mradi wa kutaka liwe zao la kuzalishwa katika
maeneo mengi ili liwe chanzo cha mapato kwa wakazi wa Kongowe, mkoani
Pwani.
“Mpango
wa muda mrefu wa zao hilo ni kupanga daraja la uwezo wa zao, ama kutibu
peke yake au kwa kuunganisha na dawa nyingine,” anasema Dk. Mainen
Moshi, kiongozi wa mradi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mitishamba,
Muhimbili. Mradi huo una malengo mawili, kwanza, una lengo la kuchangia
katika mkakati wa kitaifa wa kupunguza umaskini kwa kuzalisha zao hilo
na kuwa chanzo cha lishe bora na kuongeza kipato cha wananchi.
Pili,
ni kuchangia katika uboreshaji sera za taifa za chakula na lishe bora
ambazo zinalenga katika kuongeza mazingira ya uzalishaji lishe bora
miongoni mwa watoto na wanawake hata wanaoishi na virusi vya ukimwi.
Kuwapo
kwa mmea huo nchini, ni kitu kizuri na cha kujivunia, na hivi karibuni,
wanasayansi wamekuwa wakiutangaza kwa nguvu zao zote, kuhakikisha taifa
linatambua umuhimu wa mti huo na namna linavyoweza kuutumia.
EmoticonEmoticon