WATANZANIA WANUNUA KANSA KWA SHILINGI 750

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj-Ud0li8SLf9xpW8QvPuhU9uhs-CRhrgn1SLl5ymkKOlGlkNWazDPO31v7GCmtIianJRfDYHoXhWicM0orHsgV96rnAPQHXX9fPkO71cuLcLsirR65eG7pL-Vqw3ciGyjsDWpF7LgTpC0/s1600/Vipodozi-26Jan2015.jpg 

Baadhi ya vipodozi vyenye viambata vilivyiopigwa marufuku
 huchanganywa na vipodozi halali na kisha kuuzwa waziwazi kama hivi vilivyokutwa maeneo ya Soko la Tandika, jijini Dar es Salaam.
Kasi ya wananchi kujiweka katika hatari ya kupata magonjwa ya kansa imeendelea kupamba moto jijini Dar es Salaam na kwingineko nchini licha ya jitihada kubwa zinazoendelea kufanywa kila uchao katika kudhibiti hali hiyo, imefahamika.


Wananchi hao, hasa kina mama na wasanii wa fani mbalimbali wakiwamo wa filamu, muziki wa dansi na bongofleva, wamekuwa vinara wa kununua vipodozi vyenye viambata vya sumu na kujipaka mwilini kwa nia ya kujiongezea urembo na utanashati lakini bila kujua kuwa wanajiweka katika hatari ya kupata magonjwa ya kansa, hasa ya ngozi na ini.  


Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE kuanzia wiki iliyopita umebaini kuwa watu wanaojiweka katika hatari hiyo hununua vipodozi hivyo kwa kati ya Sh. 750 hadi Sh. 7,000 kwa chupa kutegemeana na ujazo na pia aina ya kipodozi na chapa yake (brand) huku mkorogo wenye mchanganyiko wa vipodozi hivyo, maarufu kama 'manjano' au 'kijiko special' ukiuzwa kwa Sh. 1,000 kwa kipimo cha kijiko kimoja kikubwa cha chai.

Kadhalika, imebainika kuwapo kwa utitiri wa vipodozi vyenye sumu katika maduka na masoko mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kwingineko nchini huku wauzaji na wateja wao wakionekana kupuuza au kutofahamu lolote juu ya ukweli kwamba bidhaa hizo zinahatarisha afya yao na vilevile wanajiweka katika hatari ya kukumbana na mkono wa dola kwani kuuza au kutumia bidhaa hizo kunakiuka sheria za nchi.


Katika maeneo kama ya masoko ya Tandika, Buguruni, Manzese, Magomeni, eneo la Mbagala Rangi Tatu na kwingineko nchini, vipodozi hivyo huuzwa bila kificho na baadhi huuzwa kwa kuwekwa kwenye viroba na kupangwa ardhini huku vikipigiwa debe na wauzaji kama ilivyo kwa biashara ya nguo za mitumba.


Katika tovuti yao (http://www.tfda.or.tz) na pia kupitia kampeni mbalimbali za kuelimisha umma, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imekuwa ikivitaja viambata vyenye sumu kwenye vipodozi kuwa ni pamoja ni Bithionol, Hexachlorophene, Mercury, Vinyl chloride, Zirconium, Halogenated salicylanilides (di-, tri- metabromsalan and tetrachlorosalicynilide), Chloroquinone, Steroids, Chloroform, Chlofluorocarbon na Methyelene chloride.


Aidha, TFDA imetaja vipodozi zaidi ya 100 vyenye viambata vyenye sumu. 


Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya vipodozi hivyo ndivyo vilivyojaa sokoni na kwenye baadhi ya maduka, vikiwamo vya Mekako, Rico, Princess Cream, Butone Cream, Extra Clear Cream, Viva Super Lemon Cream, Ultra Skin Tone Cream. Vingine ni Clere Extra, Top Lemon, Diproson, sabuni aina ya Jaribu, Riki, Amira na pia cream kama Movate, Demovate na Oranvate.


HATARI ILIYOPO

Vipodozi hivi vyenye viambata vya sumu husababisha pia ngozi kuharibika na kuifanya kuwa nyepesi, hivyo kusababisha miale hatari ya jua (UV-B) kupenya kirahisi kwenye ngozi na kusababisha kansa.


Kaimu Mkuu wa Idara ya Kuzuia Udhibiti wa Kansa katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, Dk. Maguhwa Stephano, ameiambia NIPASHE kuwa vipodozi vyenye viambata vya sumu vina madhara makubwa na wananchi wanapaswa kujua kuwa kuvitumia ni kujihatarishia uhai kwani magonjwa ya kansa ni ya hatari na kutibu kwake huligharimu taifa fedha nyingi.


Akieleza zaidi, Dk. Maguhwa anasema kuwa matumizi ya vipodozi vyenye viambata vya sumu kama Sterodis huchangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa ongezeko la wagonjwa wa kansa ya ngozi kwenye Hospitali ya Ocean Road, hasa ya aina za Kaposis Sarcoma na Squamous Cell Carcinoma.


Dk. Maguhwa anasema mbali na watumiaji waliobobea wa vipodozi vyenye viambata vya sumu, wengine wanaokumbwa zaidi na saratani hizo za ngozi ni watu waliopungukiwa na kinga za mwili, hasa wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na pia watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).


"Hatuna takwimu za kuonyesha moja kwa moja idadi ya watu wanaopata kansa kwa sababu ya kutumia vipodozi vyenye viambata vya sumu... hata hivyo, kansa ya ngozi ni miongoni mwa kansa wanazokutwa nazo watu wengi tunaowapokea," anasema Dk. Maguhwa.


Anaongeza kuwa maradhi hayo (ya kansa ya ngozi) ni miongoni mwa aina tatu za kansa zinazoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wanaofika Ocean Road, wengine wengi wakiwa ni wa kansa za shingo ya kizazi (cervical cancer) na wa kansa ya matiti.


"Anayetumia vipodozi vyenye viambata vya sumu anajiweka katika hatari pia ya kupata aina nyingine za kansa... ni vyema wananchi wakawa makini na kuchana na matumizi ya vipodozi hivi vinavyohatarisha afya zao," anasema Dk. Maguhwa.


Kwa mujibu wa Dk. Maguhwa, gharama za kuwatibu wagonjwa wa kansa ni kubwa na hivyo serikali hufanya kazi ya ziada ya kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika kila mwaka ili kuwatibu wananchi wake; rasilimali ambayo pengine inaweza kutumiwa kwa shughuli nyingine za maendeleo ikiwa wananchi watajiepusha kutumia vipodozi hatari wanavyovinunua kwa fedha kidogo lakini wakijiweka katika hatari kubwa kiafya.


Anasema tiba kubwa wanazotoa kwa wagonjwa wa kansa huwa ni za aina tatu, ambazo ni kwa kutumia mionzi, drip na pia kwa dawa maalum (chemotherapy). Na matibabu yote hayo huhitaji gharama kwa kila mgonjwa. 


"Kwa kawaida, gharama ya kipimo cha wagonjwa wa kansa (Biops) ni Sh. 50,000 hadi 80,000 kulingana na mahala anakokwenda mgonjwa. 


Gharama nyingine na mionzi huwa kati ya Sh. 800,000 hadi 1,200,000. Katika hali ya kawaida, wastani wa gharama za kuwatibu wagonjwa wa kansa ya ngozi kwa mwaka huwa ni zaidi ya 2,000,000. Isipokuwa, lazima ifahamike kuwa gharama kuwa juu au chini hutegemeana na stage ya ugonjwa wenyewe na mahala ulipo katika mwili,” anasema.


"Kwa mfano, kansa inapokuwa kooni gharama za tiba yake huwa tofauti na mkononi... wapo wanaotibiwa kwa mionzi na pia wapo wanaolazimika kutibiwa kwa mchanganyiko wa mionzi na drip ili kuwanusuru. Vifaa, dawa na huduma zenyewe huwa ghali sana. Hapa kwetu (Ocean Road) serikali ndiyo hugharimia kwa kiasi kikubwa," anasema Dk. Maguhwa.


Akieleza zaidi, Dk. Maguhwa anasema changamoto pekee ni ukweli kwamba saratani huwa haifahamiki kirahisi bali ni kwa kutumia vipimo kama Biops na vinginevyo.


Anasema watumiaji wa vipodozi vyenye viambata vya sumu wanaweza wasijue kuwa tayari wana kansa kwa sababu dalili huwa hazijitokezi mapema na hivyo, ni bora wakaacha bidhaa hizo sasa na kufanya utaratibu wa kwenda kuchunguzwa afya zao kabla hali haijawa mbaya.   


"Njia pekee ya kubaini saratani mapema ni kwa kila mtu kujenga mazoea ya kwenda kuchunguzwa afya yake. Dalili za saratani huwa hazionekani kirahisi. Mara nyingi huja kubainika wakati hali imeshakuwa mbaya na hivyo ushauri wetu bado ni huo wa kuwataka wananchi waepuke kutumia vipodozi hivi hatari kwao," anaongeza Dk. Maguhwa.


Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu takriban milioni 3 hupata kansa kila mwaka, huku milioni moja kati yao wakiwa ni watu wanaopata saratani ya ngozi.


TFDA WANENA

Afisa Uhusiano wa TFDA, Gaudencia Simwanza anasema vipodozi vya sumu ni janga kubwa linalopaswa kudhibitiwa kwa ushirikiano wa pamoja baina ya mamlaka yao na wadau wengine, hasa wananchi wenyewe.


Anasema tafiti mbalimbali zimethibitisha kuwa watumiaji wa vipodozi vyenye sumu wanajiweka katika hatari kubwa ya kupata maradhi ya kansa na pia athari nyingine nyingi za kiafya.


Anataja madhara mengine mbali na kansa ya ngozi kuwa ni kansa ya ini, kina mama wajawazito kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo, shinikizo la damu na pia uwezekano wa kina mama kuota ndevu pindi wanapotumia vipodozi vyenye sumu kwa muda mrefu.


"Watumiaji wa vipodozi hivi wanajiweka katika hatari pia ya kutoweza kutibiwa vizuri na kupona pindi wanapopata ajali... hii ni kwa sababu ngozi zao zinapopata majeraha huwa haziwezi kushonwa," anasema Simwanza.  


Kuhusiana na udhibiti, Simwanza anasema kuwa mamlaka yao hujitahidi kufanya ukaguzi wa kustukiza kila mara kwenye maduka na maeneo mengine yauzayo vipodozi, kushirikiana na mamlaka nyingine kama jeshi la polisi katika kufanya ukaguzi maeneo ya mpakani mwa nchi na pia kufanya kampeni mbalimbali za kuelimisha umma.


Anaongeza kuwa kasi ya uingizaji wa vipodozi vyenye sumu nchini ni kubwa lakini wameendelea kufanya jitihada za kutosha za kudhibiti. Hadi kufikia sasa, wamekuwa wakikamata na kuteketeza wastani wa tani 54 za vipodozi vyenye viambata hivyo kila mwaka, thamani yake ikiwa ni takriban Sh. milioni 354.


Anasema Sheria ya Chakula, Dawa  na Vipodozi ya mwaka 2014 inawapa mamlaka ya kukamata na kuteketeza vipodozi vyenye viambata vya sumu.


"Sheria inapiga marufuku viambato vyenye sumu na vipodozi vyenye viambato viletavyo madhara... ni katika vifungu 87(i) na 90," anasema Simwanza.


Hata hivyo, anasema kuna changamoto kadhaa za kisheria kwani kadri inavyoonekana sasa, adhabu kwa wahusika zinaonekana zimepitwa na wakati na kwamba hazitishi wahalifu kiasi cha kutosha. 


 "Watuhumiwa wanaokutwa na vipodozi visivyofaa hunyang'anywa vipodozi hivyo na hulipia gharama ya kuviteketeza. Sambamba na hilo, wengine hufikishwa mahakamani. Kesi 10 zilifikishwa mahakamani."


Anasema matumizi ya vipodozi visivyofaa yatakoma mara moja pindi jamii ikibadilika na kwamba,  TFDA inaamini kwa kuendelea kutoa elimu, lengo hilo litatimizwa kwani kidogokidogo jamii itakuwa ikibadilijka.


"Suala kubwa ni elimu kwa watumiaji. Hao wanaoviuza hawatakuwa na soko kama wananchi wataacha kununua. TFDA imeanza kupita shuleni kutoa elimu kwa walimu na wanafunzi juu ya madhara ya vipodozi. Tumefanikiwa kufikia wanafunzi na walimu 2,000 mwezi Novemba na Desemba, 2014 jijini Dar es Salaam," anasema Simwanza.


WAUZAJI

Baadhi ya wafanyabiashara wanaouza vipodozi vyenye viambata vya sumu wanasema kuwa wanajua baadhi ya vile vinavyokatazwa lakini hawana namna ya kuacha kuviuza kwa sababu vina wateja wengi, vinawapatia fedha za kujikimu kimaisha na familia zao na kwamba, kubwa kuliko yote ni ukweli kuwa huingia nchini kila uchao na ndiyo maana huviuza kwa uwazi.


"Vipodozi hivi vinaruhusiwa katika nchi za Kongo, Malawi na hata Zambia. Vinapita mipakani kila siku na hakuna hatua zozote za maana zinazochukuliwa kwa waingizaji wakubwa. Kuja kutukamata watu kama sisi huku Buguruni na kwingineko ni kutuonea tu. Wazuie huko vinakoingia," anaema mmoja wa wauzaji wa vipodozi hivyo.


"Mimi najua vimepigwa marufuku na tena vina madhara makubwa. Lakini vinanisaidia kupata fedha ya kujikimu kimaisha. Hapa nilipo, katika umri wangu wa miaka 34 tayari nimeshajenga nyumba ninayoishi na familia yangu, ninasomesha wanangu wawili pamoja na mdogo wangu mmoja anayeingia kidato cha nne na pia nimeajiri vijana watatu katika maduka yangu mengine matatu ya vipodozi hivi," anasema.


"Cha kushangaza, baadhi ya wateja wetu wakubwa ni askari polisi wa kike na pia wa kiume wanaokuja kuwanunulia vipodozi wake zao. Ni mara chache huwa tunatishiwa kukamatwa na askari wa hivyo huwa anapozwa kitu kidogo kama elfu kumi, anaondoka... ni vigumu kuzuia biashara hii," anaongeza mfanyabiashara mwingine anayeuza vipodozi hivyo Manzese jijini Dar es Salaam.


FAIDA, NAMNA YA KUPATA MZIGO

Akielezea namna ya kupata vipodozi hivyo, mmoja wa wauzaji wakliopo katika soko la Tandika alisema kuwa ni lazima anayetaka mzigo aunganishwe kwa wakala wanaoleta vipodozi hivyo kila siku, hasa kupitia Tunduma mkoani Mbeya.


"Yapo maghala makubwa tu yenye kupokea mizigo hii (ya vipodozi vya sumu). Ukishaaminiwa, unapata mzigo bila shida yoyote na faida siyo mbaya sana. Kwa mfano, kipodozi tunachouziwa bei ya jumla Sh. 1,500 tunauza kwa reja reja hadi Sh. 3,500. Mimi kwa siku huwa sikosi kupata mauzo ya Sh. 70,000," anasema muuzaji mwingine wa Mbagala Rangi Tatu.


Mfanyabiashara mwingine wa Soko la Tandika anasema yeye huingiza fedha nzuri kupitia mauzo ya mkorogo uitwao manjano au 'Kijiko Special'.

Anasema aina hiyo ya kipodozi huitengeneza kwa kuchanganya manjano ambayo hutumiwa na kina mama kujiondoa chunusi na vipodozi vingine kadhaa kama Extra Clare, Top Lemon na Carolight.


"Kila siku huwa nauza kisado (plastiki dogo la ujazo wa lita 5) kimoja au zaidi. Watumiaji wanapenda huu mkorogo kwa sababu una mchanganyiko wa vipodozi vingi na bei yake ni Sh. 1,000 tu. Ni mzuri sana kwa sababu wanakuwa weupe mapema na ngozi yao inakuwa nyororo kama ya mtoto mchanga," anasema mfanyabiashara huyo anayekataa kutaja jina lake.


Muuzaji huyo aliwataja wateja wake wakubwa kuwa ni kina mama wanaopenda kubadili rangi za ngozi zao ili kuonekana weupe na pia wanamuziki na wasanii mbalimbali, wakiwamo wa filamu na muziki wa kizazi kipya 'bongofleva'.


MBEYA, ARUSHA

Kwa mujibu wa TFDA, mikoa iliyopo mipakani ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vipodozi vinavyokamatwa vikiwa na viambata vya sumu, na hasa mkoa wa Mbeya unaopakana na Zambia na Malawi.


Akizungumzia uingizwaji wa vipodozi hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi anasema wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kudhibiti uingizwaji wa vipodozi hivyo ingawa kumekuwa na changamoto kubwa, hasa kutokana na ukweli kwamba kuna njia nyingi za panya; jambo lililowahi kuelezwa pia na Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo, aliyesema kuwa mpaka wa Tanzania na Malawi mkoani Mbeya ni mdogo lakini una njia 32 za panya.


Mwishoni mwa wiki, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Kanda ya Kaskazini iliteketeza vipodozi vyenye sumu kufuatia msako mkali ulioendeshwa kwenye maduka mbalimbali jijini Arusha.


Meneja wa TFDA Kanda ya Kaskazini, Damas Matiko, alisema vipodozi vilivyokamatwa ni vya uzito wa kilogram 68.029, vikiwa na thamani ya Sh. 2,981,000. Vilikamatwa Novemba na Desemba, 2013.


KWINGINEKO AFRIKA

Katika makala kuhusiana na vipodozi vyenye vimabata vya sumu iliyochapishwa na mtandao wa BBC Januari 1, 2013, ilielezwa kuwa matumizi ya vipodozi hivyo ni janga kubwa barani Afrika. Kwa mfano, madaktari wa ngazi katika hospitali moja jijini Dakar, Senegal walikaririwa wakisema kuwa hupokea takriban kina mama 200 kila wiki wanaokuwa wameathiriwa vibaya ngozi zao baada ya kutumia vipodozi vyenye sumu kwa nia ya kubadili rangi za ngozi zao.


Mtandao wa voices in bioethics unakariri taarifa za utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoonyesha kuwa nchi za Mali, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini na Togo ndizo zinazoongoza kwa matumizi ya vipodozi vyenye viambata vya sumu barani Afrika. Katika utafiti huo, inaelezwa kuwa wanawake ndiyo vinara kwani kila uchao, asilimia 77 ya wanawake wa Nigeria hutumia vipodozi hivyo, wakifuatiwa na Togo (59), Afrika Kusini (35), Senegal (27) na Mali (25).

Na Ramadhan Mbwaduke -NIPASHE
 
 
Previous
Next Post »