Uchaguzi wa rais na wabunge Angola


Wananchi wa Angola wanapiga kura kumchagua rais mpya pamoja na wabunge wapya katika uchaguzi wa pili nchini humo tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe kumalizika muongo mmoja uliopita.

Vituo vingi vya kupigia kura katika mji mkuu Luanda, vilifunguliwa mapema licha ya hofu kuzuka kuhusu utaratibu wa usafirishaji wa vifaa.

Chama cha zamani cha waasi, Unita, ambacho sasa ndio chama rasmi cha upinzani, kilitoa wito wa kuakhirishwa kwa uchaguzi huo kikidai kuwepo changamoto nyingi zitakazoathiri uchaguzi huo.

Rais Jose Eduardo dos Santos, mwenye umri wa miaka 70, anatarajiwa kushinda uchaguzi huo na kuongoza kwa muhula mwingine wa miaka mitano. Amekuwa akiitawala nchi hiyo tangu mwaka 1979.

Uchumi wa Angola umeweza kuimarika tangu mwaka 2002, baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kumalizika. Vita hivyo viliathiri pakubwa nchi hiyo ilipoanza kujitawala mwaka 1975.

Lakini upinzani unasema kuwa ni wachache tu walioweza kunufaika kutokana na uchumi huo.

Uchaguzi huo pia ni wa kwanza kufanyika chini ya katiba mpya ambayo iliharamisha uchaguzi wa moja kwa moja wa rais.

Badala yake kiongozi wa chama kinachopata viti vingi vya bunge ndiye anakuwa rais.

Uchaguzi huu bila shaka ni hatua muhimu kwa Angola wakati ikiimarisha demokrasia na amani na ikitaka kuonekana kama nchi inayoweza kuendesha uchaguzi wake kwa njia mwafaka.

Hakuna anayetarajia kuwa chama tawala cha MPLA kitashindwa. Hii ni kwa sababu ya kampeini zake kubwa ambazo kilifanya pamoja na kuwa ni chama tawala, hatua ambayo inakipa nafasi nzuri ya kushinda kuliko vyama vingine.

Ikiwa uchaguzi utakumbwa na dosari zozote basi huenda vyama vya upinzani havitakubali matokeo ya uchaguzi na huenda kukazuka vurugu.

Wananchi wa Angola bado wana kumbukumbu za matukio ya baada ya uchaguzi wa mwaka 1992 uliogombaniwa sana na ambayo yaliirejesha nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Wadadisi wanasema kuwa nchi hiyo ingetaka kuzuia kabisa jambo kama hilo kutokea tena.

Previous
Next Post »