Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias akitoa mada kuhusu tabia hatarishi zinazochangia maambukizi mapya ua VVU kwa Vijana katika warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa.
Na Mwandishi wetu
Idadi kubwa ya Vijana hususan wa kike wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanaanza kufanya mapenzi katika umri mdogo jambo ambalo linaashiria hatari ya maambukizi ya VVU ikilinganishwa na idadi ya Vijana wa Kiume.
Akitoa mada kuhusu tabia hatarishi zinazochangia maambukizi mapya ua VVU kwa Vijana katika warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa, Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias, amesema hadi sasa kuna Asilimia 3.9 ya wasichana wenye umri huo wamepata maambukizi ya VVU ikilingaishwa na asilimia 1.7 ya wavulana.
Kufanya mapenzi pia katika umri mdogo kunachangia kwa kiasi kikubwa mimba za utotoni na kuathiri ustawi wa maisha ya wasichana. Wastani wa watoto wa kike 6,000 huachishwa masomo kila mwaka kutokana na mimba za utotoni.
Mratibu na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu akichangia mada iliyotolewa na Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias (hayupo pichani) katika warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa.
“Wasichana wengi wamekatishwa masomo kwa ajili ya kupata Mimba za utotoni zinazochangiwa na kufanya mapenzi katika umri mdogo tabia ambayo pia inachangia maambukizi ya VVU”, alisema Bw. Mathias.
Amezitaja tabia nyingine hatarishi zinazochangia maambukizi ya VVU kuwa ni kuwa na wapenzi wengi kwa wakati mmoja, kuwa na wapenzi wenye umri mkubwa na ngono wenzi.
Nyingine ni matumizi duni na yasiyoendelevu ya Kondomu, kufanya ngono wakati umelewa, ngono kinyume na maumbile na ngono ya jinsia moja.
Akichangia suala hilo Mratibu na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu amesema tamaduni zinazoendelezwa katika jamii pia zinachangia kumuweka msichana katika kundi hatarishi la kupata maambukizi ya VVU.
Afisa Mipango VVU/UKIMWI kutoka UNICEF, Bi. Alice Ijumbe akitoa mada ya Afya ya Uzazi kwa Vijana na mahusiano yake na maambukizi ya VVU wakati wa warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa.
Amezitaja tamaduni hizo ikiwa ni pamoja na kumbagua Mwanamke katika majukumu mbalimbali Kijinsia kutokana na tabia inayofundishwa na kutolewa kwa mtu kulingana na jinsi yake.
“Jinsia, Utamaduni na VVU ni masuala yenye mahusiano yanayomuweka Mwanamke katika hali ya hatarishi kupata maambukizi ya VVU, na kubadili tabia si jambo rahisi kwa sababu limejikita katika tamaduni zetu zinazoelekeza majukumu mbalimbali ya mwanamke na mwanaume kijinsia na hivyo kuchangia maambuki ya VVU” amesema Bi. Mwalimu.
Amesema ni jukumu la Wanahabari Vijana kuhakikisha kuwa wanahamasisha kubadilisha tabia hatarishi zinazochangia maambukizi ya VVU ambazo zimemzunguka mwanamke.
Baadhi ya mifano halisi ya kijinsia kwa wanaume na wanawake katika Afrika ikiwemo Tanzania ni kumuona mwanamume kama kiongozi katika kaya, jamii na kuwajibika kufanya maamuzi yote wakati mwanamke huonekana ni mlezi na kulinganishwa na mtoto mdogo.
Mfano mwingine ni mitala. Mahusiano ya kimapenzi hata katika jamii isiyokumbatia mitala kutoka na tamaduni zilizojikita katika jamii inakubalika kwamba mwanaume ana haki ya kuwa na wapenzi wengi wakati wanawake wanatakiwa kuwa waaminifu kwa mtu mmoja ambao ni waume zao.
“Wanawake pia wanatarajiwa kuwa watiifu kwa waume zao lakini utiifu huo hautegemewi wapewe wanawake kutoka kwa waume zao. Wanawake watakaokwenda kinyume na kanuni hiyo hunyooshewa vidole na kuambiwa kuwa wazinzi na wanaweza kuadhibiwa na jamii kwa namna yoyote ile hususani kupigwa, kutolewa maneno makali na kupewa talaka lakini wanaume hawafanyiwi hivyo”.
Kutokana na tamaduni hizo yanajengwa mazingira ambayo mwanamke anakuwa hana uwezo wa kujadili masuala ya ngono salama au ya kuridhisha kwa sababu kunakuwa hakuna mawasiliano katika nyumba kuhusu ngono kati ya mume na mke.
Mshiriki wa warsha hiyo Veronica Mtauka kutoka Kitulo FM Redio Makete akishiriki kuchangia mada wakati wa warsha hiyo.
Mradi wa SHUGA Redio unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Mashirika ya Kimataifa moja linaloshughulikia Huduma za Watoto (UNICEF), Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Redio Jamii 10 nchini Tanzania una lengo la kuendeleza kampeni za hamasa kwa vijana kupunguza maambukizi mapya ya VVU.
Redio hizo ni kutoka Karagwe, Kahama, Kyela, Kitulo na Kwanza Jamii. Nyingine ni kutoka Iringa, Simanjiro, Ifakara, Sengerema na Uvinza.
Mtangazaji wa Uvinza FM Redio, Mwinyi Mtulla akichangia hoja wakati wa warsha hiyo ya siku tatu inayoendelea mjini Iringa.
Mratibu na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu akiwaelekeza jambo baadhi ya washiriki wakati wa warsha hiyo inayoendelea kwenye kituo cha Redio Nuru FM mjini Iringa.
Pichani juu na chini ni baadhi ya washiriki wa warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa inayolenga kuendeleza kampeni za hamasa kwa vijana kupunguza maambukizi mapya ya VVU.
Baadhi ya washiriki kutoka Redio za Jamii mbalimbali watakaotekeleza Mradi wa SHUGA Redio wakiwa kwenye vikundi kazi.
EmoticonEmoticon