Na Othman Khamis Ame OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekasirishwa na kitendo cha kufungwa kwa milango ya skuli ya Msingi ya mchangamdogo kufuatia hitilafu ya mabadiliko ya jina la skuli hiyo iliyopelekea kuibuka kwa mzozo wa muda mrefu kati ya wanakijiji wa Kambini Jimbo la Kojani na wale wa Kijiji cha Mchangamdogo Jimbo la Ole.
Mzozo huo uliendelea kufukuta licha ya juhudi zilizochukuliwa na Viongozi wa Matawi, Jimbo , Wilaya na Hata Mkoa wa Kaskazini Pemba za skuli hiyo kubadilishwa jina la Kambini Mchangamdogo ili kuridhisha pande zote mbili jina lililopendekezwa na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohd Shein.
Kasirisho hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada yak upokea hoja za malalamiko ya mzozo huo zilizotolewa na Wazee pamoja na Viongozi wa wananachi wa Vijiji vyote viwili kwenye Skuli ya Sekondari ya Mchangamdodo Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Balozi Seif alisema inasikitisha kuona wazee wenye akili na busara zao kuchukuwa hatua ya kuwakosesha fursa ya kuendelea na masomo watoto wao kwa sababu nyepesi ya kugombania jina la skuli.
“ Mishipa ya shingo inatoka na kuzihangaisha akili zetu kwa kugombania jina la skuli ambazo uendeshaji wake uko chini ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya amali”. Alionyesha mshangao wake Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa siku mbili tuu kwa pande hizo mbili zinazohitilafiana kabla hajarudi Zanzibar zifikie ufumbuzi wa kama wameafiki na kukubaliana na wazo la Rais wa Zanzibar la skuli hiyo kuitwa Kambini Mchangamdogo ili kuondosha kabisa sintafahamu hiyo.
Balozi Seif alisema Serikali itaamua kutoa jina jipya kabisa litakaloona linafaa ambalo halitafanana kabisa na majina yanayogombaniwa na wananchi hao wa Kambini na Mchangamdogo.
“ Natoa siku mbili nipate jibu mtakaloliwasilisha kwa Mkuu wa mkoa wa Kaskazini Pemba kabla sijarudi Unguja kupeleka ripoti kwa Rais wa Zanzibar kama mmeliridhia jina hilo au laa “. Alisisitiza Balozi Seif.
Skuli hiyoya msingi ilibadilishwa jina tarehe 13 Januari mwaka 2014 na Kuitwa Kambini Mchangamdogo badala ya lile la mwanzo la Mchanga mdogo hali ambayo ilileta hitilafu baada ya wananchi wa Mchangamdogo kulikataa kata kata jina hilo hali ilizoashiria kuvunjika kwa amani kati ya pande hizo.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliiagiza Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kuhakikisha kwamba inatoa hati za umiliki wa viwanja kwa Wananchi wa Mtaa wa Kizimbani Wete katika kipindi kifupi kijacho ambavyo vimeshapimwa kihalali na Wizara hiyo kwa ajili ya kupewa wananchi hao kujenga nyumba za kuishi.
Balozi Seif alilazimika kutoa agizo hilo kufuatia Mkaazi mmoja wa eneo hilo Bwana Bakari Ali Omar kujilimbikizia eneo hilo la ekari 20 kinyume na utaratibu uliowekwa na Serikali kupitia Wizara inayohusika na ardhi.
Katika kuondosha mgongano kati ya Mkaazi huyo na wananchi waliopata hati za ujenzi wa nyumba zao kwenye eneo hiyo ambalo lilikuwa ni eka za Serikali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuagiza Kamanda wa Polisi Wilaya ya Wete kumchukulia hatua za kisheria mara moja mtu ye yote atakayerejea kuleta vurugu zinazohusiana na eneo hilo.
Balozi Seif alionya kwamba Serikali haitolipa fidia yoyote ya miti iliyooteshwa na Mkaazi huyo Bwana Bakari kwa vile aliamua kupanda miti kinyume na utaratibu wa Kiserikali.
“ Serikali haitakulipa chochote kwa vile ulilima na kupanda miti ndani ya shamba la serikali bila ya idhini ya vyombo vinavyohusika “. Alimuonya Mkaazi huyo.
Balozi Seif aliwataka Wananchi wote waliobahatika kupata viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kudumu katika eneo hilo kufuata taratibu zote za ukataji wa miti kwenye viwanja vyao.
Mapema Afisa mdhamini Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Nd. Hemed Salum alisema eneo hilo lilikuwa likitumiwa na mzee Ali Luswerere baada ya kukatiwa eka na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Nd. Hemed alisema Bwana Bakari alipata mwanya wa kuanza kulitumia shamba hilo baada yam zee Swerere kushindwa kuliendesha kutokana na kupitwa na umri pamoja na uwezo wa kuliendesha.
Hata hivyo Afisa Mdhamini huyo wa wizana ya Ardhi alieleza kwamba Wizara hiyo ilifikia uwamuzi wa eneo hilo kulikata vinja baada ya kuzunguukwa na makaazi ya watu pamoja na kupanuka kwa mahitaji ya viwanja kwa wanchi walio wengi wa maeneo hayo.
EmoticonEmoticon