Maswali 10 Ya Kujiuliza Kila Wakati, Kama Una Nia Ya Kuwa TAJIRI.

TOA THAMANI, UPATE PESA.
Wengi wetu mara nyingi huwa tuna nia ya kufikia mafanikio makubwa na hatimaye kuwa matajiri. Lakini, kwa bahati mbaya sana huwa pia hatujui tuanzie wapi hasa ili kufikia hilo lengo. Matokeo yake hujikuta tukifanya hiki mara kile bila kupata matokeo ya kutufikisha kwenye lengo husika.
Kwa kawaida, ili kuwa tajiri huwa zipo kanuni zake za msingi kabisa ambazo ukizifuata  ni lazima uwe tajiri. Kwa kutumia kanuni hizi huwa haijalishi wewe ni nani, unaishi kijijini au mjini, umesoma au hujasoma lakini ukizifuta ni lazima ufanikiwe na kuwa TAJIRI.
Kutokana na umuhimu wa hilo, leo hii ningependa nikushirikishe kanuni mojawapo itakayokusaidia kukufikisha kwenye UTAJIRI. Kanuni zingine tutaendelea kujifunza polepole katika makala zinazofuata  hapa kwenye mtandao huu wa DIRA YA MAFANIKIO.
Kanuni hii ambayo tunajifunza leo ni kanuni ya kujiuliza maswali ambayo yatakusaidia kufikia lengo lako. Hii ni kanuni ya msingi sana ambayo unatakiwa uitambue ipo na inafanya kazi. Je, unataka kujua kivipi? Twende pamoja nami, kujua maswali muhimu ya kujiuliza ili uwe TAJIRI.
1. Jiulize, ni kwanini unataka kuwa tajiri?
Hili linaweza likaonekana ni swali la kawaida sana kwako, lakini ni lazima uwe na sababu kwa nini unataka kuwa tajiri. Bila kuwa na sababu ya msingi inayokusukuma wewe kuwa tajiri huwezi  kupata msukumo utakaokufanya utafute pesa kwa nguvu zote hadi ufikie lengo hilo unalolitaka.
Hapa sio suala tu la kusema ‘Oooh nataka kuwa tajiri’ ni lazima ujue sababu ipi inayokufanya utake kuwa tajiri.  Je, unataka kuwa tajiri ili uwe huru kifedha? Au je, unataka kuwa tajiri ili kusaidia jamii inayokuzunguka? Ni muhimu sana kuwa na sababu yenye mashiko ili kufikia malengo yako.

TOA THAMANI, UPATE PESA.
2. Jiulize, una imani ya kutosha kukusaidia kufikia lengo lako?
Unaweza ukawa una sababu nzuri inayokufanya utake kuwa tajiri. Lakini hiyo peke yake haitoshi ni lazima uende hatua ya ziada kwa kujiuliza wewe  mwenyewe je, una imani ya kufikia malengo yako? Unaamini kabisa kwamba hayo malengo ya kuwa tajiri utayafikia?
Ili uweze kufanikiwa ni lazima kupima imani hii. Kumbuka hakuna mafanikio yanayoweza kuja pasipo kuhusisha imani hata iweje. Hapo ulipo kimaisha ni matokeo ya imani fulani hivi ambazo unazo au ulizibeba na kuziamini sana. Kwa imani hizo ndizo zimekufikisha hapo ulipo. Kupima imani, ni lazima sana kwako ili kufikia mafanikio.
3. Jiulize, ni tabia zipi za kimafanikio zitakazokusaidia kufanikiwa?
Najua tayari una sababu na imani ya  kukutosha kukupeleka kwenye utajiri. Kitu kingine kwako cha kujiuliza je, una tabia zipi za kimafanikio zenye uwezo wa kukufikisha kwenye mafanikio makubwa unayoyataka. Kama tabia hizi unazo upo kwenye njia sahihi.
Huwezi kuwa unasema unataka kuwa tajiri wakati huo huo una tabia mbaya zinazokurudisha nyuma kimafanikio. Tabia hizi zinaweza zikawa ukosefu wa nidhamu, matumizi mabaya ya pesa, muda na nyinginezo. Kwa kuendekeza tabia hizi na zinazofanana nazo hata ulie machozi ya damu huwezi kuwa tajiri.
4. Jiulize, je, unatoa thamani inayoendana na unachokitaka?
Kwa kawaida ili ufanikiwe ni lazima utoe thamani kwa jamii ili ikulipe pesa. Kama ni huduma fulani ipe jamii husika itakulipa tu hizo pesa hata kama umelala. Kinyume cha hapo, yaani nikiwa na maana kushindwa kutoa thamani huwezi kufanikiwa wala kupata pesa yoyote.
Sasa hapa ndipo unatakiwa jiulize je, wewe binafsi unatoa thamani kwa jamii. Nini ulichonacho  ambacho ni msaada kwa watu wengine. Kama huna kitu hiki unalazimika kukitafuta haraka sana vinginevyo huwezi kufanikiwa. Na ndiyo maana unalazimka kujiuliza kila wakati  ‘je, ninatoa  thamani’. Hii itakuwa njia bora sana kwako ya kuufikia utajiri.
5. Jiulize, una mipango imara ya kukufikisha kwenye utajiri?
Sawa, inawezekana una toa thamani inayotakiwa, lakini je una mipango imara ya kukufikisha kwenye lengo la mafanikio hayo makubwa. Hapa ili ufanikiwe ni lazima kwako uwe na mipango iliyo sawa ambayo unatakiwa uifate kila siku.
Na katika kuhakikisha hili linatimia ni vyema ukawa umejitengenezzea mpango wa siku, juma, mwezi na hata mwaka na utekelezaji unatakiwa uanze mara moja. Lakini bila ya kufanya hivi kufanikiwa na kuwa tajiri inaweza ikawa ndoto kama ndoto zingine. Kuwa na mipango imara ni nguzo imara ya kukufikisha kwenye utajiri.
6. Jiulize, je, una hofu zinakuzuia kufanikiwa?
Mara nyingi na kwa asilimia kubwa kinachomzuia binadam kufanikiawa si yale mambo ya nje tunayoyaona, hapana. Kitu kikubwa kinachomzuia binadamu kufanikiwa ni mambo yanayoendelea ndani yake ikiwamo pamoja na hofu.
Unapokuwa na hofu ni adui mkubwa sana wa mafanikio yako kwa ujumla. Acha kuruhusu hofu ikachukua nafasi kwenye moyo wako kwa nama yoyote ile. Kwa vyovyote vile kama utairuhusu hofu ni lazima itakurudisha nyuma. Hivyo inabidi ujifunze kukabiliana nayo mpaka kuweza kuishinda.
ZUNGUKWA NA WATU WENYE MAFANIKIO.
7. Jiulize, unazungukwa na watu wenye mafanikio?
Ukichunguza kidogo maisha ya watu wenye mafanikio, utagundua wanazungukwa na watu wenye mafanikio pia. Hapa ndipo ilipo pia siri ya kuufikia utajiri. Huwezi kufanikiwa kama wanaokuzunguka ni watu maskini na ambao maisha yao ya kushindwa siku zote.
Unataka kuwa tajiri, jiulize tu swali hili rahisi ‘ni watu gani wanao nizunguka? Ukiona umezungukwa na watu wengi maskini nakushauri kubadili mwelekeo haraka sana kutafuta watu wenzako wasaka mafanikio. Kwa kuwa na watu hawa watakutia moyo na kukupa hamasa ya kuendelea mbele.
8. Jiulize, uko tayari kujifunza?
Kama una nia ya kuwa TAJIRI lakini wakati huo huo hujajitoa kwenye kujifunza, sahau mafanikio hayo. Kujifunza kila siku iwe kwenye vitabu au pale tunapokosea ni jambo la msingi sana kwa msaka maendeleo yoyote yule. Bila kufanya hivi hakuna mafanikio.
Unashangaa, ndiyo huwezi kufanikiwa. Kitakachokufanya usifanikiwe kwa sababu utarudia makosa yake yale kila wakati na hutaweza kupiga hatua. Maisha ya watu wenye mafanikio ni ya kujifunza siku zote. Kwa hiyo kama unataka kuwa tajiri jiulize unajifunza. Kama hufanyi hivyo huwezi kupingana na ukweli mbio za kuelekea kwenye utajiri sio zako.
9. Jiulize, uko tayari kukubaliana na vizuizi?
Kwenye safari yoyote ya mafanikio changamoto huwa hazikosekani. Changamoto hizi usipokuwa makini nazo ni rahisi sana kuweza kukurudisha nyuma.  Sasa kitu cha kujiuliza hapa je, unapokutana na changamoto uko tayari kukabiliana nazo?
Jiulize ni mara ngapi ulishindwa au uliona wengine wakishindwa kwa sababu ya changamoto? Hapa ndipo wewe unatakiwa uoneshe utofauti wa kuweza kukabiliana na changamoto. Amua tu kwamba utafanikiwa, hata kitokee kitu gani mbele yake lazima ukishinde.
10. Jiulize, una tabia ya kutathmini safari ya mafanikio yako?
Hakuna mafanikio ambayo unaweza ukayapata bila ya kujiwekea tathmini. Ni lazima kujiuliza na kutathmini safari nzima ya mafanikio yako? Kama hufanyi hivo unatakiwa kuanza mara moja. Utayafikia mafanikio yako kwa kujiwekea tathmini kila wakati?
Anza kujiwekea tathmini ya siku, kisha jiwekee tathmini ya juma hata mwezi. Kwa kufanya hivyo utaboresha sana maisha yako. Hiyo itakusaidia kurekebisha yale maeneo ambayo hujafanyi vizuri na kujiweka sasa kwenye nafasi nzuri ya kuendelea mbele kimafanikio.

Je, una nia, hamasa na shauku kubwa ya kuufikia UTAJIRI? Kama jibu ni ndiyo jifunze kutumia mbinu hii kwa kujiuliza maswali yatakayokusaidia kuufikia UTAJIRI.

Ni wako rafiki,
Imani Ngwangwalu,
Simu; 0713 048035,
Blog; dirayamafanikio.blogspot.com
Previous
Next Post »