Rais Paul Kagame amewasha mwenge wa maombolezo utakaowaka siku 100 kukumbuka mauaji ya kimbari

Rwanda leo inakumbuka miaka 20 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari ambapo watu 800,000 waliuawa, huku nchi hiyo ikiituhumu Ufaransa kwa kuhusika na mauaji hayo.
 Rais Paul Kagame, amewasha mwenge wa maombolezo utakaowaka kwa siku 100, muda ambao uliwachukua wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa Kihutu kuwaua maelfu ya watu, wengi wao wakiwa Watusti na wahutu wenye msimamo wa wastani
Shughuli za kuweka mashada ya maua zimefanyika katika uwanja wa mpira wa Kigali, katika kumbukumbu iliyohudhuriwa  na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon na viongozi kadhaa wa Afrika.
Rais Barack Obama wa Marekani ametoa heshima zake kwa wahanga wa mauaji hayo na kuitaka jamii ya kimataifa kuchagua upendo badala ya chuki.
 Akizungumzia mauaji hayo yaliyoitikisa dunia, Rais Obama amesisitiza kuwa mauaji ya kimbari hayakuwa ajali wala jambo lisiloepukika.
Wakati huo huo, balozi wa Ufaransa nchini Rwanda, Michel Flesch amesema amezuiwa kuhudhuria kumbukumbu hiyo, kufuatia  mzozo wa kidiplomasia wa Rwanda kuituhumu  Ufaransa  kwamba ilishiriki kwenye mauaji hayo ya mwaka 1994.
Previous
Next Post »