TAARIFA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA




Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.
KUPATIKANA NA DAWA ZA KULEVYA [BHANGI]

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuanzia tarehe 30.04.2017 hadi tarehe 01.05.2017 lilifanya msako katika maeneo Manga, Uyole Jijini Mbeya na maeneo ya Kitongoji cha Iponjola, kijiji cha Isuba, kata ya Kisondela, tarafa Pakati, Wilaya ya Rungwe. Katika Msako huo uliolenga kukamata watu wanaojihusisha na uuzaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya, Watuhumiwa 03 walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi yenye uzito wa Kilogram 35 na Gram 55.
Watuhumiwa waliokamatwa wametambulika kwa majina ya:-
GOODLUCK GEOFREY [16] Mkazi wa Manga Jijini Mbeya
JAMES S/O MWASEBA [22] Mkazi wa Manga Jijini Mbeya
KISA SHABAN [26] Mkazi wa Kasumulu Wilaya ya Kyela

Watuhumiwa ni wauzaji na wasambazaji wa dawa hizo za kulevya na watafikishwa Mahakamani mara baada ya Upelelezi kukamilika.

KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI [MENO YA TEMBO]

Mnamo tarehe 30.04.2017 majira ya saa 08:30 Asubuhi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko katika maeneo ya Uyole, Kata ya Iganjo, Tarafa ya Iyunga Jiji na Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la MAIKO KIWAGE [39] Mkazi wa Isyesye akiwa na vipande vitatu vya meno ya tembo.Mtuhumiwa alikutwa na nyara hizo za Serikali ambazo alikuwa amezihifadhi ndani ya nyumba yake na baada ya kumkamata na upekuzi kufanya ndipo zilionekana. Ikumbukwe mnamo tarehe 24.04.2017 huko Kijiji cha Lyangadupa, Kata na Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya watuhumiwa wawili walikamatwa wakiwa na meno mawili ya Tembo.Upelelezi unaendelea ili kubaini mtandao mzima unaojishughulisha na uwindaji haramu pamoja na biashara haramu ya Nyara za Serikali ikiwani pamoja na Meno ya Tembo na Pembe za Faru.Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo Kumekuwa na tukio 01 la mauaji kama ifuatavyo:-Mnamo tarehe 01.05.2017 majira ya saa 10:30 Asubuhi huko katika Kijiji na Kata ya Mjele, Tarafa Usongwe, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja ambaye amefahamika kwa jina la SIKITU MWAWALA [25] Mkazi wa Kijiji cha Ijenga aliuawa kwa kupigwa na kundi la wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi na kisha mwili wake kuchomwa moto. Inadaiwa kuwa chanzo cha kifo chake ni kipigo kilichotokana na kulipiza kisasi kufuatia marehemu na wenzake kuhusika katika tukio la mauaji ya mwanamke aitwaye ZAITUNI SAISONI [20] Mkazi wa Kijiji cha Katusi kilichotokea tarehe 25.04.2017 majira ya saa 11:00 Asubuhi huko katika Kitongoji cha Kitusi, Kijiji na Kata Mjele ambaye baada ya kumuua walichukua baadhi ya viungo vyake ikiwemo matiti, masikio, macho na ngozi ya paji la uso kwa imani za ushirikina.



Marehemu alihusika kwenye tukio hilo ambalo walilitenda pamoja na wenzake wawili ambao mmoja kati yao amekamatwa na pia mmoja kati ya watuhumiwa ni mume wa marehemu ZAITUNI SAISONI aitwaye MATESO WILLISON [30] Mkazi wa Mjele.



Aidha katika tukio hilo zilikamatwa bunduki mbili aina ya Gobole na golori 36 na unga wa milipuko ambazo moja kati ya bunduki hizo ni ya mali ya marehemu aitwaye SIKITU MWAWALA na nyingine ni ya mtuhumiwa ambaye amekiri kuwa ni ya kwake.



Marehemu pamoja na wenzake wametajwa kuhusika katika matukio ya Unyang’anyi wa kutumia silaha, utekaji katika eneo la Msangamwelu na Mjele na pia wamekuwa wakikodishwa katika matukio ya mauaji.

WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wajenge tabia ya kuwafikisha watuhumiwa wanaowakamata kwa tuhuma mbalimbali katika mamlaka husika kwa hatua zaidi ya kisheria. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kuacha mara moja kujihusisha na uwindaji haramu, biashara haramu ya meno ya tembo pamoja na uuzaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya kwani ni kinyume cha sheria.


Imesainiwa na:

[DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA
Previous
Next Post »