Na:
Meshack Maganga-Iringa.
Katika
makala yangu ya ‘Uwezo Wa Kujua Kama
Tutakufa Maskini Tunao’, nilizungumzia kwa kirefu uwezo wa binadamu hasa katika
mawazo yake ya kina. Baadhi ya wasomaji walitoa maoni yao kwa barua pepe, na
wengine walitoa maoni yao kwenye ukurasa wa maoni wa MjengwaBlog. Napenda
kuwashukuru walionishauri, na maoni yao ndiyo yaliyo pelekea kuzaa mada ya leo
ambayo ni ya wiki hii.
Aidha,wiki
iliyopita pamoja na mambo mengine, nilibahatika kusoma vitabu na makala
mbalimbali,moja ya makala niliyoisoma ni ile ya mwandishi maarufu Jack Canfield
aliye andika kitabu kinacho tamba
duniani katika ‘sheria ya mvuto’ (The law of attraction) kiitwacho ‘The Success
Principles’. Kwenye moja ya makala yake Jack Canfield anasema, watu wote wenye mafanikio duniani,
ambao huonekana kana kwamba wamebarikiwa hutafuta maana ya wao kuwa wao, uwezo
wao wa kipekee na kutumia upekee walionao na kuishi maisha yao kimafanikio watakavyo
wao. Dunia hii inayo nafasi kwa mwanadamu ambaye anatafuta maana ya maisha yake
mwenyewe, haijalishi umezaliwa katika familia ya aina gani bali ukikubali
ukweli kuwa unayo hazina ya maisha ndani yako basi maisha yako yatapata maana.
Katika makala hii ya
leo,nitazungumzia juu ya tabia zetu na maamuzi yetu mabalimbali ambayo hutuletea
taaifa ‘feedback’ ambazo wengi wetu huziita mikosi au bahati mbaya.
Kuna makala moja nimeisoma,
inasema hivi ‘Siku hizi kuna virusi va HIV ambavyo vinahesabiwa kama maadui wa
watu wote. Kila kona hapa duniani kuna juhudi za kila aina katika kupambana na
virusi hivi. Ukimuuliza mtu atakwambia, virusi hawa ndiyo adui zetu katika
suala la maradhi haya, lakini je, kuna ukweli wowote katika hili? Kila mtu
anafahamu vizuri mazingira ya aina mbalimbali ambayo kwake huyaita adui, kila
mtu anawafahamu watu wa aina mbalimbali ambao kwake kwa sababu mbalimbali
anawaita adui zake na kila mtu anafahamu vizuri vitu Fulani maalum ambavyo kwa
sababu Fulani anaviita na kuamini kwamba ni adui zake.”
Lakini huenda hakuna ambaye
anajua ni kwa kiasi gani tabia, mienendo na mawazo yake ni adui zake wakubwa.
Ni mara chache sana na ni watu wachache sana ambao wako tayari kujiuliza na
kukiri kwamba, tabia mienendo na mawazo yao kwa kiasi kikubwa sana huenda
vinawadhuru na kuwaumiza, kuwaharibia mipango yao na maisha kwa ujumla, kuliko
wanvyodhani kwamba athari hizo hutoka nje yao.
Ni wachache kwa sababu,
binadamu hujipenda sana kiasi ambacho huogopa kufunua macho zaidi na kuukabili
udhaifu alionao. Ukweli ni kwamba, kama mtu atataka kuishi bila kujidanganya,
atagundua kuwa hata mbu na virusi vya ukimwi siyo adui zetu. Atagundua kwamba,
tabia mienendo na mawazo yetu ndiyo adui zetu. Kama mtu ataamua kujikinga dhidi
ya mambo yote yanayoweza kumwambukiza virusi vya ukimwi au kuishi katika
mazingira ya mbu wengi na kuchukua
tahadhari dhidi ya wadudu hao, anakuwa amemkwepa kwa karibu asilimia
tisini huyu au hawa anaowaita adui zake.
Kila siku, hata pale ambapo
tunatangaza kwamba akina Fulani na
Fulani ni adui zetu, huwa tunafanya hivyo kwa makosa kwa sababu tu ya kujipenda
na hivyo kujipendelea katika kuutazama ukweli. Tunapofilisika tunajitahidi sana
kutafuta maadui wa hali hiyo, huku tukiwa tumesahau kwamba tabia zetu ndizo zilizotufilisi.
Kwenye
kitabu chake cha ‘Kichwa chako ni Dhahabu’, Geoffrey Tenganamba anasema kuwa, Janga kubwa duniani si kifo wala ajali, Bali Ni maisha ya
mwanadamu aliyekubali kuishi maisha ya bora liende, asiyetaka kubadilika Na
kukua, anayeishi leo kama jana na atakayeishi kesho kama leo.
Tunaposhindwa kupata
tunachokitafuta maishani, hatuzitazami tabia, mitazamo, mienendo, imani na
mawazo yetu, bali tunatazama nje yetu ili kumpata adui. Ilivyo ni kwamba, kama
tunamtafuta adui, kwa sababu tunataka kumpata ni Lazima tutampata. Hivyo
tukishampata tutaamini kabisa kwamba huyu ni adui yetu na kuziweka nguvu zetu
hapo kujaribu kupambana naye.
Inachukua muda, na wakati
huo tunakuwa tumechelewa sana tunapokuja kugundua kwamba tuliyemdhani ni adui
alikuwa ndani mwetu. Lakini kwa bahati mbaya sana ni kwamba huwa hatufanikiwi
kung’amua kwamba huyu tunayedhani ni adui yetu siyo adui yetu. Kwa hali hiyo,
huwa tunaishi katika dhiki, misukosuko na nuksi zisizokwisha tukijaribu
kupambana na adui ambaye siyo, huku adui yetu akiwa ni sisi wenyewe. Kupigana
huku na adui asiyekuwepo popote bali ndani mwetu huweza hata kutupotezea maisha
yetu.
Kwa nini basi kabla
hatujatangaza au kudhani Fulani ndiye adui yetu, tusitazame au kuzikagua kwamba
tabia zetu, mienendo, imani na mawazo yetu? Wanasema wataalamu wa Nyanja zote
za kimaisha katika nadharia zao nyingi kuhusu maisha kwamba, adui wa mtu ni mtu mwenyewe.
Eckhart Tolle, katika kitabu
chake cha ‘The Power Of Now’ anasema
kuwa, watu wengi hawabadiliki kwasababu wamefungwa, na ni watumwa wa mifumo ya
zamani, yenye akili ileile, kanuni zilezile, mawazo yaleyale, tamaduni
zilezile, vipato vilevile na vipimo vilevile.watu wa aina hii wanatembea lakini
hawaishi. ‘Sikiliza zauti
za dunia lakini sikiliza sana sauti yako ya ndani kwani’...ITAENDELEA
Tanzania
inahitaji watanzania wanaoweza kujitambulisha kama wao, waliotayari kuishi kama
wao wanaotengeneza mifumo mipya, vipimo vipya,ramani mpya na mageuzi
mapya.
Tusipojitazama kwa makini tutajikuta kila siku tukizidi kuongeza idadi ya
maadui huku hali zetu kielimu, kiuchumi na kijamii kwa ujumla zikizidi kudorora.
Zitazidi
kudorora kwa sababu Yule tunayemdhani ni adui yetu atatupotezea muda wetu na
kutusumbua sana, wakati adui yetu tunaye ndani mwetu na tunaweza kumuondoa kwa
saa kadhaa tu kama tutamgundua.
Kwa nini huwa ni vigumu
kwetu kumjua au kumgundua adui yetu pale mambo yetu yanaposhindwa kwenda kama
tulivyotarajia au kutaka? Ni kwa sababu tumefundishwa na mazoea kwamba sisi ni
vitu vilivyo nje yetu na hivyo, kusimama au kuanguka katika maisha yetu
hutegemea wengine na mazingira ya nje yetu. Tunapopata fedha na kuzitumia
vibaya, hatujikagui na kujiuliza kama chanzo cha kufikia hatua hiyo siyo sisi
wenyewe, bali tunaanza kuwaambia wake
zetu kwamba wana nuksi au kuwasingizia jirani zetu kwamba wametuendea kwa
waganga kutuharibia bahati zetu.
Tunapotoka nje kwenye ndoa
zetu na kufanya uzinzi, hatuko tayari kujikagua ili kuuona ukweli, bali
tunachoweza kufanya ni kuwasingizia wake au waume zetu kwamba wao ndio chanzo
kwa sababu hawatujali, kwa sababu ni dhaifu wa tendo la ndoa au kwa sababu
hawana fedha. Ni vigumu kwetu kujiuliza
kama sisi siyo chanzo au kujiuliza mchango wetu kwenye suala zima. Tunajipenda
sana na kuamini kwamba sisi ni watu na vitu vinavyotuzunguka.
Tunapopoteza kazi zetu
hatujikagui kama sisi wenyewe hatukuchangia kufukuzwa huko, kwani adui zetu
siku zote wako nje yetu na ni Lazima tutawatafuta. Tunaweza kumnyooshea kidole
cha lawama bosi wetu au walio chini yetu, tunaweza kudai kwamba nijirani au
ndugu zetu ambao ati siku zote hawakuwa wakifurahia mafanikio yetu.
Ndiyo ubaya wa kujipenda na
kuamini kwamba adui zetu wako nje yetu na ni Lazima kila linalokwenda kinyume
na matarajio yetu liwe limesababishwa na watu hao au mazingira hayo. Umefika
wakati ambapo inabidi tubadilike sana na kuanza kuujua ukweli kwamba sisi
ndiyo waamuzi na waendeshaji wa maisha yetu. Kila linalotutokea ni matokeo ya
tabia, mienendo na mawazo yetu.
meshackmaganga@gmail.com 0713 48 66
36
EmoticonEmoticon