MAKALA LEO:KWENYE UJASIRIAMALI NG’OMBE WA MASIKINI HUZAA (1)

              
Na: Meshack Maganga- Iringa

Katika makala zangu zilizo tangulia nilipoandika kuhusu ujasiriamali nilipata mwitikio kwa kiwango kikubwa kutoka kwa wasomaji wengi. Baadhi walinitafuta kutaka ushauri wa mazungumzo ya ana kwa ana kuhusu dhana hii tunayoiita ujasiria mali.
Baadhi ya wasomaji wameenda mbali sana na kunisisitiza niandike kitabu kinacho husu  ujasiriamali,ninapenda kuwaahidi wasomaji wa Mjengwa Blog kwamba kitabu kipo njiani kinakuja.Tuombe uzima.
Kuna kanuni inayofanya kazi hapa duniani, ipo na ukubali usikubali ipo, uamini usiamini ipo, uelewe usielewe ipo.  
Ukifikiri kuhusu maisha ya hapa duniani hasa kwa kuangalia mfumo wa maisha kwa kila binadamu tukianzia kwa walemavu,ombaomba,maskini,wagonjwa,vichaa,wanaohangaika usiku na mchana kwaajili ya chakula tu na nguo za kuficha utupu wao na makundi mengine lazima utafika mbali sana na kufika mahali na kukubali kuwa kuna kitu hakijakamilika katika maisha ya hapa duniani.  Au unaweza kuhisi kana kwamba dunia hii ina mapungufu sana.Najua kwa mwingine anaweza kusema hayo yote ni mipango ya Mungu na kuishia hapo.

Ukifikifiri tena kuhusu matajiri wa dunia hii akina Reginald Mengi, Yusuf Manji, Billgates, Carlos Slim,marehemu Steve Jobs, warren Buffet,   Bernard Arnault na Larry Ellison lazima utajikuta kuwa kuna shida kuelewa hiyo mipango au majaliwa ambayo wengi huamini kuwa ni ya Mungu kwa  watu hawa huwa kama walivyo. Hebu turudi katika uhalisia wa maisha.

Fikiri kuhusu nchi za Afrika zenye kila rasilimali zenye utajiri kupita kipimo lakini bado zinashika mkia katika umaskini duniani, nayo hiyo kama unaamini tuseme ni mipango ya Mungu Juzi, ijumaa nilikuwa pale Manzese BIG BROTHER, nikimsubiri rafiki yangu,nilianza kusoma  kitabu cha rafiki yangu Tenganamba, ana sema kuwa, katika kuishi kwangu duniani kwa kipindi kifupi tu nimejikuta napingana na kauli hizo zilizo  zoeleka kama: Ng’ombe wa Maskini hazai, kupata ni majaliwa,asiyekubali kushindwa si mshindani,maisha ni bahati,kisicho riziki hakiliki, maskini akipata makalio hulia mbwata, na nyingine nyingi zinazosisitiza kukubali matokeo madogo  bila ubishi wowote.

Mfumo na imani potofu kama hizi ndio ulionisukuma mpaka nikaandika makala nyingi kwenye gazeti hili na pia katika mitandao ya kijamii hasa Mjengwablog makala zimenikutanisha na wadau mbalimbali wa ujasiriamali kutoka ndani na nje ya mkoa wa Iringa.
Kutokana na hilo nadiriki kusema kuwa hapa duniani lazima kuna kanuni inayofanya kazi, haiwezekani binadamu wengine waishi maisha mazuri  halafu wengine tukubali kuwa ni mapenzi ya Mungu wao tu kuwa walivyo wakati wengine kulala chini ya madaraja ya Ubungo bila chakula.
Kuna kanuni inafanya kazi hapa duniani, ipo na ukubali usikubali ipo, uamini usiamini ipo, uelewe usielewe ipo .Nilipokuwa nasoma historia ya watu maarufu duniani kama akina Lincoln, Pluto, Tiger Woods, Billgates, Einstein, Hugo na wengine nilikubaliana na ukweli kuwa lazima kuna siri ya kanuni ya kuishi waliyokuwa wanaijua ambayo binadamu wengi duniani hawaitambui. Sikubali na haiwezekani kuamini kuwa mafanikio yao yalikuja kama ajali lazima kuna kanuni inayofanya kazi duniani waliijua mapema.
Na huu ukweli inabidi kila binadamu ajue, na kanuni hiyo ipo ndani ya kila binadamu na kila binadamu anayo.Jamani tuchoke kusikia mafundisho ya kutumaliza na kutudumaza kiakili kuna siri ya kanuni na hii iwekwe wazi ijulikane.
Kimsingi, ujasiriamali Tanzania umeshika kasi miaka ya 2000, hasa kutokana na juhudi za Serikali ya awamu ya tatu ya Mh. Benjamin Mkapa aliyeruhusu uwekezaji na ndipo msamiati wa Utandawazi uliposhika kasi na kuboreshwa na sera na sheria mbalimbali za uchumi kwa mfano, sera ya maendeleo ya biashara ndogo ndogo.
 Kutokana na hili, tumeshuhudia watu wengi wakijitoa kimasomaso kuanzisha biashara au kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali. David McClelland ambaye ni mwanasaikolojia kutoka chuo kikuu cha Havard nchini Marekani aligundua tabia za kisaikolojia zinazojengeka ndani ya mjasiriamali ambaye amefanikiwa kibiashara. Akifafanua hoja yake msaikolojia huyo alisema, wajasiriamali waliofanikiwa huwa na hamasa, malengo na huwa tayari kutumia muda wao kufanya kile anacho kitaka.
Msamiati huu ulianza kutumiwa kwa mara ya kwanza na mwana uchumi maarufu Richard Cantillon wa Ufaransa mwaka 1755 na baadaye ulipata mashiko kuanzia miaka ya 1800 ambapo wafanya biashara wenye mitaji mikubwa “mechants” kutoka  Ulaya walipoanza kuzunguka dunia  wakitafuta malighafi na madini kwa ajili ya viwanda vyao binafsi na vile vya makampuni yao.
Katika kipindi cha zama za kwanza za mawe (Hunter-Gatherer au miaka ya barafu) Jamii iliishi kwa kutegemea uwindaji na kukusanya matunda,Jamii iliishi katika makundi madogo madogo ya watu hasa koo zenye nasaba moja. Watu wote walikuwa sawa,iwapo alitokea mmoja wa Jamii akawa chifu au  mkuu wa kaya bado hakuonesha tofauti yoyote na wenzake,mkuu wa kabila au chifu hakumiliki mali nyingi na wala hakuwa milionea.
Baada ya kipindi hicho kikaja kipindi cha Mapinduzi ya kilimo katika kipindi hiki binadamu alianza kulima na kufuga aliwekeza nguvu zaidi na alipata mafanikio makubwa na aliyefanya uzembe  wa roho na mwili aliishia kuwa mlalamishi (tunajua kwamba mlalamishi siku zote hupata ulalamishi).
Kipindi kingine ambacho ndio kiini hasa cha makala haya ni kile cha ya mapinduzi ya  Viwandani kilikuwa kipindi kutoka karne ya 18 hadi karne ya 19 ambapo mabadiliko makubwa katika kilimo, utengenezaji wa bidhaa, uchimbaji wa madini, na uchukuzi yalikuwa na matokeo makubwa kwa hali ya kiuchumi, kijamii na ya kitamaduni ikianzia Uingereza, na hatimaye kuenea Ulaya nzima, Marekani ya Kaskazini, na mwishowe Duniani kote. Mwanzo wa Mapinduzi ya viwanda ulidokeza mabadiliko muhimu katika historia ya kibinadamu; karibu kila kipengele cha maisha ya kila siku hatimaye yaliathirika kwa njia fulani.
Mwanzo wa wakati wa mwisho wa Karne ya 18 mabadiliko katika baadhi ya sehemu za Uingereza yalianza na kazi ambazo hapo awali zilikuwa za mkononi na uchumi uliotumia wanyama kuendesha kazi kulibadilishwa na uundaji bidhaa uliotegemea mashine. Ilianza na utumizi wa mashine katika viwanda vya nguo, uundaji kwa mbinu za kutengeneza chuma na kuzidi kutegemea makaa ya mawe yaliyosafishwa.
Upanuzi wa biashara na ujasiriamali uliwezeshwa na kuanzishwa kwa mifereji, uboreshaji wa barabara na reli. Kuvumbuliwa kwa nguvu za mvuke kulikowezeshwa hasa na makaa ya mawe, utumizi mwingi wa gurudumu la maji na mashine za nguvu (hasa katika kutengeneza nguo) kulisisimua kuongeza kiwango   na uwezo wa uzalishaji mali
 Kuundwa kwa vifaa vya mashine ambavyo vilikuwa vya chuma pekee katika miongo miwili ya kwanza ya karne ya 19 kuliwezesha kutengenezwa kwa mashine zaidi za kuunda vifaa katika viwanda vingine. Matokeo yalienea kote katika Ulaya ya Magharibi na Marekani ya Kaskazini wakati wa karne ya 19, na hatimaye kuathiri karibu Dunia yote, mchakato ambao unaendelea katika kuenea kwa viwanda. Athari ya matokeo kwa jamii ilikuwa kubwa sana.
Mapinduzi ya Viwanda ya Kwanza, ambayo yalianza katika karne ya 18, yaliingia katika Mapinduzi ya Pili ya Viwanda mnamo mwaka wa 1850, ambapo maendeleo ya kiteknolojia na kiuchumi yalizidi kuendelea huku meli zinazotumia mvuke, reli, na baadaye katika karne ya 19 injini ya mwako wa ndani na uzalishaji wa nguvu za umeme. Urefu wa Mapinduzi ya Viwanda unatofautiana na wanahistoria mbalimbali. ITAENDELEA
              meshackmaganga@gmail.com



Previous
Next Post »