KAIMU katibu M kuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na serikali za mitaa(TAMISEMI, Jumanne Sagini, ameyanyoshea kidole Mashirika ya Tanesco, TTCL na Mamlaka za Maji katika Halmashauri mbalimbali nchini kuwa ni chanzo cha kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kutokana na kutoondoa miundombinu yake kwenye maeneo inakopita miradi hiyo.

Sagini alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa nne wa tathimini wa utekelezaji wa miradi hiyo uliofanyika Jijini Mbeya ambapo mkutano huo pia ushirikisha wakurugenzi na wakuu wa Idara wa Halmashauri nane nchini.

 Alisema kuwa kutokana na ucheleweshaji huo Sagini aliwataka wakuu wa idara husika na miundombinu yao kuondoa haraka ili kupisha miradi hiyo na kutekelezwa na kumalizika kwa wakati uliopangwa.

“Naagiza kwamba wakuu wa mashirika yote niliyoyataja hap kwa kushirikiana na Halmashauri, katika maeneo husika wakutanishwe na wakuu wa mikoa ili miundombinu hiyo iweze kuondolewa haraka”alisema na kuongeza.

 “Tunataka utekelezaji wa miradi hii tunayofadhiliwa na Benki ya Dunia ufanyike haraka na kuweza kukamilika kwa wakati,” alisema Sagini.

 Mtaalam wa Miji na Majiji wa Benki ya Dunia, Martin Onyach Olaa alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo nchini umefikia wastani wa asilimia 50 na kwamba anaamini kuwa kama vikwazo vidogovidogo vilivyopo vitaondolewa kazi hiyo inaweza kumalizika kwa wakati.

 Alisema kuwa miradi hiyo ina lengo la kuwasaidia wananchi kujikwamua na umasiki na kuwaletea maisha bora kama ambavyo dira ya mwaka 2025 inavyoelekeza.

 Miradi hiyo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia inatekelezwa katika Halmashauri za majiji ya Mbeya, Mwanza, Tanga na Arusha na kwenye Halmashauri za Manispaa ya Mtwara Mikindani, Moshi, Dodoma na Kigoma Ujiji.


Previous
Next Post »