Sekta
za kifedha zinazohusika na utoaji wa mikopo nchini zimetakiwa kutenga
utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali wa wadogo, kati na wakubwa ili kuleta
unafuu wa masharti ya ukopaji. Hayo yalisemwa katika kilele cha mafunzo
ya Wiki ya Huduma ya Kifedha na Uwekezaji na Waziri wa Sera, Bunge,
Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama alipokuwa anafunga siku
ya mwisho ya mafunzo hayo Agosti 27.
Mhagama
alisema kuwa mafunzo kwa wajasiriamali yamekuwa yakitolewa mara kwa
mara ila kikwazo kimekuwa ni mkopo hususani kwa wajasiriamali wanaoenda
kukopa masharti wanashindwa yakiwemo uwekaji wa hati ya nyumba kama
dhamana na riba kubwa.
“Tanzania
kuna takribani wajasiriamali milioni tano, ila wengi wao wanashindwa
kupiga hatua kutokana na masharti mazito ya mikopo, mfano mama anauza
vitumbua unamwamabia alete hati ya nyumba na wakati kapanga chumba
kimoja” Alisema Mhagama.
Alieleza
kuwa banki na wadau wote wa maendeleo wakutane ili kujadili ni namna
gani wanavyoweza kupunguza masharti kwa wajasiriamali wadogo ili
kuwakomboa na kupunguza tatizo la ajira na umasikini nchini. Mhagama
ambae pia ni Mbunge
wa Peramiho alisema kuwa Serikali itakuwa tayari kufanya majadiliano
kuona namna ya kumsaidia mjasiriamali mdogo na wa kati huku akiwapongeza
Banki ya Finca kwa kupunguza gharama za ukopaji kwa wananchi.
Meneja Masoko na Afisa Mahusiano wa Bank ya Finca, Spacio Aboubakar
alisema walijitahidi kufatilia vikwazo vyote vinavyowakwamisha
wajasiriamali na kuvifanyia kazi na kwa sasa kuna unafuu mkubwa wa
masharti kwa mkopaji na ulipaji wa riba. Banki ya Finca imekuwa mkombozi
kwa wajasiriamali nchini katika maonyesho hayo walifanikiwa kusajili
zaidi ya wajasiriamali 4000 wapya.
Katika
mafunzo hayo wajasiriamali kutoka vikundi mbalimbali vilishiriki
ikiwemo Vikoba pia washindi walikabidhiwa fedha taslimu laki tano ili kuwapa motisha wajasiriamali wengine
kushiriki miaka inayofata. Nuru Salim ni mmoja wa washindi wa zoezi
lililofanywa na banki ya Finca na kuibuka mshindi alisema wamama
wajitokeze kwa wingi kujifunza na kupata elimu ya uwekezaji na
ujasiriamali ili kuepukana na tatizo la kuwa tegemezi.
“Mimi
najihusisha na uuzaji wa nguo za wanawake Kariakoo, ila hapohapo nauza
vitafunwa ninavyotengeza mwenyewe kama vitumbua ila nimekuja hapa
kuongeza vitu vipya” Aleleza Nuru.
Maonyesho
hayo yalikuwa ya tano na huwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta za
banki, bima na uwekezaji kutoa elimu kwa wajasiriamali zaidi ya 20,000
na muitikio mkubwa ulikuwa wa wamama kuliko vijana na wanaume.
Mwandishi: Muyonga Jumanne (Mwananchi)
EmoticonEmoticon