LAFARGE TANZANIA YATOA SARUJI MIFUKO ZAIDI YA 1,000 KUJENGA UPYA MABWENI SEKONDARI YA IYUNGA.

Meneja Rasilimali Watu wa kampuni ya saruji ya Lafarge ya jijini Mbeya Bryson Tarimo akizungumza mara baada ya kukabidhi mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya shule ya Sekondari Iyunga ambayo hivi karibuni yaliteketea kwa moto,Kampuni ya Lafarge imetoa mifuko ya saruji yenye thamani ya shilingi milioni 14. Mkuu wa shule ya sekondari ya Iyunga Edward Mwantimo akitoa neno la shukrani mara baada ya kukabidhiwa mifuko 1,000 ya saruji kutoka kampuni ya Lafarge ya jijini Mbeya kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya shule ya Sekondari Iyunga ambayo hivi karibuni yaliteketea kwa moto ambapo pia alielezea madhara yaliyotokana na moto uliosababisha kuungua kwa mabweni ya wanafunzi wa shule hiyo. Viongozi wa kampuni ya saruji ya Lafarge wakiwa pamoja na watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya wakati wa kukabidhi mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya mabweni yaliyoteketea ya shule ya Sekondari Iyunga. Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Dkt. Samwel Lazaro(kushoto) akipokea mifuko 1000 ya saruji kutoka kwa Meneja Uajiri watu wa kampuni ya saruji ya Lafarge Bryson Tarimo kwa ajili ujenzi wa mabweni ya shule ya Iyunga yaliyoteketea kwa moto hivi karibuni.
 Kampuni ya Saruji ya Lafarge Tanzania (Mbeya Cement Company) imetoa msaada wa zaidi ya mifuko 1,000 ya saruji na vifaa vingine vya ujenzi kwa shule ya Sekondari ya Iyunga mkoani Mbeya kufuatia mabweni ya shule hiyo kuungua moto hivi karibuni.
Mashine ya kampuni hiyo pia itatumika kufyatua zaidi ya matofali 40, 000 yanayohitajika kukamilisha ujenzi huo na kufanya jumla ya msaada huo kuwa na thamani ya shilingi 14 milioni. Akizungumza kwenye makabidhiano ya msaada huo, Meneja Rasilimali Watu wa Lafarge Tanzania, Bryson Tarimo alisema “tulipata habari za kushtusha kuhusiana na tukio la moto ambao uliteketeza miundombinu ya shule pamoja na mali za wanafunzi.
Tunatambua kwamba huu umekuwa ni wakati mgumu kwa uongozi wa shule pamoja na wanafunzi.” Aliongeza kusema kwamba Lafarge inaamini kwamba elimu ni muhimu kwa maendeleo ya mustakabali wa Tanzania na pia kwamba elimu itasaidia kufungua mianya ya fursa mbalimbali kwa Watanzania. Tarimo alieleza kwamba Lafarge ina jukumu la kujenga mabweni hayo ili kuwarudishia wanafunzi wa Sekondari ya Iyunga mazingira mazuri ya kujisomea. “Hii ni sehemu ya jukumu letu kuifikia jamii na kuisaidia jamii pamoja na taasisi mbalimbali zilizopo mahali tunapofanyia kazi.”
 Aliongeza: “Uhusiano wetu na shule hii ni mkubwa sana kwa sababu tunaelewa imewafundisha baadhi ya watu ambao hivi sasa wanaendesha kiwanda chetu na kutufanya tuendelee kuwa na mafanikio. Tunataka kuona wanafunzi wakirejea madarasani na walimu wakiendelea kutimiza majukumu yao kama kawaida kwani azma yetu ni kuona shule hii inapata mafanikio na kuwapa wanafunzi fursa ya kutimiza ndoto zao na kuwa na mustakabali mzuri.
Mtazamo wetu ni kuona Tanzania ikiwa nchi inayotoa fursa ya elimu kwa kila mtoto ili watoto hawa wote kila mmoj aweze siku moja kuchangia maendeleo ya nchi hii.” Tarimo alisema kwamba Lafarge inajali maendeleo ya jamii na ina fahari kuweza kutoa msaada huu kwa shule ya Sekondari ya Iyunga kufuatia moto ulioteketeza mabweni ya shule hiyo.
Tunaamini msaada huu utarejesha hali ya kawaida katika shule hii na sisi kama sehemu ya jamii hii tunapenda kuona wanafunzi hawa wakiishi katika mazingira salama.” Tarimo aliyaomba makampuni mengine na taasisi mbalimbali, watu binafsi na jamii kwa ujumla kuisaidia ujenzi wa shule hiyo.
Previous
Next Post »