DARAJA LA KIGAMBONI KUFUNGULIWA RASMI APRILI


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akipata maelezo kutoka kwa Meneja Msimamizi wa ujenzi wa daraja la Kigamboni Eng. Karim Mattaka alipokagua daraja hilo leo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Meneja miradi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Eng. John Msemo wakati alipotembelea daraja la Kigamboni kuangalia ujenzi wa daraja la Kigamboni leo jijini Dar es salaam.
Mwonekano wa lango la kuingilia daraja la Kigamboni kwa upande wa Kigamboni, linavyoonekana pamoja na vyumba vya kukatia tiketi.
Mwonekano wa vyumba vya ofisi zitakazotumiwa na wasimamizi wa Daraja la Kigamboni.
Mwonekano wa daraja la Kigamboni ambalo litafunguliwa rasmi mwezi ujao.
Barabara za maingilio (inter change) ya Daraja la Kigamboni upande wa Kurasini.
 
 


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amesema daraja la Kigamboni litafunguliwa rasmi Aprili, 16 mwaka huu. Amesema kazi inayoendelea sasa hivi ni kupitisha magari maalum kwa ajili ya kupima ubora wa daraja hilo ili kujiridhisha kabla ya kukabidhiwa rasmi Serikalini.

Amewataka watumiaji wa daraja hilo kuwa waangalifu, kulinda miundombinu na kuepuka vitendo vya hujuma ili lidumu kwa muda mrefu. “Daraja hili lina urefu wa mita 640, barabara sita, tatu zinapanda na tatu zinashuka, hivyo tunawaomba wananchi watakaovuka kuzingatia usafi na ustaarabu”, amesema Profesa Mbarawa.

Amebainisha kuwa Serikali itaweka sheria kali kwa wote watakaokiuka matumizi sahihi ya daraja hilo na kusisitiza umuhimu wa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani wanapovuka katika daraja hilo.

Meneja Msimamizi wa ujenzi wa daraja hilo Eng. Karim Mattaka amesema wataalam wanaendelea na taratibu za kulipima daraja hilo ili kujiridhisha kama linamudu kupitisha uzito uliokusudiwa kabla ya kulikabidhi kwa Serikali mapema mwezi ujao.

Amesema awamu ya kwanza ya kulipima daraja hilo imekamilika na sasa wanaendelea na awamu ya pili hadi watakapomaliza awamu nne ili kujiridhisha kabla ya kuanza kutumika.

Takribani shilingi bilioni 216 zimetumika katika ujenzi wa daraja hilo linalotazamiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa abiria na magari katika kivuko cha Magogoni na Kigamboni.
Previous
Next Post »