Ufaulu wa
wanafunzi waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka
2015 mkoani Iringa umeongezeka ukilinganisha na mwaka jana, ambapo
ufaulu kwa mwaka huu ni asilimia 73.25, wakati mwaka jana ulikuwa ni
asilimia 68.58, sawa na ongezeko la asimilia 4.67.
Hayo
yalisemwa na Afisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Iringa, Euzebio Mtavangu
hivi karibuni wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa matokeo ya mtihani wa
kumaliza elimu ya msingi 2015 kwa wajumbe wa kamati ya uchaguzi wa mkoa
wa kuchagua wanafunzi wataojiunga kidato cha kwanza mwaka 2016.
Alisema
kuwa kuongezeka kwa ufaulu mwaka huu mkoani Iringa ni kutokana na
utekelezaji mzuri wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) ulioanzisha na
serikali hivi karibuni.
Alisema
kuwa wanafunzi waliofaulu mwaka 2015 ni 15,311 (7,163 wavulana na 8,148
wasichana) ambapo wanafunzi wote waliofaulu mwaka huu wamechaguliwa
kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016.
Katika
mwaka 2014 matokeo ya watahiniwa waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya
msingi walikuwa ni wanafunzi 14,650 (6,835 wavulana na 7,815
wasichana).
Mtavangu
aliongeza kuwa kwa mwaka 2015 wanafunzi 413 (258 wavulana na 155
wasichana) ambao ni asilimia mbili hawakufanya mtihani wakilinganishwa
na 177 (109 wavulana na 68 wasichana) ikiwa ni asilimia moja kwa mwaka
2014.
“Sababu
za wasiofanya mtihani ni utoro, vifo, ugonjwa, mimba na kuhama. Idadi ya
utoro kwa wanafunzi mwaka huu ni kubwa ukilinganisha na mwaka jana,
ambapo mwaka 2015 utoro ulikuwa ni wanafunzi 399 wakati mwaka 2014 utoro
kwa wanafunzi ulikuwa ni 158,” alisema.
Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ulifanyika tarehe 09-10 Septemba 2015 nchini kote.
Aidha,
alisema kuwa shule za msingi 467 kati ya shule 491 ndio zilizokuwa na
watahiniwa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2015 mkoani
Iringa.
Mtavangu
alisema kuwa watahiniwa waliofanya mtihani na kumaliza elimu ya msingi
2015 wanaendelea kujibu maswali ya mitihani kwa kutumia fomu za ‘Optical
Mark Reader’ (OMR).
Alisema
kuwa matumizi ya fomu za OMR yalianza mwaka 2012 na lengo la kutumia OMR
ni kusoma moja kwa moja kwa kompyuta majibu ya mtahiniwa kutoka katika
karatasi yake ya majibu na kuokoa muda wa usahihishaji.
Takwimu
za watahiniwa waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015
ni wanafunzi 20,905 (9,612 wavulana na 11,293 wasichana) na waliofaulu
ni jumla ya wanafunzi 15,311 (7163 wavulana na 8148 wasichana), sawa na
asilimia 73.25.
Hata
hivyo, kiwango cha kumaliza elimu ya msingi (completion rate) mkoani
Iringa kimeongezeka kutoka asilimia 77.2 (2014) hadi kufikia asilimia
81.1 (2015).
Mwenyekiti
wa Kamati ya Uchaguzi wa Mkoa ya kuchagua wanafunzi wataojiunga kidato
cha kwanza mwaka 2016 alikuwa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa (RAS),
Ayubu Wamoja.
EmoticonEmoticon