Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, amewaonya vikali
mawakili wa serikali wanaokula njama za kuhujumu kesi mahakamani kwa
kushirikiana na mawakili wa kujitegemea na kusababisha serikali
kushindwa kesi na kuingia hasara za mabilioni ya fedha.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaapisha mawakili wapya 104 wa
serikali jijini Dar es Salaam jana, Masaju alisema ili kutenda haki kwa
Watanzania, mawakili wa serikali wanatakiwa kutojihusisha na mchezo huo
mchafu wala kushiriki kwa namna yoyote kesi za mawakili wa kujitegemea.
Alisema wakati mwingine mawakili wa serikali wanakula njama na
wateja wao kuharibu kesi mahakamani au wakati mwingine wakili hao
anashirikiana na mteja kuvujisha kesi mahakamani.
“Kuapishwa kwenu leo (jana) kusiwe ni sehemu ya uvunjifu wa sheria
za mahakama, kwa sababu mtaungana na kundi jingine la maofisa wa
mahakama kwa lengo la kupigania utawala wa haki uliothabiti katika
sehemu zote,” alisema.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman,
alisema mawakili hao wamefikisha idadi ya mawakili 5,176 nchini, lakini
kati yao 55 wanakabiliwa na mashtaka ya nidhamu na kuwataka mawakili
hao walioapishwa kufanya kazi kwa uadilifu, pamoja na kulinda siri za
wateja.
Alisema kila mwaka serikali inawaapisha mawakili wapya 450 hadi
500, hali ambayo imesaidia kutatua changamoto ya uhaba wa mawakili
katika mahakama mbalimbali nchini, pamoja na kupunguza mrundikano wa
kesi ambazo zingeweza kusikilizwa kwa wakati.
CHANZO: NIPASHE
EmoticonEmoticon