Rais Kikwete afungua mkutano wa majaji Afrika Mashariki.


Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh. Dk. Jakaya Kikwete amefungua mkutano mkuu wa 15 wa mwaka wa chama cha mahakimu na majaji wa Afrika Mashariki na kuwataka mahakimu na majaji kujenga imani kwa wananchi wa nchi zao kupitia uwajibikaji, utendaji wa kazi na usimamizi wa kazi ili kupunguza malalamiko katika kushughulikia mashauri mbalimbali.
Akifungua mkutano huo unaofanyika kwa siku tatu jijini Mwanza, rais Kiwete amesema kuwa hivi sasa jamii imekuwa na mwamko mkubwa katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na dhana ya utawala bora, sanjari na suala zima la uwajibikaji na uwazi katika utumishi wa umma bila kuisahau idara ya mahakama. 
 
Awali rais wa chama cha mahakimu na majaji wa Afrika Masharika Mh. Jaji Lawrence Gidudu pamoja na rais wa chama cha mahakimu na majaji Tanzania Mh. Jaji Ignas Kitusi wanaeleza lengo la mkutano huo unaowaleta pamoja washiriki kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zanzibar na majaji wa mahakama ya rufani ya Afrika Mashariki.
 
Kwa upande wake mwakilishi wa jaji mkuu wa Tanzania, Mh. Jaji Edward Lutakangwa amesema kaulimbiu ya mkutano huo ambayo inasema kuimarisha imani ya wananchi kwa mahakama za Afrika Mashariki kupitia uwajibikaji na mifumo ya kupima utendaji na usimamizi wa mashauri inalenga katika kupanua misingi ya haki na usimamizi wa dhana ya uaminifu na uadilifu katika jamii kupitia idara ya mahakama.
Previous
Next Post »