MWANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI KIWIRA KIDATO CHA TATU AFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA BARABARANI.



TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 17.03.2015.

·        MTU MMOJA AKUTWA AMEUAWA KWA KUKATWA KITU CHENYE NCHA KALI KICHWANI NA WATU WASIOFAHAMIKA.


·        MWANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI KIWIRA KIDATO CHA TATU AFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA BARABARANI.


·        JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LINAWASHIKILIA WATU WATATU WAKIWA NA KETE 123 ZA BHANGI.


·        JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LINAWASHIKILIA WATU WAWILI WAKIWA NA POMBE KALI [VIROBA] ZILIZOPIGWA MARUFUKU NCHINI.


·        JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LINAMSHIKILIA MGANGA MPIGA RAMLI CHONGANISHI AKIWA NA NYARA MBALIMBALI ZA SERIKALI KINYUME CHA SHERIA.


KATIKA TUKIO LA KWANZA:

MTU MMOJA MKAZI WA CHITETE ALIYETAMBULIKA KWA JINA LA MINGSON LWABI (45) ALIKUTWA NDANI YA NYUMBA YAKE AKIWA AMEUAWA KWA KUKATWA KITU CHENYE NCHA KALI KICHWANI NA SHINGONI NA MTU/WATU WASIOFAHAMIKA.

MWILI WA MAREHEMU ULIKUTWA KATIKA NYUMBA ALIYOKUWA AKIISHI MNAMO TAREHE 16.03.2015 MAJIRA YA SAA 10:00 ASUBUHI HUKO KATIKA KITONGOJI CHA RUSUNGO, KIJIJI NA KATA YA CHITETE, TARAFA YA BULAMBYA, WILAYA YA ILEJE, MKOA WA MBEYA.

MWILI WA MAREHEMU ULIKUTWA UKIWA NA MAJERAHA SEHEMU ZA KICHWANI YA KUKATWA KITU CHENYE NCHA KALI NA HUKU UKIWA UMEANZA KUHARIBIKA. CHANZO CHA TUKIO HILI KINACHUNGUZWA, UPELELEZI ZAIDI UNAENDELEA IKIWA NI PAMOJA NA KUWATAFUTA WATU WALIOHUSIKA KATIKA TUKIO HILI.

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA KAMISHNA MSAIDIZI MWANDAMIZI WA POLISI AHMED Z. MSANGI ANATOA WITO KWA YEYOTE MWENYE TAARIFA ZITAKAZOSAIDIA KUPATIKANA KWA WATU WALIOHUSIKA KATIKA TUKIO HILI AZITOE KATIKA MAMLAKA HUSIKA ILI WAKAMATWE NA HATUA ZA KISHERIA ZICHUKULIWE  DHIDI YAO.

KATIKA TUKIO LA PILI:

MWANAFUNZI WA KIDATO CHA TATU KATIKA SHULE YA SEKONDARI KIWIRA WILAYANI RUNGWE ALIYEFAHAMIKA KWA JINA LA YOHANA KAINI (17) MKAZI WA KIJIJI CHA IBULA ALIFARIKI DUNIA BAADA YA KUGONGWA NA GARI AMBALO HALIKUWEZA KUFAHAMIKA NAMBA ZAKE ZA USAJILI WALA DEREVA WAKE.

TUKIO HILO LIMETOKEA MNAMO TAREHE 16.03.2015 MAJIRA YA SAA 07:00 ASUBUHI HUKO KATIKA KITONGOJI CHA KIKUMBE, KIJIJI CHA IBULA, KATA YA KIWIRA, TARAFA YA UKUKWE, WILAYA YA RUNGWE, MKOA WA MBEYA.

INADAIWA KUWA, MAREHEMU AKIWA NA MWANAFUNZI MWENZAKE AITWAYE ROJAS YUSUPH (15) MKAZI WA KIJIJI CHA IBULA WAKIWA WAMEPAKIZANA KWENYE BAISKELI WAKIELEKEA SHULE NDIPO WALIGONGWA NA GARI HILO LILILOKUWA LIKITOKEA TUKUYU KUELEKEA MBEYA MJINI.

KATIKA AJALI HIYO ROJAS YUSUPH ALIJERUHIWA NA AMELAZWA KATIKA HOSPITALI YA MISHENI IGOGWE-TUKUYU. CHANZO CHA AJALI NI MWENDO KASI. DEREVA ALIKIMBIA MARA BAADA YA AJALI NA JUHUDI ZA KUMTAFUTA ZINAENDELEA.

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA KAMISHNA MSAIDIZI MWANDAMIZI WA POLISI AHMED Z. MSANGI ANATOA WITO MADEREVA KUWA MAKINI WANAPOTUMIA VYOMBO VYA MOTO IKIWA NI PAMOJA NA KUFUATA SHERIA NA ALAMA ZA USALAMA BARABARANI ILI KUEPUKA AJALI. AIDHA ANATOA WITO KWA YEYOTE MWENYE TAARIFA ZA MAHALI ALIPO DEREVA WA ALIYESABABISHA AJALI HII AZITOE KATIKA MAMLAKA HUSIKA ILI AKAMATWE NA HATUA ZA KISHERIA ZICHUKULIWE DHIDI YAKE.



TAARIFA ZA MISAKO:

KATIKA MSAKO WA KWANZA, WATU WATATU WALIOFAHAMIKA KWA MAJINA YA 1. FRED JACKSON (25) MKAZI WA SOWETO 2. CLAUD FRED (16) MKAZI WA MAKUNGULU NA 3. SHAIBU ANGULWISYE (17) MKAZI WA MAKUNGULU WANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA WAKIWA NA BHANGI KETE 123 SAWA NA UZITO WA GRAM 615.  

WATUHUMIWA KWA PAMOJA WALIKAMATWA MNAMO TAREHE 16.03.2015 MAJIRA YA SAA 11:00 ASUBUHI WAKIWA KWENYE KIJIWE CHAO HUKO ENEO LA SIDO-MWANJELWA, KATA YA IYELA, TARAFA YA IYUNGA, JIJI NA MKOA WA MBEYA. WATUHUMIWA NI WATUMIAJI WA BHANGI, TARATIBU ZA KUWAFIKISHA MAHAKAMANI ZINAENDELEA.


KATIKA MSAKO WA PILI, JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LINAMSHIKILIA MTU MMOJA MKAZI WA NZOVWE AITWAYE FRANK MTENDA (19) AKIWA NA POMBE KALI [VIROBA] KUTOKA NCHINI MALAWI ZILIZOPIGWA MARUFUKU NA SERIKALI AINA YA CHARGER PAKETI 09 NA BOSS PAKETI 23.

MTUHUMIWA ALIKAMATWA MNAMO TAREHE 16.03.2015 MAJIRA YA SAA 11:30 ASUBUHI KATIKA MSAKO ULIENDESHWA NA JESHI LA POLISI HUKO KATIKA ENEO LA SIDO-MWANJELWA, KATA YA IYELA, TARAFA YA IYUNGA, JIJI NA MKOA WA MBEYA. MTUHUMIWA ALIKAMATWA AKIWA ANAUZA POMBE HIZO KWENYE GLOCERY YAKE.

KATIKA MSAKO WA TATU, JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LINAMSHIKILIA MTU MMOJA MKAZI WA SOWETO AITWAYE OBEID YESAYA (25) AKIWA NA POMBE KALI [VIROBA] KUTOKA NCHINI MALAWI ZILIZOPIGWA MARUFUKU NA SERIKALI AINA YA CHARGER PAKETI 06.

MTUHUMIWA ALIKAMATWA MNAMO TAREHE 16.03.2015 MAJIRA YA SAA 11:00 ASUBUHI HUKO KATIKA ENEO LA KABWE, KATA YA RUANDA TARAFA YA IYUNGA, JIJI NA MKOA WA MBEYA. MTUHUMIWA ALIKAMATWA AKIWA ANAUZA POMBE HIZO KWENYE KIBANDA CHAKE CHA BIASHARA MAENEO YA KABWE.

KATIKA MSAKO WA NNE, JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA LINAMSHIKILIA MGANGA MPIGA RAMLI CHONGANISHI ALIYEFAHAMIKA KWA JINA LA MONINGI NYENYESI (25) MKAZI WA MTAKUJA WILAYANI CHUNYA AKIWA NA MAFUTA YA SIMBA, MIFUPA YA KAKAKUONA NA DAWA ZA ASILI ZA AINA MBALIMBALI ZIKIWA KWENYE VIBUYU VIDOGOVIDOGO ZANA AMBAZO ANATUMIA KUPIGIA RAMLI.

MGANGA HUYO ALIKAMATWA MNAMO TAREHE 16.03.2015 MAJIRA YA SAA 07:00 ASUBUHI HUKO KATIKA KITONGOJI CHA MTAKUJA, KIJIJI NA KATA YA LUALAJE, TARAFA YA KIPEMBAWE, WILAYA YA CHUNYA, MKOA WA MBEYA. MTUHUMIWA HANA KIBALI CHA KUENDESHA SHUGHULI ZA UGANGA WALA KIBALI CHA KUMILIKI NYARA HIZO ZA SERIKALI. TARATIBU ZA KUMFIKISHA MAHAKAMANI ZINAENDELEA.

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA KAMISHNA MSAIDIZI MWANDAMIZI WA POLISI AHMED Z. MSANGI ANAENDELEA KUTOA WITO KWA JAMII KUACHA KUTUMIA DAWA ZA KULEVYA, KUJIHUSISHA NA UINGIZAJI, USAMBAZAJI NA UUZAJI WA BIDHAA HARAMU KAMA VILE POMBE KALI ZILIZOPIGWA MARUFUKU NCHINI KWANI NI KINYUME CHA SHERIA NA NI HATARI KWA AFYA YA MTUMIAJI. AIDHA ANATOA WITO KWA WATU WANAOJISHUGHULISHA TIBA ASILIA KUFUATA TARATIBU ZA KUFANYA KAZI HIYO IKIWA NI PAMOJA NA KUPATA VIBALI VINAVYOWARUHUSU KUFANYA KAZI HIZO.
                                                                     Imesainiwa na:
[AHMED Z. MSANGI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

Previous
Next Post »