Na Lucy Patrick
“Naombeni nilindwe nisiuawe nami niweze kutimiza ndoto yangu ya kuwa
mwalimu”Haya
ni maneneo ya Mtoto mdogo wa miaka mitatu Princess
Suo ambaye ni mlemavu wa ngozi yaani Albino.
Nimaneno
yanayotia uchungu huzuni sana hasa kwa
nchi kama Tanzania ambayo inajulikana duniani kote kama kisiwa cha amani hivi
amani hiyo iko wapi?
Kama
mtanzania unajisikiaje kuona vitendo vya kikatili kama kuuawa kwa
Albino,kukatwa viungo na kubaki na ulemavu wa kudumu vikiendelea majibu unayo
mwenyewe chukua hatua kuwa mlinzi kwa watu wenye ulemavu
Inaumiza
sana kuona wenzetu wakiishi maisha yasiyo na amani katika nchi yao wenyewe
tutaendelea kusema Kwa nguvu zote tunaumia sana na hii hali kuona wenzetu wakiwwa wanauawa kama wanyama
mpaka lini lazima tuchukue hatua kuhakikisha ndugu zetu hawa wanaishi kwa amani
na kufurahia uubwaji wao lazima tukumbuke kuwa wao ni kama binadamu wengine tu
hizi imani za kwamba wao ni dili hazina manufaa yoyote kwetu.
“Au hii sio issue ya kitaifa mkaichukulia mkazo kama mnavyochukulia zingine ,” alihoji Keisha.
” Inaniuma sana na ninakata tamaa na nchi yangu kila siku zinavyozidi kwenda natamani niiikimbie hii nchi niende mbali ambapo labda sitoweza kushuhudia huu ukatili unaoendelea ndani ya nchi mnayoiita nchi yenye amani.”
“Maisha yetu yapo hatarini Mh Raisi sijawahi kujutia kuzaliwa hivi am always proud na nilivyo lakini this time aahh ee mungu Nisamehe mja wako kwa mara ya kwanza najutia kuwa na hii hali.”Hayo ni maneno ya Msanii wa bongo flavor Keisha ambaye naye pia ni Albino .
Kwa hali ya
kawaida ukisoma maneno kama hayo ambayo yanaumiza sasa imefika hatua ya kusema
imetosha sasa lazima liwe jukumu letu sote kwa umoja wetu kama watanzania
tuseme kwa pamoja inatosha sasa na kuwalinda ndugu zetu albino.
Ipo haja
kubwa kama taifa tukiwa katika mchakato wa kupata katiba mpya kuhakikisha
sheria inafanyiwa ukarabati mkubwa kwenye vipengele ambavyo vinachelewesha hukumu za kesi ya mauaji ya Albino na badala
yake kesi hizo ziweze kuharakishwa na
mtuhumiwa aweze kupewa adhabu kali. Kwa kufanya hivyo kunauwezekano wa
kupunguza ama kutokomeza kabisa matukio ya mauaji ya albino hapa nchini .
Kwa mujibu
wa Bwana Joseph Tona ambaye ni Rais wa
Chama cha Albino Tanzania matukio zaidi ya 120 ya kesi za mauji ya albino, kati
yake 11 ndiyo yaliyofikishwa Mahakama, ambapo kati ya hizo kesi tano tu
zimeweza kutolewa hukumu hadi sasa.Kwa hiyo tunaweza kuona uwiano jinsi kesi hizo zinavyokwenda kwa kasi
ndogo huku mauaji haya yakiendelea.
Mauaji haya
yanayoendelea yanaichafua nchi yetu ambapo tumeona tamko la Kamishna wa Haki za
Binadamu wa Umoja wa Mataifa (UN), Zeid Ra’ad Al Hussein, kuitaka Serikali ya Tanzania kuchunguza na kuwashtaki
watu waliohusika na uhalifu wa mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi
(albino).
“Nalaani vikali mauaji haya ya kutisha na ukataji viungo vya Yohana Bahati, mtoto albino mwenye umri wa mwaka mmoja kaskazini mwa Tanzania, Yohana alitekwa kutoka kwa mama yake na watu watano wasiojulikana waliokuwa na silaha za jadi, na kumjeruhi kwa mapanga mama yake alijeruhiwa vibaya wakati akijaribu kumwokoa mwanae”alisema Zeid Ra’ad Al Hussein
Mwili wa mtoto huyo uliokotwa Februari 17 ukiwa hauna mikono wala miguu.
Al Hussein, alisema mashambulizi dhidi ya albino, mara nyingi huchochewa na matumizi ya viungo vyao vya mwili kwa ajili ya ushirikina, ambapo hadi sasa yamegharimu maisha ya watu 76 nchini Tanzania tangu mwaka 2000.
Bado watu wengi wamekuwa wanahoji ongezeko la vitendo vya mauaji ya Albino kujitokeza kipindi cha uchaguzi ambapo tunashuhudia karibu kila mwaka wakati tukikaribia uchaguzi mkuu ndipo vitendo vya namna hii ya ukatili hujitokeza kwa kasi kuna nini kimejificha hapo.
Wakati nakua
nilikuwa Napata kusimuliwa kuwa albino huwa hawafi bali wanapotea tu na mimi
niliamini hivyo na nina imani wengi story hii mliisikia.Hili jambo la kupotea
tu limenifanya kutafakari kwa upya kuwa kuna uwezekano albino walikuwa wakiuawa
toka zamani kwa siri hivyo watu wakiwa hawawaoni wanasema wametoweka kumbe kuna
uwezekano mkubwa walikuwa wanauawa kwa imani hizi za ushirikina na jamii
ilikuwa haielewi jambo hili.
Kwa upande
wenu viongozi mbona kuna ukimya katika hili tumeshuhudia wasanii na watu
mbalimbali wakikemea na kupinga ukatili huu katika mitandao mbalimbali ya
kijamii lakini hali ni tofauti kwa viongozi wetu swali ni kwanini mko kimya? je
ukimya wenu ni kwamba mnaunga mkono jambo hili au ndio mnaunda tume ya
uchunguzi.
Tumeshuhuda
mkiwa wepesi kupinga nguvu zote Suala la Escrow,,EPA na mengineyo je ni kwamba
hili haliwasumbui na hamuoni kama wananchi wanawatazama ninyi mbona wepesi ule
tulio uona katika mambo ya ufisadi hatuuoni katika hili la mauaji ya Albino au
ninyi sio wawakilishi wao jitafakarini.
Mauaji haya
yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku ambapo katika Maadhimisho ya Siku ya
Amani Kimataifa ya mwaka jana 2014 Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu
Tanzania (Shivyawata), limeitaka serikali kupitisha adhabu ya kunyongwa kwa
wale wanaohusika na mauaji ya Albino.
Mimi naamini
walikuwa sawa maana tunaambiwa utamu wa ngoma sharti uingie ucheze.Imani yangu
ni kwamba kama mambo haya ya ukatili yangemkuta mmoja kati ya viongozi wetu
labda mngeamka na kuanza kuwatetea na kuwalinda albino lakini kwa sababu hamna
uchungu nalo hamuwezi kujua ni maumivu kiasi gani wanayapitia ndugu zetu hawa.
Kadhalika, takwimu za kutoka mwaka 2006
zinaonyesha kuwa Albino 74 na sasa 76 akiwemo
mtoto Yohana Bahati aliyeuawa hivi karibuni wameshauawa kikatili, huku
56 wakinusurika kifo, na kati yao 11 wameongezewa ulemavu mwingine wa kudumu
kwa kukatwa viungo vyao.
Hali hii kwa
sasa inawafanya watu wenye aina hii ya ulemavu wa ngozi kuathirika kisaikolojia
na kupata msongo wa mawazo pamoja na kuishi kwa mashaka,wasiwasi,woga,kutojiamini
na kufichwa kwa kuhofia usalama wao maana hawana amani kabisa katika nchi yao
wenyewe, imefika wakati mimi na wewe
kuchukua jukumu la kuwalinda ili tuweze kutokomeza ukatili huu.
Tukiwa
tunaelekea uchaguzi mkuu picha hii inaashiria nini hili ni swali ambalo
tunatakiwa kujiuliza kuna mahusiano gani kati ya hivi vitu viwili imekuwa
ikisemekana waganga wa jadi kutumiwa na na viongozi wa kubwa katika kuwania
nyadhifa mbalimbali serikalini.
Suala hili inaonekana ni mambo ya ushirikina yanahusishwa hapo lakini pia kwa upande wa serikali haiamini mambo ya ushirikina je ndio sababu ya ukimya wao, lakini wanashuhudia na kuona mauaji hayo hatua gani Serikali imeshachukua ukimya hausaidii ndio maana naona imefika wakati kama jamii kulitazama hili kwa jicho la tatu na kuwalinda Albino.
“Japokuwa Tanzania inasifika ndani na nje kama kisiwa cha amani, tafsiri hiyo ni kinyume kwani ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa mauaji ya kikatili, hivyo mwito wangu kwa viongozi wa dini tumieni midomo yenu kupinga hali hii kwa sababu na sisi tumeumbwa na Mungu na tunastahili kuisha kama wengine,” alisema Mariam Stanford, mkazi wa Ngara, mkoani Kagera, ambaye yeye ni muathirika wa janga hili na mikono yake miwili imekatwa .
Nakumbuka mwaka
2009 Serikali kupitia waziri mkuu Mkuu
Mizengo Pinda alitoa kauli ya kupiga marufuku leseni za waganga wa kienyeji na
wale wa jadi mkakati huu uliishia wapi na ule mpango wa kura za siri
zilizopigwa toka mwaka huo wa 2009 hadi sasa ziko wapi mbona mpaka sasa hakuna
mrejesho wowote.
Ikitokea
mambo kama ya maandamano tumeona jeshi la polisi likitumia nguvu kubwa katika
kudhibiti kwanini nguvu hiyo msiihamishie kwenye mauaji na ukatili kwa albino
ili kutokomeza hilo.
Mbona katika suala la vita juu ya madawa ya kulevya
tumeona jinsi ambavyo mmeweza kupambana nayo mpaka sasa tunaamini vita hiyo iko
mbioni kumalizika kigugumizi cha nini katika hili chukueni hatua ili imani ya
albino kwa serikali yao irudi maana kwa sasa hawana imani na mtu yeyote wanahisi
kila mtu ni adui kwao na hivyo hawako salama.
Pia kwa taasisi zilizopewa jukumu la kusimamia vitendo
hivyo vya kikatili dhidi ya walemavu hususani albino mnatakiwa kutekeleza majukumu mliyopewa
kisheria kwa uadilifu mkubwa jamii ya Watanzania ione haki inatendeka ili
kudumisha amani ya nchi.
Hata hivyo Sipingi juhudi za serikali katika mapambano
dhidi ya mauaji haya kwa albino ila nafikiri wakati umefika sasa kama jamii
kushiriki moja kwa moja kuhakikisha mapambano haya yanaendelea na ukatili dhidi
ya albino unaisha kabisa maana naamini katika usemi wa umoja ni nguvu na
utengano ni dhaifu kwa pamoja tunaweza.
Simama nami
kutokomeza ukatili kwa Albino wasiishi kwa hofu na mashaka katika nchi yao
wenyewe.
Mwisho.
Simu:0754884531/0717696330
Email:lucypatrick.e@gmail.com
Blog: www.lucypatickm.blogspot.com.
EmoticonEmoticon