Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo.
Wakati Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza likiendelea kumsaka mtoto mwenye ulemavu wa ngozi (albino), Pendo Emmanuel (4) kwa siku ya 51 sasa aliyeibwa kijiji cha Ndami, Kwimba na watu wasiofahamika Desemba 27, mwaka jana, mtoto mwingine albino ameibwa mbele ya wazazi wake katika kijiji cha Ilelema, wilayani Chato, Geita.
Mtoto huyo, Yohana Bahati, mwenye umri wa mwaka mmoja, aliibwa usiku wa kuamkia jana, akiwa amebebwa na mama yake, Esther Bahati (30), ambaye alivamiwa na watu hao na kupigwa mapanga akiwa jikoni kisha kuporwa mtoto huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alisema tukio hilo la kusikitisha lilitokea juzi saa 2:00 usiku, wakati mama huyo akiwa jikoni anapika chakula na watu hao kumvamia na kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Watu wasiofahamika walimjeruhi mama wa mtoto kisha kumtwaa mgongoni pasipo kumdhuru na kutoweka sehemu isiyojulikana mpaka sasa hajapatikana wakati jeshi la polisi likiendelea kuwasaka waliotenda uhalifu huo,” alisema Kamanda Konyo.
Konyo alisema Esther baada ya kujeruhiwa kwa mapanga, aliwahishwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa usoni, mikononi na mabegani alipokuwa akijaribu kupambana na watu hao wasimchukue mwanaye.
Alisema kutokana na tukio hilo, polisi mkoani Geita inamshikilia baba wa mtoto huyo, Bahati Misalaba, ambaye wakati tukio hilo linatokea alikuwa akiota moto nje ya nyumba hiyo.
Hata hivyo, Konyo alisema polisi wameimarisha ulinzi katika nyumba ya familia hiyo kutokana na kuwapo watoto wengine wawili albino ambao wakati tukio likitoe walikuwa wakicheza nyumba ya jirani.
Kamanda huyo alisema baba wa mtoto huyo, Misalaba, wakati tukio linatokea, alikuwa akiota moto maarufu ‘kikome’ nje ya nyumba hiyo.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha siku 51 kutokea tukio kama hilo baada ya mtoto Pendo wa kijiji cha Ndami, wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, kutekwa na watu wasiofahamika, huku jeshi la polisi likiendelea kuwasaka waliotenda uhalifu huo pamoja kumtafuta Pendo akiwa hai ama mfu bila ya mafanikio hadi sasa.
Juhudi za jeshi hilo na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, kutaka mtoto huyo apatikane ndani ya siku tano, ziligonga mwaka kwa kipindi hicho licha ya polisi kuendelea na msako na upelelezi kwa watu nane inaowashikilia akiwamo baba wa Pendo, Emmanuel Shilinde.
TAKWIMU ZA KIMATAIFA
Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, asilimia mbili ya watu wanazaliwa na ulemavu wa ngozi husherehekea miaka 40 ya kuzaliwa kwao, wakati barani Afrika mtu mmoja kati ya 2,000 huzaliwa akiwa albino tofauti na Marekani ambako mtu mmoja kati ya 17,000 huishi wakiwa wa ulemavu wa ngozi.
Mauaji na albino nchini yanaonekana kushamiri hususani katika mikoa ya kanda ya ziwa kutokana sababu kubwa za imani za kishirikina ambazo pia zinasababisha mauaji ya vikongwe tangu yalipoanza mwaka 2006/2007.
UNDER THE SAME SUN
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), Under the Samesun (UTSS) lenye makazi yake nchini Canada, Peter Ash, alishangazwa na vyombo vya dola nchini kushindwa kuwakamata wanunuzi wa viungo vya albino licha ya kutajwa na waganga wa kienyeji na wauaji wenyewe.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza hivi karibuni, Ash alisema viungo vya albino vinanunuliwa kwa bei kubwa ambayo mwananchi wa kawaida hawezi, hivyo vyombo vya dola vinapowakamata wauaji na kuwahoji na kuwaelekeza wanunuzi, vinashindwa kuwakamata.
CHANZO:NIPASHE
EmoticonEmoticon