·
MTEMBEA KWA MIGUU AFARIKI DUNIA BAADA YA
KUGONGWA NA PIKIPIKI WILAYANI KYELA.
·
MTOTO WA MIAKA 05 AFARIKI DUNIA BAADA YA
KUANGUKIWA NA MTI.
·
WATU 04 WANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MKOA WA
MBEYA WAKIWA NA NG’OMBE WANNE MALI INAYODAIWA KUWA NI YA WIZI.
·
MTU MMOJA RAIA WA NCHINI MALAWI ANASHIKILIWA NA
JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA AKIWA AMEINGIA NCHINI KINYUME CHA SHERIA.
·
MTU MMOJA MKAZI WA RIFT VALLEY WILAYA YA CHUNYA
ANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA AKIWA NA POMBE YA MOSHI.
·
MTU MMOJA MKAZI WA CHIANGA NCHINI ZAMBIA ANASHIKILIWA
NA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA AKIWA NA KETE 85 NA GRAMU 10 ZA BHANGI.
KATIKA TUKIO LA KWANZA:
MTEMBEA KWA MIGUU MMOJA ALIYETAMBULIKA KWA JINA LA TUNSUME MBOPE (35) MKAZI WA KYELA
AMEFARIKI DUNIA PAPO HAPO BAADA YA KUGONGWA NA PIKIPIKI YENYE NAMBA ZA USAJILI T.496 CRL AINA YA KINGLION ILIYOKUWA IKIENDESHWA NA DEREVA ASIYEFAHAMIKA JINA WALA
MAKAZI YAKE.
AJALI HIYO IMETOKEA MNAMO TAREHE 16.10.2014 MAJIRA YA SAA
19:30 JIONI HUKO MAFULA SOP, KATA YA KYELA, TARAFA YA UNYAKYUSA, WILAYA
KYELA, MKOA WA MBEYA. CHANZO CHA AJALI KINACHUNGUZWA. DEREVA ALIKIMBIA MARA
BAADA YA AJALI NA JUHUDI ZA KUMTAFUTA ZINAENDELEA. MWILI WA MAREHEMU
UMEHIFADHIWA KATIKA HOSPITALI YA WILAYA YA KYELA.
KAMANDA WA POLISI MKOA
WA MBEYA KAMISHINA MSAIDIZI MWANDAMIZI WA POLISI AHMED Z. MSANGI ANATOA WITO KWA MADEREVA KUWA MAKINI WANAPOTUMIA
VYOMBO VYA MOTO IKIWA NI PAMOJA NA KUZINGATIA SHERIA NA ALAMA ZA USALAMA
BARABARANI ILI KUEPUKA AJALI ZINAZOWEZA KUEPUKIKA. AIDHA, ANATOA WITO KWA
YEYOTE MWENYE TAARIFA ZA MAHALI ALIPO MTUHUMIWA [DEREVA] AZITOE KATIKA MAMLAKA
HUSIKA ILI AKAMATWE NA HATUA ZA KISHERIA ZICHUKULIWE DHIDI YAKE.
KATIKA TUKIO LA PILI:
MTOTO MWENYE UMRI WA MIAKA 05 ALIYETAMBULIKA KWA JINA LA ISACK JACOB MKAZI WA KIJIJI CHA ILUNDO ALIFARIKI DUNIA BAADA YA
KUANGUKIWA NA MTI ULIOKUWA UNAKATWA NA WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI KIWIRA
ILIYOPO WILAYA YA RUNGWE.
TUKIO HILO LIMETOKEA MNAMO TAREHE 16.10.2014 MAJIRA YA SAA
11:00 ASUBUHI HUKO KATIKA MAENEO YA SHULE YA SEKONDARI KIWIRA, KATA YA
KIWIRA, TARAFA YA UKUKWE, WILAYA YA RUNGWE, MKOA WA MBEYA.
INADAIWA KUWA, MAREHEMU ALIKUWA AKIOKOTA KUNI NA
WATOTO WENZAKE VICHAKANI NA NDIPO ALIANGUKIWA NA MTI HUO NA KUPELEKEA KIFO
CHAKE.
KAMANDA WA POLISI MKOA
WA MBEYA KAMISHINA MSAIDIZI MWANDAMIZI WA POLISI AHMED Z. MSANGI ANATOA WITO KWA WAZAZI/WALEZI KUWEKA UANGALIZI WA
KUTOSHA KWA WATOTO WADOGO ILI KUEPUKA MADHARA YANAYOWEZA KUEPUKIKA. AIDHA,
ANATOA WITO KWA JAMII KUTOWARUHUSU WATOTO WADOGO KWENDA MAENEO YA
VICHAKANI/PORINI BILA KUWA NA WATU WAZIMA KWANI NI HATARI.
TAARIFA ZA MISAKO:
KATIKA MSAKO WA KWANZA, WATU WANNE WALIOFAHAMIKA KWA MAJINA YA 1. ZAKAYO NOVA (27) 2. HAMADI NGEKA (27) WOTE WAKAZI WA
TUNDUMA 3. YONA SIWALE (23) MKAZI WA
KIJIJI CHA CHIWANDA NA 4. EZEKIA
SIKAPONDA (33) MKAZI WA CHITETE WANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MKOA WA
MBEYA WAKIWA NA NG’OMBE WANNE WANAODHANIWA KUWA MALI YA WIZI.
WATUHUMIWA HAO WALIKAMATWA MNAMO TAREHE 16.10.2014 MAJIRA YA SAA
05:00 ALFAJIRI HUKO KATIKA MACHINJIO YA TUNDUMA, MTAA WA SOGEA, KATA NA
TARAFA YA TUNDUMA, WILAYA YA MOMBA, MKOA WA MBEYA.
INADAIWA KUWA, NG’OMBE HUO NI MALI YA MTU MMOJA
ALIYEFAHAMIKA KWA JINA LA LUSANGIA
JIHUMBI, MKAZI WA CHITETE. AIDHA, THAMANI YA HALISI YA NG’OMBE HAO NI TSHS.2,400,000/=. NG’OMBE HAO
WAMEHIFADHIWA KITUO CHA POLISI TUNDUMA WAKISUBIRI TARATIBU NYINGINE ZA
KISHERIA.
KATIKA MSAKO WA PILI, MTU MMOJA RAIA WA NCHINI MALAWI ANASHIKILIWA NA
JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA KOSA LA KUINGIA NCHINI KINYUME CHA SHERIA.
MHAMIAJI HUYO AMEFAHAMIKA KWA JINA LA ALFRED
RUNGU (40) ALIKAMATWA MNAMO TAREHE 16.10.2014 MAJIRA YA SAA 08:50 ASUBUHI
HUKO STENDI YA MABASI TUKUYU MJINI, KATA YA KAWETELE, TARAFA YA TUKUYU MJINI, WILAYA
YA RUNGWE, MKOA WA MBEYA. TARATIBU ZA KUMKABIDHI IDARA YA UHAMIAJI KWA HATUA
ZAIDI ZA KISHERIA ZINAENDELEA.
KATIKA MSAKO WA TATU, MTU MMOJA MKAZI WA RIFT VALLEY WILAYA YA CHUNYA
AITWAYE LUCY EDWARD (25)
ANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA AKIWA NA POMBE HARAMU YA MOSHI
UJAZO WA LITA 20.
MTUHUMIWA ALIKAMATWA MNAMO TAREHE 16.10.2014 MAJIRA YA SAA
17:30 JIONI HUKO KATIKA KITONGOJI CHA RIFT VALLEY, KIJIJI CHA MALANGAMILO,
KATA YA MKOLA, TARAFA YA KIWANJA, WILAYA YA CHUNYA, MKOA WA MBEYA. MTUHUMIWA NI
MTENGENEZAJI NA MUUZAJI WA POMBE HIYO.
KATIKA MSAKO WA NNE, MTU MMOJA MKAZI WA CHIANGA NCHINI ZAMBIA
ALIYEFAHAMIKA KWA JINA LA GEORGE
SIKAMANGA (18) ANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA AKIWA NA KETE 85 NA GRAMU 10 ZA BHANGI.
MTUHUMIWA ALIKAMATWA MNAMO TAREHE 16.10.2014 MAJIRA YA SAA
19:45 JIONI HUKO ENEO LA CUSTOM, KATA NA TARAFA YA TUNDUMA, WILAYA YA
MOMBA, MKOA WA MBEYA KATIKA MSAKO ULIOENDESHWA NA JESHI LA POLISI KATIKA MAENEO
HAYO. MTUHUMIWA NI MUUZAJI WA BHANGI HIYO NA TARATIBU ZA KUMFIKISHA MAHAKAMANI
ZINAENDELEA.
KAMANDA WA POLISI MKOA
WA MBEYA KAMISHINA MSAIDIZI MWANDAMIZI WA POLISI AHMED Z. MSANGI ANATOA WITO KWA JAMII KUACHA KUTUMIA POMBE YA
MOSHI/DAWA ZA KULEVYA KWANI NI KINYUME CHA SHERIA NA NI HATARI KWA AFYA YA
MTUMIAJI.
Imesainiwa na:
[AHMED Z. MSANGI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
EmoticonEmoticon