Kuna sababu mbalimbali kwanini
mtu atake kuajiri, badala ya kuajiriwa, mfano kipato kidogo anachopata katika
kazi husika, hitaji la kutaka uhuru zaidi binafsi wa kufanya kazi, hitaji la
kuweza kutoa ajira kwa wengine na zaidi sana kuweza kutumia vema kipaji na
uwezo wa kuzalisha ambao katika kazi ya sasa mtu hapati nafasi ya kufanya
hivyo.
Kujiajiri ni jambo linalohitaji
maandalizi ya muda mrefu na kuna mambo ya msingi kuyafahamu, haiwezekani tuu ,
ukaacha kazi na kusema ok, acha nijiajiri.
Makala hii inachambua mambo ya
msingi ya kujiandaa na kuyafahamu kabla mtu hajaamua kuacha kuajiriwa.
Mkakati ni muhimu: Wazo au ndoto isiyo na mkakati wa kuitimiza ni upuuzi yaani
ndoto hiyo au wazo hilo halina maana, hivyo basi ndoto yako ya kujiajiri siku
moja, ni lazima iwekewe mkakati wa kuifanikisha ikiwa ni pamoja na muda hasa wa
lini utaitimiza hiyo ndoto.
Katika kuweka mkakati huu
wa kutimiza ndoto yako, fanya utafiti wa kina kuhusu mipango yako binafsi ya
maisha, mtazamo wako kuhusu maisha, mpenzi/mke wako, familia yako, na hali ya
jamii kwa ujumla inavyoenda kama vile mabadiliko ya hali ya kisiasa,
teknolojia, na uchumi.
Tengeneza malengo ya aina
ya shughuli unayotaka kuifanya ukiacha kuajiriwa, na pima uwezekano wa shughuli
hiyo kufanyika kweli na kama itakulipa. Utambue pia aina ya watu na rasilimali
nyingine utakazozihitaji, na jinsi utakavyozipata.
Unahitaji fedha: Ndio, unahitaji kiasi cha fedha za kutosha kununua vifaa na
malighafi za kutengenezea bidhaa yako. Pia unahitaji fedha za kuwalipa
wafanyakazi wako, na zaidi sana , unahitaji fedha za kuendesha maisha yako na
familia yako , kwa kipindi fulani kabla ya biashara kuanza kukulipa mshahara.
Hivyo kabla haujaacha kibarua chako, hakikisha umetengeneza bajeti ya kutosha
na una akiba ya kutimiza mahitaji ya bajeti yako. Usingependa uache kazi halafu
uanze kuwa omba omba kwa rafiki na jamaa, au uanze kujuta.
Network ni muhimu: Kumbuka katika kujiajiri kwako, utahitaji wateja, washirika,
wafanyakazi na hata washauri mbalimbali ili mambo yako yaende vizuri. Hivyo,
wakati ukiwa umeajiriwa ndio wakati wako muafaka wa kutengeneza na kupanua wigo
wako wa watu unaowafahamu na waliokaribu nawe.
Kumbuka kuendeleza mawasiliano
kwani watu hawapendi kuona wewe unataka kuwatumia tuu kisha unawatupa. Endeleza
mawasiliano walau hata kwa salamu tuu. Zaidi sana, heshimu watu wote, hata
usiowafahamu au wale unaodhani 'sio watu muhimu'.
Jenga taswira nzuri kwa
jamii kwa lugha fasaha, picha na matukio mengine, usifanye watu wakufikirie
vibaya.
Usipitwe na wakati: Hakikisha kuwa unafuatilia taarifa za matukio, dili na watu
wanaohusiana na aina ya shughuli unayopanga kuifanya wakati utakapojiajiri. Hii
itakusaidia kupata uzoefu na kusoma alama za nyakati, na pengine kutambua fursa
nyingine zaidi.
Endelea kujifunza zaidi
kuhusu kazi yako, watu na jamii kwa ujumla kwani kujiajiri kunahitaji uzoefu
zaidi, na zaidi sana uwezo wa kupambana na changamoto nyingi ambazo nyingine
haujawahi kukutana nazo kabisa, ila taarifa za awali na kujua jinsi mambo
yanavyoenda kwa ujumla katika jamii vitakufanya ushinde changamoto.
Maana halisi ya biashara: Baada ya kuacha kuajiriwa, hautarajii kuwa mtu wa ‘kuganga njaa’
yaani kufanya biashara ili mradi tuu hela iingie, lakini haujui mwelekeo wa
biashara yako upoje, na wala hakuna mkakati wa kuikuza na kuimarisha biashara
husika.
Biashara inahusu kutimiza
mahitaji ya watu, kwahiyo ili mradi utakuwa na uwezo mkubwa wa kutimiza
mahitaji ya watu, na kuendelea kuhamasisha watu zaidi kuja kwako uweze kutimiza
mahitaji yao , basi biashara itakua, na itaendelea kuwa endelevu.
Kinyume cha hapo,
ushindani utakutoa katika biashara kwani wateja watakambilia kwa wengine.
Biashara sio tuu kupata wateja, ni vile kuweza kuendelea kupata wateja na
kuendelea kupanua biashara.
Inabidi uipende shughuli
husika unayoifanya, na uweze kutimiza mahitaji ya wateja kupitia biashara
husika.
Muda wako mwingi
utautumia katika shughuli yako mpya utakayojiajiri hivyo, kama ambavyo kazi
uliyonayo pengine ‘inakuboa’, hakikisha ajira yako binafsi ‘haikuboi’.
Umuhimu wa wafanyakazi: Watendaji wa shughuli husika za biashara yako utakayoianzisha ni
muhimu wawe wenye ujuzi na uzoefu wa kutosha wa kufanya shughuli husika, na
uweke mikakati ya kuwapatia nyenzo zote muhimu za kufanyia kazi ikiwemo
teknolojia na mazingira mazuri ya kazi. Hivyo basi wakati unajiandaa kujiajiri
tilia maanani hili katika bajeti yako ya kuajiri. Usingependa wafanyakazi wao
wajisikie vibaya kama vile wewe ulivyojisikia vibaya katika ajira yako fulani
(pengine ajira yako ya sasa). Muda huu ambao umeajiriwa, ndio muda pia muafaka
wa kusaka 'vipaji'- yaani watu ambao utafanya nao kazi utakapojiajiri.
Inakuhusu wewe : Mafanikio yako katika kujiajiri yanategemea mambo mengi ila
zaidi sana yanakutegemea wewe. Je, nini hasa sababu yako ya kutaka
kujiajiri?
Ni kweli una bidhaa au
huduma haswa ya kupeleka sokoni itakayokufanya iendeshe maisha yako na
kuiendeleza biashara husika au ni hasira tuu za jinsi bosi wako anavyokuchulia
hapo ofisini kwako, au kwakuwa mshahara uliopo sasa haukutoshi. Je, mipango
yako mingine ya maisha ipoje?
Ndoto zako za kusoma, au
kuishi sehemu tofauti tofauti, pengine mkoa mwingine tofauti na uliopo sasa, au
pengine hata nchi husika. Je, yote hayo yanaathiri vipi mipango na mikakati
yako ya kujiajiri, bila kusahau msukumo toka kwa familia yako.
Ndoto sahihi: Ni kweli kuwa upo sahihi kufikiria au kuota kufanya biashara
kubwa na yenye mafanikio sana, lakini kumbuka mafanikio hayaji kwa usiku mmoja,
na hata kama yatakuja kwa usiku mmoja, inahitajika kazi ya muda mrefu kuyafanya
yawe endelevu.
Hivyo basi, usingoje
wakati ‘muafaka’ wa wewe kuwa na kiasi kikubwa cha fedha au kwamba ‘umeyaset’
vema mambo yote.
Anza kidogo kidogo,
kubali kufanya makosa, na tambua kuwa hata kama utafanya uchambuzi na uchunguzi
wa kutosha kuhusu soko, jamii na teknolojia, hali halisi unayoenda kukumbana
nayo inaweza kuwa tofauti na ile uliyojifunza wakati wa uchambuzi au uchunguzi
wako kwakuwa hicho unachoenda kufanya ni kipya hakikufanyiwa uchambuzi, bali
unakifanya kutokana na uchambuzi uliofanya hapo awali.
Kuna mtu mwingine atakuja kutumia makosa au mafanikio yako
kupanga mambo yake.
EmoticonEmoticon