Magari yanayojiendesha bila ya dereva kushika usukani yataanza kusambazwa duniani kabla ya muda uliotarajiwa.
Hiyo inatokana na makubaliano yaliyofikiwa na kuondolewa kwa kipengele cha sheria za usalama barabarani ambacho kilikuwa kinazuia gari kujiendesha bila ya kuongozwa na binadamu.
Kipengele hicho katika makubaliano ya Umoja wa Mataifa, kilisababisha utafiti uliofanywa kwa muda mrefu wa kutengeneza magari ya aina hiyo kukwama, lakini hivi karibuni, mataifa ya Ulaya yalipambana na kuhakikisha kipengele hicho kinabadilishwa.
Jitihada kubwa zilifanywa na mataifa yanayozalisha magari ya kifahari ya Ujerumani, Italia na Ufaransa ambayo yalipambana kuingiza teknolojia hiyo ili kuipiku Marekani ambayo nayo ilikuwa imeanza kufanya majaribio ya magari hayo. “Leo nina furaha kwamba nitaweza kuendesha gari bila ya kushika usukani kwa kiasi fulani. Tushukuru makubaliano ya Vienna (Austria), kuhusu usalama barabarani yamefanyiwa mabadiliko,” alisema mkuu wa utafiti wa kampuni ya Daimler, Thomas Weber na mkuu wa maendeleo wa Mercedes - Benz.
Alisema kwa miaka mingi, gari kujiendesha lenyewe imekuwa ndoto kubwa kwa udereva wa baadaye. “Tunashukuru kampuni kama Google kwa kuja na wazo kama hili,” alisema.
Jimbo la Nevada, Marekani lilipitisha sheria ya kuruhusu magari hayo Juni, 2011 na Google ililijaribu moja mwaka 2012.
Agosti 2013, Mercedes-Benz ilitengeneza gari aina ya S-Class ambalo lilijaribiwa kwa kutembea kilomita 103.
Hata hivyo, majaribio hayo yalikwazwa na Ibara ya 8 ya Makubaliano ya Usalama Barabarani ya mwaka 1968 ambayo yalitaka “kila dereva kwa muda wote kuongoza gari lake na kulinda viumbe alionao.”
Mabadiliko yaliyofanywa katika Sheria ya Usalama Barabarani na Umoja wa Mataifa yanaelekeza kuwa pamoja na kuwa gari litajiendesha, ni lazima kuwe na mtu wa kuwasha na kulizima na mtu lazima awemo kwenye gari muda wote.
Mabadiliko hayo yanaondoa urasimu wote uliokuwapo katika utekelezaji. Nchi 72 zilizosaini makubaliano hayo, zitalazimika kukaa na kutunga kanuni za utekelezaji wa sheria zao. Kampuni kubwa za Ujerumani tayari zimeingiza teknolojia kubwa katika magari yao kama Audi, Mercedes - Benz, BMW na zinatarajiwa kuwa mstari wa mbele kuwekeza katika teknolojia hii.
EmoticonEmoticon