Na,
Albert Sanga, Iringa.
Miaka takribani mitatu
iliyopita niliandika makala hapa safuni iliyokuwa na kichwa, “Njooni shambani
mtajirike”. Ilikuwa ni makala iliyoshirikisha fursa kuhusu uwekezaji katika
kilimo cha miti. Kwa rekodi nilizonazo inaonesha kuwa ile ni moja ya makala
zangu ambayo iliwavutia maelfu ya wasomaji; kutokana na mamia ya mirejesho ya
niliyoipokea.
Si nia yangu kukumbusha
habari ya fursa ile, lakini kuna mambo mengi sana nilijifunza [kupitia makala
ile] kuhusu hulka za watanzania linapokuja suala la uwekezaji. Kwa mujibu wa
rekodi zangu inaonesha kuwa kati ya waliowasiliana nami, asilimia 7% walivutiwa
na kuikubali fursa hii lakini kikwazo kikubwa kikawa ni ukosefu wa fedha; wengi
wao wakaahidi kwamba wanaendelea kujipanga na ipo siku watawekeza.
Asilimia 4% tu ndio
walioipenda na kuchukua hatua ya kuchangamkia fursa hii katika maeneo
mbalimbali nchini; wakiwemo wachache waliosafiri kuja Iringa na wengine
walionijulisha kuwa wamefanikiwa kupata mashamba maeneo mbalimbali ikiwemo
Tanga, Njombe, Tabora, Bukoba na kule Mbeya.
Asilimia 89%
walinieleza kuwa fursa ya uwekezaji katika miti ni nzuri lakini inachukua muda
mrefu mno. Nakumbuka niliwaeleza kuwa wastani wa miti tangu kupandwa hadi kuvunwa
inaweza kuchukua kuanzia miaka mine hadi kumi na kuendelea kutegemea na aina ya
miti, bidhaa unayotaka kuvuna, kiwango unachotaka kuvuna na hali ya udongo na
ya hewa ya mahali ulipopanda.
Mathalani; miti ya mbao
inachukua kuanzia miaka saba hadi kumi na tano tangu kupandwa hadi kuvunwa.
Miti ya fito(mirunda) inachukua miaka kuanzia minne hadi mitano mpaka kuvunwa.
Hii ina maana kwamba hawa asilimia 89% waliipuuza fursa hii kwa sababu
inachukua kuanzia miaka minne, saba, hadi kumi na tano.
Sasa tafakari hili:
waliosema kuwa kupanda miti ni kitu kisichofaa kwa sababu inachukua miaka
mingi(mf minne); kama leo wangalikuwa walipanda miti ya fito miaka mitatu
iliyopita, ingekuwa bado mwaka mmoja tu wavune. Cha kujiuliza ni hiki: Je,
katika miaka mitatu iliyopita hadi sasa wamefanya jambo gani la maana lenye
faida na tija kubwa kushinda uwekezaji
katika kilimo cha miti?
Jiulize swali la pili:
Shamba pamoja na miti la ekari moja ambalo huenda lingekugharimu (laki mbili
hadi sita-sawa sawa na nilivyoainisha maeneo ninayoyafahamu nilipoandika makala
ile); ambalo mwaka mmoja ujao(mwakani) wangeweza kuuza miti pekee kwa fedha si
chini ya milioni mbili huku ukibaki na ardhi kuwa mali yako; Je, kuna kitega
uchumi gani chenye thamani zaidi ya faida hiyo ambacho wamewekeza?
Kupitia tafakari hizo
kuna mambo utayagundua kuhusu sisi watanzania tuliowengi. Wengi wa watanzania
wanapenda sana hela za chapchap! Ukitaka umpate mtanzania mpe fursa inayoonesha
kuwa fedha itapatikana kesho, wiki ijayo, mwezi ujao na ikizidi sana mwaka ujao.
Ukitaka mtanzania asiwe rafiki yako, mweleze habari za kufanya mambo
yatakayoleta faida ama fedha kuanzia miaka mitano, kumi, ishirini ama hamsini
mbele. Kwanza hatakuelewa na pili atakupuuza.
Tatizo la pili
linalowakabili watanzania wengi ni uwezo mdogo wa kubaini fursa. Uwezo huu
mdogo umesbabishwa na mambo mawili; mosi ni uvivu wa kutafuta taarifa na pili
ni utamaduni mbaya wa kupenda kulalamika kila wakati.
Ninaposema kutafuta
taarifa ninamaanisha kutafuta, kusoma, kusikiliza, kutazama, kutafakari,
kuchakata na kuzielewa kwa umakini kabisa habari na mambo yenye uwezo wa kuleta
tija katika eneo fulani la maisha. Mathalani, kujua fursa kuhusu ardhi ni
kutafuta taarifa kuhusu mazingira, kilimo, hali ya chakula na mabadiliko ya
hali ya tabia nchi.
Ukijua kuwa tabia nchi
imebadilika pia ukifahamu kuwa yapo mashirika ya Magharibi ambayo yananunua
hewa ukaa inayotokana na miti; hutafanya mchezo linapokuja suala la kumiliki
ardhi na ukishamiliki ardhi hutaiacha utupu; bali utaipanda miti ili uboreshe mazingira
na ujiandae kukinga dola kutokana na kuuza hewa ukaa inayozalishwa na miti
iliyopo shambani kwako.
Sio tu kwenye habari ya
miti bali mtazamo huo unatakiwa kuwepo katika ubongo wa kila mtu anapoyatazama
maeneo yote katika maisha.Watanzania wangapi wapo makini linapokuja suala la
kutafuta taarifa za maana za kuwasaidia?
Jibu la swali hili ni
rahisi kwani linapatikana unapoyaangalia maisha ya watanzania wengi kiuchumi:
Ni maisha ya kubahatisha ambayo hayana uhakika kamili kiuchumi kwa miaka
ishirini ama hamsini ijayo. Tafuta watanzania mia moja, kisha waulize swali
hili, “Unategemea maisha yako kiuchumi yatakuwaje miaka 10 ijayo?”
Ninakuthibitishia kwamba watakaokuwa na uhakika wa maisha yao baada ya muda huo
hawatazidi wawili; waliobaki watakujazia porojo na kujitetea kwingi kulikojaa
kukata tama! Unajua tatizo linapoanzia?Nitakueleza.
Tatizo linaanzia katika
hulka ya watanzania wengi kuhangaikia na kuchekelea habari na taarifa nyepesi
nyepesi zinazojadili matukio, zinazojadili maisha ya watu; ambapo kimsingi
hazina chochote cha maana zaidi ya kuwafanya watu wazidi kuchanganyikiwa na
ugumu wa maisha. Bahati mbaya ni kwamba vyombo vyetu vingi vya habari
vinahangaika kujaza bongo za watanzania kwa matukio na taarifa nyepesi nyepesi
kiasi kwamba watanzania wengi wanaendelea kuwa wepesi mno wanapopimwa kwenye
mizani ya kiuchumi.
Jambo la pili
linalopelekea watanzania wengi kuwa “mambumbumbu” wa kubaini fursa ni hulka ya
kulalamika. Kulalamika huwa ninakufananisha na utumiaji wa madawa ya kulevya;
yanampa mtumiaji faraja kwa muda yawapo katika damu lakini yakiisha mtumiaji
anabaini kuwa hakuna kilichobadilika. Bila kujali ni nani aliyekusababishia
ugumu wa maisha, kulalamika hakuwezi kukuondolea ugumu wa maisha wala tatizo
linalokukabili.
Katika historia haijatokea
mahali popote mtu aliyewahi kupewa taji ama tuzo ya umahili wa kulalamika. Ni
kweli matatizo yapo, ni kweli kuna wakati serikali inakwama kufanya hili na
lile katika maeneo kadhaa; lakini kulalamika unapokabiliwa na matatizo na
kuilalamikia ama kuilaani serikali hakuwezi kukupa nafuu ya matatizo yako kwa
namna yeyote ile. Kulalamika huwa kuna zalisha upofu wa kutoona mambo yanayoweza
kukukwamua likiwemo suala la kubaini na kuzitumia fursa.
Lazima utembee na
mtazamo wa utele, lazima utembee na mtazamo unaoamini kuwa wewe ndie
unaewajibika kuboresha maisha yako; sio UKAWA, CCM wala CHADEMA! Kinyume na
hapo utaendelea kusema kuwa fedha ni ngumu ilhali wengine wanapata fedha kila
siku; tena katika mazingira hayo hayo uliyomo. Kulalamika hakuna mafuta yeyote
yanayoweza kulainisha ugumu wa maisha ama kusafisha matatizo!
Suala jingine ambalo
limekuwa sababu ya kupooza kwa hali za kiuchumi za mamilioni ya watanzania ni
kushindwa kusoma alama za nyakati. Waingereza wanasema “timing”. Kuna jambo
ambalo unaweza kuwa na uwezo wa kulifanya leo; ukilipuuza utajikuta huwezi
kufanya tena wakati ujao. Nitakupa mifano miwili.
Mosi; kuna mzee wangu
mmoja ambae alinionesha kiwanja kilichopo katikati ya mji hapa Iringa ambacho
alipuuza kukinunua kwa shilingi laki moja mwaka 1998, lakini mwaka 2013
kikauzwa kwa shilingi milioni mia mbili na themanini! Alichokoseani “timing”.
Mfano wa pili: Kabla ya
mwaka 2010 kuna maeneo katika wilaya za Kilolo na Mufindi ambapo ekari moja ya
shamba uliweza kununua kwa shilingi elfu ishirini (20,000/=) tu; lakini mara
baada ya kuingia makampuni ya uwekezaji katika kilimo cha miti; maeneo hayo sio
tu kwamba yamepanda mara dufu lakini pia hata kuyapata ni kwa mbinde.
Swali la kujiuliza ni hili: kwa nini
watanzania wengi tunakwama “timing” linapokuja suala la uwekezaji? Jibu lipo: ni kwa sababu hatupendi kutafuta taarifa za
maana, ni kwa sababu hatuna maono, ni kwa sababu hatuna mipango na malengo ya
muda mrefu, ni kwa sababu tunapenda hela za chapchap na ni kwa sababu tupo bize
mno kulalamika kiasi kwamba tunapokuja kushtuka tunabaki tukilia baada ya kila
fursa kuchukuliwa na “wengine” walio ‘bize’
Kabla sijahitimisha
makala hii leo ninapenda kulisema jambo lifuatalo. Huwezi kuwa mwekezaji ikiwa
huna tabia ya kujiwekea akiba pamoja na kutenga sehemu ya kipato chako maalumu
kwa ajili ya uwekezaji. Huwezi kuwa na mafanikio imara na ya muda mrefu kiuchumi ikiwa hutakuwa na
maono na mipango ya muda mrefu na ikiwa hutaachana na hulka ya kupenda fedha za
chapchap, fedha za madili na za mikato-mikato ambazo nyingi huwa hazina usafi
wala haki.
stepwiseexpert@gmail.com 0719 127 901
EmoticonEmoticon