TAARIFA KWA UMMA KUTOKA WIZARA YA KAZI NA AJIRA: UTEKELEZAJI WA TAMKO LA SERIKALI KUHUSU UENDESHAJI WA WAKALA BINAFSI WA HUDUMA ZA AJIRA NCHINI





 
Afisa Kazi wa Wizara ya Kazi na Ajira Bw. Themistocles Rumboyo akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuwa hadi kufikia Februari mwaka huu jumla ya maombi 56 ya makampuni ya huduma za ajira nchini yamewasilishwa kwa Kamishna wa Kazi. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bw. Ridhiwani Wema.

 
Afisa Kazi wa Wizara ya Kazi na Ajira Bw. Themistocles Rumboyo akiwaeleza waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuwa hadi kufikia Februari mwaka huu jumla ya maombi 56 ya makampuni ya huduma za ajira nchini yamewasilishwa kwa Kamishna wa Kazi. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bw. Ridhiwani Wema.

 
Afisa Kazi wa Wizara ya Kazi na Ajira Bw. Omari Sama akijibu swali la waandishi wa habari waliotaka kujua taratibu za kusajili wakala binafsi wa huduma za ajira hapa nchini. Kulia ni  Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bw. Ridhiwani Wema.
---

 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
 WIZARA YA KAZI NA AJIRA 

1.      Tarehe 27/1/2014, Wizara ya Kazi na Ajira ilitoa Tamko la Serikali kuhusu uendeshaji wa Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira nchini. Pamoja na mambo mengine Wizara imepiga marufuku Wakala kuajiri na kukodisha wafanyakazi na kuwataka Wakala na kampuni zilizo katika utaratibu huu ziwahamishie Wafanyakazi husika kwa Kampuni zilizokodishwa. Aidha, Wakala waliagizwa  wawasilishe upya maombi ya  usajili wa Uwakala kwa Kamishna wa Kazi.
 
2.    Hadi kufikia tarehe 28/02/2014, jumla ya maombi hamsini na sita (56) yamewasilishwa kwa Kamishna wa Kazi.
 
3.    Aidha Kampuni au Wakala zilizoomba usajili  tumewaarifu watupatie taarifa zifuatazo:
·         Katiba ya uendeshaji na usimamizi wa shughuli za kampuni au Wakala (Memorandum&Articles of Assocition).
 
·         Hati ya usajili wa kampuni (Certificate of incorporation).
·         Leseni ya Biashara(Business License).
 
·         Namba ya usajili wa mlipa kodi (Tax identification Number).
 
·         Wasifu wa Kampuni au Wakala pamoja na ujuzi  na uzoefu wa wataalamu au watumishi katika uendeshaji wa huduma za ajira(Company profile).
 
·         Uthibitisho wa Kampuni au Wakala kama analipa kodi kwa mujibu wa taratibu(The current tax clearance letter from Domestic revenue/larger tax payers department) 
 
·   Anuani kamili ya makazi(Permanent  physical company address) n.k.
 
Wizara itazitumia taarifa hizi katika upekuzi,ufuatiliaji,ukaguzi na utoaji uamuzi sahihi juu ya utoaji  vibali vya uendeshaji wa huduma za ajira nchini.
 
4.Baadhi ya Wakala tayari wamefuata agizo na wamesitisha utaratibu wa kukodisha wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuhamishia Ajira za wafanyakazi hao kwenye Makampuni husika. Aidha, Mawakala wengine wameomba kuongezewa muda ili waweze kukamilisha taratibu za kuhamisha wafanyakazi. Wizara imepitia kwa kina maombi haya na imekubali kuongeza muda wa miezi miwili kuanzia tarehe 28/02/2014.
5.Kufuatia upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya watu au makampuni kuhusiana na maudhui ya Tamko la Serikali, Wizara inapenda kusisitiza yafuatayo.
 
                      i. Kwamba, “Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira” inajumuisha  Mtu binafsi, Kampuni,Taasisi au chombo chochote kinachotoa huduma ya kuunganisha watafuta kazi na waajiri pasipo wakala wa huduma za ajira kuwa sehemu ya mahusiano ya kiajira yanayoweza kujitokeza baina ya watafuta kazi na Waajiri. Pia, inajumuisha utoaji wa huduma zingine zinazohusiana na utafutaji kazi kama vile kutoa ushauri nasaha wa ajira, kutoa taarifa za soko la ajira kwa watafuta kazi na waajiri.
 
ii.Kwamba, ukodishaji wa huduma (outsourcing of services) haujapigwa marufuku bali kilichopigwa marufuku ni ukodishwaji wa watu (outsourcing of persons). Hivyo ni marufuku kwa Wakala wa huduma za Ajira kuajiri na kukodisha wafanyakazi, au kuajiri kwa niaba ya kampuni nyingine na wakala hao kuwa sehemu ya mahusiano ya ajira yanayoweza kujitokeza baina ya watafuta kazi na Waajiri.
 
6.Mwisho, Wizara inapenda kusisitiza kuwa Mtu yeyote anayetaka  kufanya shughuli za huduma za ajira hana budi kuzingatia taratibu na kanuni chini ya Sheria ya Kukuza Huduma za Ajira Na. 9 ya 1999.
IMETOLEWA NA
SAUL.H.KINEMELA
KAMISHNA WA KAZI
03/04/2014
Previous
Next Post »