KANSA INAUA WANAWAKE 250,000 KILA MWAKA


uterine-cancer-2_d713d.jpg
Kansa ya mji wa uzazi
Na Albano Midelo
TAKWIMU zinaonyesha kuwa kila mwaka nchini Tanzania akina mama zaidi ya 8,000 hufariki dunia kutokana na matatizo mbalimbali ya uzazi.
Wanawake pia wanakabiliwa na tatizo jingine la kiafya ambalo ni ugonjwa wa saratani au kansa ya kizazi ambayo inaelezwa ndiyo inayoongoza katika kusababisha vifo vitokanavyo na kansa kwa akina mama waliopo katika nchi zinazoendelea.
Utafiti unaonyesha kwamba akina mama zaidi ya 500,000 hupatwa na ugonjwa wa kansa ya uzazi kila mwaka ulimwenguni, kati ya hao akina mama 250,000 hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huo ambapo hapa nchini inakadiriwa wanawake 4,000 wanakufa kila mwaka.
Ugonjwa wa saratani umekuwa tishio katika nchi za Afrika zilizo chini ya Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania ambapo kwa mwaka 2010, takwimu zinaonyesha ugonjwa huo umeua watu milioni 9.9 duniani.
Mratibu wa kampeni ya kupambana na ugonjwa huo nchini kutoka Taasisi ya Tanzania 50 Plus, Mchungaji Dk. Emmanuel Kandusi, amesisitiza kuwa saratani ni hatari ukilinganisha na takwimu za magonjwa mengine.
Takwimu za magonjwa za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2010 zinazoonyesha kuwa ugonjwa wa malaria uliua watu 500,000, kifua kikuu milioni 2.1, UKIMWI milioni 1.8 na Saratani iliongoza kwa kuua watu milioni 9.9.
Previous
Next Post »