Mshambuliaji wa klabu ya Juventus ya nchini Italia Carlos Tevez, huenda akaachwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Argentina, ambacho kitakwenda nchini Brazil kushiriki fainali za kombe la dunia.
Hati hati ya kutokuitwa kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, imeanza kujionyesha kufuatia kauli iliyotolewa na kocha mkuu wa timu ya taifa ya Argentina Alejandro Sabella, ambapo amesema kikosi chake kitazingatia uwepo wa wachezaji waliocheza siku za hivi karibuni.
Alejandro Sabella, ametoa kauli hiyo huku zikisalia siku 14 kabla hajatangaza kikosi chake ambacho kitaingia kambini tayari kwa maandalizi ya kujiandaa na fainali za kombe la dunia, ambazo zimepangwa kuanzia June 12 hadi July 13 mwaka huu.
Utaratibu wa kocha huyo unaonyesha wazi Carlos Tevez, huenda asiitwe kikosini kutokana na kutokuwa na sifa za kuitwa kwenye timu ya taifa siku za hivi karibu, kwani kwa mara ya mwisho alionekana akiwa amevaa jezi ya Argentina mwaka 2011.
"Nina siku chache kabla sijatangaza kikosi changu ambacho nitakwenda nacho nchini Brazil, hivyo nitazingatia utaratibu ambao nimejiwekea wa kuhakikisha wachezaji walioichezea timu hii katika siku za hivi karibuni ninawaita kikosini kwa sababu watakua wanaelewa nini ninacho kihitaji.” Amesema Sabella.
Alejandro Sabella, tangu ameingia madarakani mwaka 2011, hakuwahi kumuita kikosini Carlos Tevez, kutokana na sakata la utovu wa nidhamu lililokuwa likimiandama mshambuliaji huyo wakati akiitumikia klabu ya Man City ya nchini Uingereza.
Hata hivyo bado kauli ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 59 imeendelea kuwaweka njia panda mashabiki wa soka nchini Argentina ambao wanahitaji kumuona Carlos Tevez, anarejea kwenye kikosi cha timu ya taifa kutokana na kuamini kwamba huenda Sabella, akabadili mawazo kufuatia uwezo unaoonyeshwa na mchezaji huyo akiwa na klabu yake ya Juventus huko nchini Italia.
Kwa msimu huu wa mwaka 2013-14 Carlos Tevez, ameshajumushwa kwenye kikosi cha Juventus katika michezo 18, na amekua akifanya vyema kwa kuisaidia klabu hiyo kusogelea mafanikio ya kutetea taji la Scudeto.
EmoticonEmoticon