Kitoto kichanga kilichotelekezwa na wazazi wake kinyume cha sheria kikiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
N hali ya kushangaza, lakini ndivyo ilivyo, baadhi ya watu wanasaka watoto lakini wengine wanawapata na kuwatupa.Kisa hiki kimetokea jijini Dar es Salaam hivi karibuni ambapo mtoto huyo wa mwaka mmoja sasa anayelelewa Hospitali ya Taifa Muhimbili, wazazi wake wamekutana na mkono wa sheria na kutupwa Gereza la Segerea baada ya kubainika kuwa, walimtupa mtoto huyo huku wakijua ni kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka Idara ya Ustawi wa Jamii Muhimbili zinasema kuwa, wazazi hao ambao wametajwa kwa jina mojamoja, Peter na Happiness walikutana na kuishi kama mke na mume, baadaye mwanamke huyo alipata ujauzito na ulipotimiza miezi miwili, mwanaume huyo akaingia mitini.
Mmoja wa wasamaria wema akiwa amekibeba kitoto kichanga hicho Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, baada ya miezi tisa, Happiness alijifungua salama na kuanza kumlea mtoto wake. “Lakini baada ya mtoto huyo kufikisha miezi miwili, naye alimpa rafiki yake akamwambia ampeleke Kituo cha Polisi Magomeni na kuwaambia amemuokota njiani.
“Yule rafiki alifanya hivyo, akampeleka Polisi Magomeni ambapo alipokelewa, lakini kwa sababu alikuwa anaumwa, wakampeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alitibiwa na analelewa pale akiwa amepewa jina la Baraka,” kilisema chanzo.
Ilizidi kudaiwa kuwa, hivi karibuni, baba wa mtoto huyo alifika Muhimbili na kusema amepata habari kuwa kuna mtoto ameokotwa na ameambiwa ni wake.
“Ilibidi mwanaume huyo awekwe chini ya ulinzi na kuhojiwa ili aweze kuthibitisha kuwa mtoto huyo ni wake.
“Kazi hiyo ilifanyika, hatimaye mama wa mtoto alipatikana na kueleza mazingira yote yalivyokuwa“Kufuatia maelezo hayo, sheria ilichukua mkondo wake ambapo wazazi wote wawili walibainika kutenda kosa la kutelekeza mtoto kituo cha polisi kwa madai kuwa ameokotwa kitu ambacho kilikuwa ni cha uongo.
“Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na wazazi hao kutupwa Segerea wakisubiri taratibu zingine za kisheria,” kilisema chanzo.
EmoticonEmoticon