AZAM FC MABINGWA WAIPIGA MBEYA CITY MABAO 2 -1

 



RASMI Azam fc wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu sokA Tanzania bara msimu wa 2013/2014 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City FC kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Kwa matokoe hayo, Azam fc wamefikisha pointi 59 kileleni ambazo haziwezi kufikiwa na klabu yoyote ile, huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
Taarifa kutoka Mbeya zinaeleza kuwa mechi iliingia dosari baada ya wachezaji wa Mbeya City kumshambulia mwamuzi kutokana na kutoridhishwa na maamuzi yake.
Mtandao huu unafuatilia kwa kina kujua nini kilichosababisha tafrani hizo na baadaye utapata taarifa rasmi.
Mbeya City baada ya kuchapwa leo hii, wanabakia katika nafasi ya tatu kwa pointi 47.
Rasmi wameshajiengua kutafuta nafasi ya pili kwasababu hata kama watashinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Mgambo JKT aprili 19 watafikisha pointi 50 ambazo zimepitwa na Yanga.
Kwa mazingira hayo, Mbeya City wameshika nafasi ya tatu, Yanga ya pili na Azam fc ni mabingwa wapya.
Yanga waliokuwa wanafukuziana na Azam fc kuwania ubingwa wameshinda mabao 2-1 dhidi ya JKT Oljoro katika dimba la Shk. Amri Abeid jijini Arusha, lakini ushindi huo haujawasaidia chochote kutokana na ushindi wa Azam fc leo.
Yanga wamefikisha pointi 55, pointi nne nyuma ya Azam, huku timu zote zikisaliwa na mechi moja moja mkononi.
Hata kama Yanga watashinda mechi ya mwisho aprili 19 uwanja wa Taifa dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba sc hawataweza kufikia pointi 59 walizonazo Azam fc.
Mabingwa wapya wa ligi kuu, Azam fc watafunga pazia dhidi ya Maafande wa JKT Ruvu ambao kwa asilimia zote wamefanikiwa kukwepa kushuka daraja baada ya ushindi wa bao 1-0 walioupata jana katika dimba la Mkwakwani dhidi ya Coastal Union.
Mechi nyingine muhimu leo hii imepigwa katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam ambapo Wekundu wa Msimbazi Simba waliwakaribisha Wauza Mitumba wa Ilala, Ashanti United.
Mechi hiyo imemalizika kwa kocha Abdallah Kibadeni kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mcroatia wa Simba sc, Dravko Logarusic.
Kwa matokeo hayo, Ashanti United wanapata unafuu wa kusalia ligi kuu, huku wakisubiri mechi ya mwisho dhidi ya Prisons aprili 19 mwaka huu uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro.
Sasa Ashanti wamefikisha mechi 25 na kujikusanyia pointi 25 sawa na Prisons walioshinda mabao 4-3 jana dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora, lakini Wajelajela wanakuwa juu yao kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Endelea kufuatilia mtandao huu ambapo baadaye utajuzwa kwa undani matokeo ya mechi zote za leo na kufahamu msimamo mzima wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Utafahamishwa timu gani ipo katika hatari ya kushuka daraja na timu zipi zitaambulia nafasi za katikati , na tathmini ya Azam fc kutwaa ubingwa wao wa kwanza tangu wamepanda ligi kuu msimu wa 2008/2009.
Previous
Next Post »