Hali ya kutokubaliana katika masuala kadhaa ilisababisha baadhi ya wajumbe kumtaka Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir Kificho aeleze iwapo Bunge hilo lingeendelea au la kutokana na utata wa kisheria na kikanuni kuhusu ibara na sura zitakazokataliwa na wajumbe kwa kura.
Akichangia mjadala wa kanuni mjumbe, Dk. Francis Michael aliitaka Kamati ya Mashauriano kuhusu vipengele vyenye ushindani ikae chini na kutoa ufumbuzi kuhusu utata huo.
"Inabidi tuwe na uamuzi, hapa tunataka Katiba Mpya au hapana. Hapa tunatumia fedha za walipa kodi. Kuna hoja ambazo zinaonyesha kabisa kuwa zikifika hapa zitagonga ukuta," alisisitiza.
Dk. Michael alipendekeza wanasheria na wakuu wa Serikali wa pande zote za Muungano kutafuta suluhisho mapema.
"Ni afadhali tuamue kabla hatujaendelea mbele kwa sababu hakuna mantiki ya kuendelea kukaa hapa wakati tunajua kuna hoja ambazo zinaweza zisifikie ufumbuzi," alisisitiza Dk. Michael.
"Kwa hiyo mheshimiwa mwenyekiti kama kichwa hakikupata solution (suluhisho) huko mbeleni sijui tunakwenda kujadili vipi hii rasimu... hapa ni mahali pa kuangalia sana," alisisitiza Hassan.
Naye Christopher Ole Sendeka alisema suala hilo la kupitisha ibara kwa kuzingatia wingi wa theluthi mbili za kura halihitaji ushabiki wowote ndani ya Bunge. Kanuni inataka iwapo ibara haikupitishwa kwa theluthi mbili ya wajumbe, ipelekwe katika Kamati ya Mashauriano ili kukarabatiwa na kurudishwa na baadaye kupigiwa kura kwa mara ya pili.
Iwapo wajumbe watapiga kura kwa mara ya pili na bado ikashindwa kupita, ibara hiyo itaondolewa kabisa. "Mnajadiliana iwapo Tanzania ni Shirikisho ama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inapigwa kura mnakosa theluthi mbili Zanzibar na Tanzania Bara, mtatakoje hapo?" Alihoji.
Kutokana na mkanganyiko huo, Sendeka alipendekeza wanasheria waliobobea wakae na Serikali na kukubaliana ikitokea hali hiyo, njia ipi itatumika kulinusuru Bunge lisivunjike. Pauline Gekul alisema kanuni inayozungumzia wingi wa kura katika upitishaji wa ibara imewaacha hewani kuhusu nini kitatokea kama ibara zitashindikana kupitishwa. Gekul alipendekeza kuwa badala ya ibara au sura ambayo haikupitishwa kuondolewa, alishauri suala hilo lipelekwe kwa wananchi kuamuliwa kwa wingi wa kura badala ya kuziondoa.
Naye Ummy Mwalimu alipendekeza wakati wa kupitisha ibara katika hatua ya kamati, suala hilo lipitishwe kwa kuzingatia uwiano wa zaidi ya asilimia 50 kutoka pande zote za Muungano badala ya theluthi mbili.
Bunge kubadili vifungu?
Mtaalamu aliyebobea katika masuala ya sheria, Dk. Akson Tulia alisema Bunge hilo linayo mamlaka ya kisheria kubadili muundo mzima wa Ibara na Sura za Rasimu ya Katiba.
Akijibu hoja mbalimbali za wajumbe katika Semina ya Bunge hilo juzi, Dk. Tulia alisema Kamati ya Uongozi ndiyo yenye mamlaka ya namna sura za Rasimu ya Katiba zitakavyogawanywa.
"Naomba niwakumbushe wajumbe kwamba tumepitisha kanuni ya 32(1) inayotoa mamlaka ya namna sura zitakavyogawanywa na katika hilo Kamati ya Uongozi ndiyo itakayoamua," alisema.
Dk. Tulia alisema: "Kamati ya Uongozi itajua miguu ni ipi, kichwa ni kipi na waanzie wapi."
Alisema kwa zile sura na ibara zitakazokataliwa kwa kukosa wingi wa theluthi mbili ya kura kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, zitaondolewa kabisa kwenye rasimu.
Kauli ya Dk. Tulia, ambayo aliitoa wakati akijibu hoja mbalimbali za wajumbe kwa niaba ya Kamati ya Kanuni, ilionekana kuwakanganya zaidi wajumbe kuliko kuwapa mwanga.
Chanzo:Mwananchi
EmoticonEmoticon