Siri nzito; Kichefuchefu, kutapika wakati wa ujauzito soma hapa


Wanawake wajawazito hutapika wakati mimba bado ni changa na hali hii huisha mimba inapokomaa na kufikia wiki 16, ingawa kwa wengine huweza kuendelea kutapika hadi wakati wa kujifungua.PICHA|MAKTABA 
Katika hili hakuna mpaka kwamba wanawake wengi duniani huumwa wakati wa ujauzito.
Maradhi yao kwa lugha ya kitaalamu huitwa, maradhi ya asubuhi au kwa lugha ya Kiingereza ‘morning sickness’.
Kwa kawaida, wanawake wajawazito hutapika wakati mimba bado ni changa na hali hii huisha mimba inapokomaa na kufikia wiki 16, ingawa kwa wengine huweza kuendelea kutapika hadi wakati wa kujifungua. 
Hali ya kujisikia kutapika kwa kawaida huweza kudumu kwa saa moja hadi saa nne na wengine huweza kutapika wakati wote wa siku huku wengine wakitapika asubuhi au jioni. 
Watalaamu wanaeleza kuwa nusu ya wanawake wote duniani wanaoshika ujauzito hujisikia kuumwa wakati huo hivyo jambo hilo hutajwa kuwa ni la kawaida.
Kwa kawaida kutapika huanza wakati mimba ipo katika wiki ya tisa.
Profesa Malise Kaisi, ambaye ni baktari bingwa mstaafu wa masuala ya uzazi nchini anasema, kutapika kwa wanawake au kuchukia watu, aina fulani ya chakula au wakati mwingine harufu ni kitabu kilichofungwa au kwa lugha nyingine ni siri nzito.
“Hakuna wataalamu walioweza kubaini kwa nini wanawake hutapika wakati wa ujauzito, inawezekana ni homoni, lakini haijathibitishwa, inawezekana na kuumbwa kwa kiumbe kipya na hivyo tumboni kuwa na jambo geni, nayo pia haijathibitishwa,” anasema.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Cyriel Massawe  wa Hospitali ya Muhimbili (MNH) anasema, kwa ujumla, hakina sababu maalum inayoweza kutajwa kusababisha mwanamke mjamzito kutapika wakati huo  yapo mambo mengi yanayochangia hali hiyo.
Anasema mwili huwa na mabadiliko makubwa ambayo husababishwa na kuumwa kwa kiumbe tumboni hali hiyo huubadilisha mwili kwa kiasi kikubwa na kusababisha mabadiliko hayo.
‘Kwa jumla, vichocheo vya  huweza kusababisha mambo mengi, hali ya maisha ya mwanamke huweza kubadilika ingawa hutofautiana kati ya mwanamke mmoja na mwingine,” anasema.
Anasema, mabadiliko hayo ya vichocheo huweza hata kumfanya mwanamke mjamzito kuwa na mitazamo tofauti na baadhi ya vitu kwa mfano kuchukia harufu ya vitunguu, kumchukia mtu fulani au eneo fulani.
CHANZO:MWANANCHI
Previous
Next Post »