Matukio makubwa yaliyotikisa nchi mwaka 2013

obama-tanzania2
Rais Obama atua nchini Tanzania salama
Rais wa Marekani Barack Obama aliwasili katika ardhi ya Tanzania, Jumatatu majira ya mchana, Julai 1 katika ratiba yake ya mwisho wa ziara barani Afrika.
Wadadisi na wachambuzi wa masuala ya Kiuchumi na kisiasa walieleza kuwa ziara ya Rais Obama inasemekana ililenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Afrika huku kukiwa na wasiwasi kuwa Marekani inaachwa nyuma na China katika uhusiano wao na Afrika.
Obama_Tanzania-06f91
Obama aliwasili Tanzania baada ya ziara yake ya Afrika Kusini ambako rais mstaafu Nelson Mandela alikuwa anaugua kabla umauti haujamfika tarehe 5 Desemba mwaka huu.
Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete na familia yake pamoja na maafisa wake wa serikali na wacheza densi za kitamaduni walimkaribisha Obama na familia yake mjini Dar es Salaam.
Baadaye Rais Kikwete alimuongoza Rais Obama kuelekea Ikulu ya Tanzania kwa ajili ya shughuli zingine.
********************
01 (1)
Uzinduzi wa Rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya
Kwa mara ya kwanza kwenye historia ya Tanzania, Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini ilizindua rasmi rasimu ya Katiba Mpya nayo ilikuwa siku ya Jumatatu majira ya asubuhi Juni 3 mwaka 2013 iliyosheheni mapendekezo kadhaa ikiwemo suala la uwepo wa Serikali Tatu, ikipendekeza uwepo wa mgombea binafsi, mshindi wa urais atastahili kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote lakini pia imependekeza kuundwa kwa Mahakama ya Juu ikiwa miongoni mwa yale yaliyopo katika rasimu hiyo!!
Makamu wa Rais wa Tanzania Dr Mohammed Gharib Bilali alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo wa rasimu ya katib mpya.
*****************
Dkt Mvungi
Kufariki kwa Dk Mvungi
Moja ya matukio yaliyoshtua wengi ni kufariki kwa gwiji la sheria hapa nchini tena sheria ya katiba na mjumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba na Mkurugenzi wa katiba, sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi, Dkt Sengodo Adrian Edmud Mvungi ambaye alifariki tarehe 12 mwezi Novemba mwaka huu nchini Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa na watu wanaosadikiwa ni majambazi.
Taarifa za kifo chake zilithibitishwa na Mwenyekiti Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Dk Mvungi ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alijeruhiwa kwa kukatwa na mapanga kichwani nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kulazwa Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (Moi) na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Milpark, Johannesbarg, Afrika.
********************
IMG_95770
Kuuawa kwa Padre Evarist Mushi Huko Zanzibar.
Hali haikuwa shwari nchini baada ya Padri Mushi ambaye alikuwa ni Paroko wa Parokia ya Minara Miwili – Zanzibar kuuwawa kinyama kwa kupigwa risasi .
Padri huyo aliuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mida ya saa moja asubuhi akielekea kanisani hiyo ilikuwa Februari, 17 mwaka huu.
Taarifa zilisema kuwa Paroko wa Kanisa la Katoliki Minara Miwili Zanzibar, Evarist Mushi alifariki dunia baada ya kupigwa risasi saa 1.00 asubuhi na kufariki kabla hajafika hospitali ya Mnazi Mmoja. Paroko huyu amepigwa risasi akishuka katika gari lake wakati akienda kuendesha ibada ya saa 3.00 leo.
Padri Evarist Mushi alipigwa risasi kichwani na kufa papo hapo na watu wasiojulikana akiwa njiani anaenda kuendesha misa katika Kanisa la Mt.Theresia eneo la Mtoni Zanzibar.
*****************
Julius-Nyaisanga
‘Uncle J’ naye alitangulia mbele za haki
Morogoro/Dar es Salaam. Mtangazaji mkongwe nchini, Julius Nyaisanga ‘Uncle J’ (53), alifariki dunia oktoba 20 mkoani Morogoro baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kisukari na moyo.
Meneja wa Matangazo wa Kituo cha Abood Media ya Morogoro, Abeid Dogoli alisema Nyaisanga alifariki dunia jana saa moja asubuhi katika Hospitali ya Mazimbu, Manispaa ya Morogoro alikokuwa amelazwa.
Nyaisanga alikuwa miongoni mwa wakuu wa idara katika Kituo cha Televisheni cha Abood Media.
Dogoli alisema kuwa taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa marehemu Kihonda na kwamba wanatarajia kumsafirisha kwenda nyumbani kwao mkoani Mara kwa maziko ingawa taarifa zaidi zitatolewa kama kutakuwa na mabadiliko.
Akizungumzia kifo hicho, mke wa mtangazaji huyo, Leah Nyaisanga alisema hali ya mumewe ilibadilika ghafla kwa kuzidiwa ambapo juzi aliwahishwa katika Hospitali ya Mazimbu ambako alifikwa na mauti.
Marehemu Nyaisanga ameacha watoto watatu ambao ni  Samuel, Noela na Beatrice.
Nyaisanga aling’ara Radio Tanzania
Nyaisanga ni kati ya watangazaji waliong’arisha tasnia ya utangazaji nchini Tanzania na hata nje ya nchi.
Alianzia kazi RTD, pia aliwahi kufanya kazi katika Kampuni ya IPP akiwa kama mtangazaji na baadaye Mkurugenzi wa Radio One.
Pia alifanya kazi na Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle), Sauti ya America, Redio Japan na Ghana.
************************
zkwasanii2
Kuvuliwa uongozi kwa Zitto, Dkt Mkumbo na Samsoni Mwigamba .
KAMATI Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema November 22 mwaka huu kiliwavua Uongozi Viongozi wake watatu baada ya Kugundua waraka wa Siri uliowahusisha na mpango wa kukipasua Chama vipande vipande.
Viongozi waliovuliwa Uongozi ni Zitto Kabwe ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Dr Kitila Mkumbo na Samsoni Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini.
Akizungumza katika Mkutano wa Waandishi wa Habari Mh Tundu Lissu amesema katika Waraka huo kulikuwa na mtu anayejukana kama MM ambaye ni Naibu Katibu mkuu Zitto Kabwe, M1 ni Dr Kitila Mkumbo, M3 ni Samsoni Mwigamba na M2 hajajulikana ambaye ni mtumishi wa makao makuu ya Chadema.
Mh Lissu amesema Dr Kitila Mkumbo alikana kabisa kumfahamu M2. Mh Tundu Lissu anasema Waraka huo uliojulikana kama Waraka wa Ushindi unavunja katiba ya Chama kwa sababu umepandikiza chuki za kidini, majungu na kukashifu viongozi wa Chama kinyume na katiba ya CHADEMA.
Mh.Tundu Lissu amesema tuhuma zote zilizoko katika waraka huo hazijawahi kuwasilishwa kwenye kikao chochote halali cha chama kinyume na matakwa na masharti ya katiba yetu.
******************
MAANDAMANOMTWARA11
Mgogoro wa Gesi uliotokea Mtwara.
Chanzo cha vurugu kuhusu gesi zilizotokea kati ya Juni 1 na 2 mkoani Mtwara mwaka huu, ilielezwa kuwa ni vuguvugu la kisiasa lililowaingia wananchi kiasi cha kujenga chuki kubwa dhidi ya Serikali baada ya kupata mahubiri ya wanasiasa.
Inaelezwa kuwa mzozo huo ulianza rasmi mwaka jana baada ya Serikali kuituma kamati ya kuratibu Maoni ya Sera ya Gesi ambayo ilifika mkoani Mtwara, Novemba 16, mwaka jana kukusanya maoni ya wananchi.
Katika mikutano yake mjini Mtwara, inaelezwa kuwa wananchi wengi hawakukubaliana na wazo la kusafirisha gesi kwenda nje ya Mtwara kwa njia ya bomba.
Hali hiyo ndiyo iliyowafanya viongozi wa vyama vya NCCR-Mageuzi, TLP, UDP, ADC, DP, APPT Maendeleo, Sau na Chauma, kuungana na kuhamasisha wananchi kuhusu suala hilo.
***************
kejeli
Hali tete ya kidiplomasia kati ya Rwanda na Tanzania
Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete aliamua kutangaza rasmi kuwa mgogoro baina ya Tanzania na Rwanda umemalizika rasmi.
Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, Rais Kikwete amesema hatua hiyo inafuatia mazunguzo baina ya viongozi hao wawili yaliyofanyika hivi karibuni nchini Uganda.
Kwa miezi kadhaa mwaka huu Tanzania na Rwanda zimekuwa katika mgogoro wa kidiplomasia baada ya Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete kuishauri Rwanda pamoja na Uganda kuzungumza na waasi wa nchi zao waliopo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Japo hajataja ni kwa namna gani mgogoro huo uliokuwa umefukuta baina ya Tanzania na Rwanda na vipi umepata ufumbuzi, Rais Jakaya Kikwete amesema hatua ya mazungumzo baina yake na Rais wa Rwanda Paul Kagame ndio chanzo cha mafanikio hayo yote.
Tanzania na Rwanda ziliingia katika mgogoro wa kidiplomasia hadi kufikia hatua ya kutunishiana misuli kisiri siri baada ya Rais Jakaya Kikwete kushauri nchi ya Rwanda na Uganda kuzungumza na waasi wa nchi zao waliopo nchini Jamuhuiri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Jambo lililopingwa vikali na Rwanda kwa madai kwamba Rais Kikwete aliingilia mambo ya ndani ya Rwanda kwa kuwashauri kufanya mazungumzo na watu walioua raia wa nchi hiyo.
Mgogoro huu ulipamba moto na hata kukolezwa na zaidi na vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii. Sasa Rais anavyoomba vyombo vya habari Wanasiasa pamoja na mitandao ya kijamii kusaidia kwa upande mwingine kuziba ufa wa uhusiano uliobomolewa.
**********************
mawaziri (1)
Mawaziri 4 wabwagwa sakata la Tokomeza Ujangili
FUNGA Kazi au Tisa Kumi ilikuwa ni hivi karibuni baada ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wane kufuatia shutuma nzito dhidi yao katika sakata la Oparesheni Tokomeza Ujangili.
Mawaziri waliopoteza ajira zao usiku huu ni Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), David Mathayo (Mifugo na Uvuvi), Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT).
Akizungumza Bungeni Dodoma usiku wa Desemba 19 mwaka huu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikiri kulikuwa na matatizo makubwa katika usimamizi wa zoezi hilo.
“Tulifanya operesheni kwa nia nzuri,” alisema Waziri Mkuu Pinda. “Tatizo ni namna operesheni hiyo ilivyotekelezwa.”
Katika mdahalo uliogusa nyoyo za wabunge na wachambuzi mbalimbali wa siasa, wabunge waliueleza umma jinsi ambavyo Operesheni hiyo ilitumika kutesa, kunyanyasa na kuua raia wasio na hatia na kuwadhulumu mali zao.
Previous
Next Post »