Siasa Uchumi ya Umasikini Tanzania



The Bottom 30M: Rural Tanzania
Siasa Uchumi ya Umasikini Tanzania

Zitto Kabwe, Mb
(Makala hii imetolewa kwenye utangulizi wa Kijitabu kuhusu Hoja Binafsi ya Mkonge iliyowasilishwa Bungeni katika Mkutano wa Sita wa Bunge la Kumi. Makala inajenga hoja kwamba Mkulima mdogo ndio jawabu la changamoto ya Umasikini nchini Tanzania. Zao la Mkonge ni mfano tu wa hatua mwafaka)


Sekta ya Kilimo ni sekta ambayo inazungumzwa sana kama sekta kiongozi katika Maendeleo ya Taifa letu. Kumekuwa na kauli mbiu mbalimbali za kuhamasisha Kilimo toka nchi yetu ipate uhuru. Mfano Azimio la Iringa la Siasa ni Kilimo, Kilimo cha Kufa na Kupona, Kilimo cha bega kwa bega na sasa Kilimo Kwanza! 
Kumekuwa na mipango mbalimbali inayoandaliwa na Serikali kuhakikisha kwamba Kilimo kinakuwa cha kisasa na hivyo kuzalisha chakula cha kutosha na pia mazao mengi ya biashara hivyo kuongeza kipato kwa mwananchi mmoja mmoja, kukuza pato la Taifa na kuongeza thamani ya mauzo yetu nchi za nje. 
Hata hivyo juhudi hizi kwa kiasi kikubwa hazijazaa matunda kwa kiwango cha kuridhisha.
Taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na Serikali inaonyesha kwamba Sekta ya Kilimo haijakua kiasi cha kutosha na kuweza kupunguza umasikini wa Watanzania! 
Taarifa hiyo inayoitwa Taarifa ya Umasikini na Maendeleo ya mwaka 2011 inasema kwamba mchango wa sekta ya Kilimo katika Pato la Taifa (GDP) umeporomoka kutoka asilimia 29 mwaka 2001 mpaka asilimia 24 mwaka 2010. 
Kuporomoka huku yawezekana kunachangiwa na kukua kwa sekta nyingine kama ile ya huduma au uzalishaji viwandani katika kipindi hicho. Hata hivyo kasi ya ukuaji wa Sekta ya Kilimo katika kipindi cha muongo huo (2001 – 2010) ilikuwa ni asilimia 4.3 chini kabisa ya kiwango kilicholengwa katika Mkakati wa kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA). 
Kwa mujibu wa MKUKUTA ili Tanzania iweze punguza umasikini kwa wananchi wake na kuondoa nusu ya Watanzania katika dimbwi la Umasikini ilipaswa sekta ya Kilimo ikue kwa kasi ya 10% kwa miaka mitatu mfululizo. 
Haikuwezekana katika miaka 10 ya kutekeleza MKUKUTA, Umasikini ulishuka kwa 2 tu kutoka watu 37 kati ya watu 100 kuwa masikini wa kutupwa mpaka watu 35. Kwa nini?
Hapo ni mahala pazuri sana pa kuanzia! KWA NINI Watanzania ni masikini wakati Taifa lao Tajiri? Kitendawili hiki cha Nchi Tajiri kwa rasilimali lakini wananchi wake zaidi ya theluthi kuwa mafukara kinajibiwa namna gani?
Jibu la Kitendawili hiki ni rahisi sana! Kilimo ndio sekta inayoajiri robo tatu ya Watanzania wote. Kilimo cha mazao yanayoitwa ya chakula na yale ya Biashara ndio sekta tegemezi kwa Watanzania wengi sana. 
Kwamba Sekta ya Kilimo kukua kwa kasi ndogo kama inavyoonekana katika takwimu zinazotolewa na Serikali inathibitisha kwamba Umasikini wa Tanzania umejikita vijijini ambako wanategemea kilimo kwa maisha yao ya kila siku! Hivyo jibu la kitendawili lipo kwenye Kilimo. 
Sekta nyigine za Uchumi hata zikue namna gani hazitajibu kitendawili hiki kwa uendelevu.
Kwa mfano Sekta ya Viwanda imekuwa ikikua kwa wastani wa asilimia 8 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. 
Ukuaji huu wa sekta ya Viwanda ulikuwa chini ya malengo ya Mkukuta kwani mkukuta uliweka lengo la 15%. 
Lengo halikufikiwa kwasababu kwa uchumi kama wa Tanzania viwanda vitakavyoanza kukua na kuwa na maana kwa maisha ya wananchi ni viwanda vya bidhaa za kilimo. 
Hivyo kwa kuwa Sekta ya Kilimo haikuwa na kasi nzuri ya kukua, sekta ya viwanda nayo inaathirika. 
Kwa kuwa Sekta ya Kilimo ilikua kwa kasi ndogo na mahusiano kati ya sekta ya viwanda na sekta ya Kilimo ni dhaifu malengo ya kukuza ajira,kuongeza kipato na kupunguza umasikini yalishindwa kufikiwa.
Pili Sekta ya Madini ambayo ilikuwa inakua kwa kasi sana katika kipindi cha mwanzo mpaka kati cha muongo huu na baadaye kuporomoka kutoka ukuaji wa asilimia 15% mwaka 2007 mpaka asilimia 2 mwaka 2009 inachangia kidogo sana katika Pato la Taifa.
 Licha ya kwamba Madini huchangia takribani 48% ya mauzo yote ya Tanzania nje mchango wake katika Uchumi ni asilimia 3 tu Sababu kubwa ni kwamba kuna mahusiano dhaifu sana kati ya sekta ya Madini na sekta nyingine za uchumi na hasa Kilimo na pia Viwanda.
Tatu Sekta ya Huduma ambayo ndio sekta kubwa kuliko zote katika Uchumi wetu inachangia 44% ya Pato la Taifa nayo pia ina mahusiano dhaifu na Sekta ya Kilimo. 
Utalii huchangia zaidi ya nusu ya sekta yote ya huduma (17% ya uchumi- GDP) na asilimia 40% ya mauzo nje ya nchi. Hata hivyo kwa kuwa sekta ya kilimo haikui vya kutosha na kuimarisha mahusiano na sekta hii bado mafanikio haya yanashindwa kusaidia kutokomeza umasikini nchini. 
Ndio maana jibu la kitendawili cha kuwa na Nchi Tajiri yenye Watu Fukara lipo kwenye sekta ya Kilimo.
Kijitabu hiki kimeandikwa ili kuonyesha juhudi mojawapo ya kutaka kujibu kitendawili hiki!
 Juhudi hizi zimefanywa na mwandishi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwasilisha Hoja Mahususi ya Bunge ili Bunge liazimie na kuielekeza Serikali kuchukua hatua madhubuti za kujibu kitendawili cha Utajiri na Umasikini wa Tanzania. 
Jibu linalotakiwa ni la kusawazisha mambo, kwamba Nchi yetu Tajiri kwa rasilimali iwe pia Tajiri wa maendeleo ya watu. 
Inafahamika wazi kabisa kwamba Hoja hii iliyotolewa kama hoja Binafsi Bungeni katika mkutano wa Sita wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa ni hatua tu ya kuanza kutafuta majibu ya kitendawili cha Tanzania: Nchi Tajiri, Watu Fukara.
Ili kutokomeza Umasikini Tanzania ni lazima juhudi ziwekwe katika sekta ya Kilimo. Tumeona hapo juu kwamba Uchumi wa Tanzania umekua ukikua kwa takribani asilimia 7 kwa mwaka kwa miaka kumi. 
MKUKUTA ulitaka uchumi ukue kwa wastani wa asilimia 6-8 kwa kipindi chote hiki ili kuondoa nusu ya Watanzania masikini katika dimbwi hilo na kuwafanya wawe na ahueni katika maisha. 
Asilimia 7 ya kasi ya kukuza uchumi imo ndani ya kiwango kilichotakiwa lakini Watanzania walioondolewa katika dimbwi la umasikini  ni asilimia 2 tu.
 Kwa hiyo kasi hii ya ukuaji wa uchumi, kasi kubwa sana duniani maana uchumi wa Tanzania ni miongoni wa chumi 20 duniani zinazokua kwa kasi, ilikuwa hewani.
 Uchumi ulikua bila kutengeneza ajira za kutosha na hivyo kushindwa kuondoa wananchi katika dimbwi la Umasikini. 
Hii ni kwa sababu Sekta ya Wananchi wengi(Kilimo) haikukua inavyopaswa. Uchumi ulikuzwa na Sekta zinazofaidisha wachache kama Madini, Mawasiliano na Utalii. 
Suluhisho la kutomeza umasikini nchini Tanzania lipo kwenye sekta ya Kilimo na uongezaji thamani wa bidhaa za Kilimo.
Ili kuchangia katika kuleta suluhisho nilitoa hoja Bungeni ambayo ililenga kufufua kilimo kupitia zao mojawapo nchini.
 Lengo kubwa la Hoja la hii lilikuwa kurudisha hadhi ya Taifa letu katika zao la Mkonge. Lengo ni kufanya kilimo cha Mkonge kiongozwe na wananchi wakulima wadogo. 
Badala ya Wananchi kuwa vibarua na wapagazi katika mashamba yanayomilikiwa na matajiri tunataka Mkonge ulimwe na mkulima mdogo na Serikali imsaidie kama inavyosaidia wakulima wakubwa. 
Tulitaka pia Kilimo cha Mkonge kisambae nchi nzima na sio mikoa iliyozoeleka peke yake. Mkonge unaweza kutoa ajira zaidi ya milioni moja kwa Watanzania na kujiongezea kipato hivyo kuondoa umasikini miongoni mwao.
 Mkonge unaweza kuongeza mauzo ya nchi yetu nje na hivyo kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
Previous
Next Post »