Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameahidi kuwa Serikali yake imedhamiria na itahahakisha kuwa inalimaliza balaa la watu kumwagiwa tindikali iwe ni Zanzibar ama Tanzania Visiwani.
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa katika siku za karibuni Jeshi la Polisi lilifanya operesheni kubwa katika mitaa ya Zanzibar ambako watu 10 wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kushiriki mipango ya kuandaa na kutekeleza vitendo hivyo.
Rais amemwambia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Mheshimiwa Ban Ki Moon kuwa chimbuko la tatizo hilo lina sura nyingi lakini hakuna shaka kuwa katika kipindi kifupi iwezekanavyo Serikali itafikisha tatizo hilo mwisho wake.
Rais Kikwete ametoa msimamo huo wa Serikali kuhusu vitendo ambavyo vimekuwa vinaongezeka vya watu mbali kushambuliwa kwa kumwagiwa tindikali, tatizo ambalo kimsingi lilitokea kwa mara ya kwanza Zanzibar wakati kiongozi maarufu wa Kiislamu Sheikh Soroga alipomwagiwa tindikali akifanya mazoezi ya viungo asubuhi moja kwenye mitaa ya mji wa Unguja.
Rais Kikwete ametoa msimamo huo wakati alipokuwa anazungumza na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ofisini kwake mjini New York, Marekani, Ijumaa, Septemba 27, 2013 baada ya kuwa ameulizwa jambo hilo na Mheshimiwa Ban Ki Moon kuhusu tatizo hilo.
“Ni kweli tumekuwa na vitendo hivyo, zaidi Visiwani Zanzibar kuliko Bara ambako hata hivyo nako vimekuwepo vitendo hivyo. Ni jambo la kulaaniwa sana na karibuni Jeshi la Polisi lilifanya operesheni maalum na msako mkubwa Tanzania Visiwani ambako watu 10 wametiwa mbaroni na watafikishwa katika vyombo vya sheria.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Wakati lilipoanza tatizo hilo, tulidhani kuwa alikuwa ni Sheikh Soroga aliyekuwa anatafutwa peke yake na watu ambao walikuwa hawakubaliani kisiasa na msimamo wake,lakini mara wakaanza kushambuliwa watu wengine wakiwemo wasichana wawili wa Uingereza ambao walikuwa wanafanya kazi za kujitolea tu. Tatizo hili ni lazima likome.”
EmoticonEmoticon