MLOLONGO wa matukio ya kigaidi dhidi ya raia, yanayotekelezwa na watu ambao vyombo vya dola vimeshindwa kuwabaini na kuwatia nguvuni, yameichafua Serikali kwa kiwango cha kuivika taswira ya mamlaka inayonuka damu. (HM)
Matukio ya raia kutekwa na kuteswa kinyama kwa kutobolewa baadhi ya viungo vyao vya mwili, kumwagiwa asidi aina ya tindikali na hata mauaji yanayotokea katika mijumuiko ya kisiasa ambayo mara nyingi yamekuwa yakidaiwa kuwa na mkono wa Jeshi la Polisi, huku wahusika wakishindwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani, ndiyo yaliyoibua hisia miongoni mwa jamii inayoielekezea Serikali lawama za namna hii.
Tayari baadhi ya wanasiasa wenye ushawishi hapa nchini, viongozi wa dini, wasomi na wanaharakati wa haki za binadamu, wamekwishakaririwa kwa nyakati tofauti wakieleza kuwa Serikali ama inapaswa kubeba lawama ama inahusika kwa namna moja au nyingine na matukio hayo ya kigaidi.
Kauli hizi, zimekuwa zikipata nguvu kutokana na ugoigoi ambao umekuwa ukionyeshwa na Serikali katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi ambayo sasa yameanza kuota mizizi licha ya baadhi ya wahanga wa mashambulio ya kigaidi kutoa madai mazito kwa vyombo vya usalama kwa ujumla au baadhi ya watumishi wa idara hizo kushiriki kuwatendea unyama huo.
Tukio la hivi karibuni la kumwagiwa tindikali kwa Padre wa Kanisa Katoliki huko Zanzibar, Anselmo Mwang'amba, likiwa limetanguliwa na matukio mengine kadhaa ya aina hiyo yaliyotokea katika kipindi kifupi nyuma kwa raia wa kigeni, wananchi wa kawaida na viongozi wa dini ya Kiislamu, ndilo linaloonekana kuizamisha Serikali kwenye tope hili, baada ya baadhi ya mapadre kuinyooshea kidole moja kwa moja Serikali kuwa chanzo cha kutekelezwa kwa uovu huo.
Padre Mwang'amba alimwagiwa tindikali na watu ambao hawajafahamika, wakati akiwa nje ya mgahawa wa Internet, huko Zanzibar, lakini baadhi ya mapadre wenzake waliomsindikiza Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi, walilieleza kuwa wanaamini waliotekeleza uhalifu huo ni watu wanaotaka sauti za Wazanzibari za kuukataa muundo wa sasa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zisikilizwe.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Jimbo Katoliki la Zanzibar, Padre Arbogast Mushi, wiki iliyopita alisema kuwa, sauti za wananchi wa Zanzibar zinasikika zikiupinga muungano wa sasa wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema, matukio ya kinyama yanayofanywa sasa yakiwalenga viongozi wa dini na watu wengine katika jamii, yanalenga kushinikiza visiwa hivyo kuachiwa huru.
Padre Mushi alisema jamii kubwa ya watu wa Zanzibar ni waumini wa dini ya Kiislamu, hivyo lipo kundi dogo la watu ambalo limeamua kushinikiza sauti za Wazanzibari zisikilizwe kwa kutumia njia hizo chafu, kulazimisha mamlaka kuchukua hatua na pia kuwatisha wasio waumini wa dini hiyo kuamini kuwa Zanzibar siyo sehemu salama ya kuishi kwa mtu ambaye siyo Muislamu.
Kauli hiyo ya Padre Mushi inafuatiwa na ile iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakristu Tanzania (CCT), Askofu Peter Kitula, katika mahojiano yake kupitia simu yake ya kiganjani akimtaka Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua za haraka za kuufumua uongozi wa Jeshi la Polisi, kwa kuwaondoa watendaji wake wa sasa na kuweka wapya wenye uwezo wa kulinda uhai wa Watanzania.
Askofu Kitula ambaye alikuwa akieleza msimamo wa jumuiya anayoiongoza kuhusu kushamiri kwa vitendo vya uvunjifu wa amani nchini, alisema Serikali imeruhusu wageni kuingia nchini kiholela na kusababisha Watanzania kuiga mwenendo wa maisha yao hususan wanaotoka katika nchi zenye machafuko.
"Watu wengine kweli ni magaidi, wanakuja kwa maslahi yao, wanawatumia Watanzania kutenda mambo ya kihalifu. Kwa hali hii Serikali inatakiwa kuwachukulia hatua haraka watuhumiwa wa matukio haya.
"Kitendo cha kuendelea kukaa kimya, hakileti picha nzuri kwa jamii, Serikali inaonyesha imeshindwa kuwakamata, inajipaka matope ya damu ya wananchi wake," alisema.
Kiongozi mwingine wa dini aliyezungumzia mwenendo huo wa mambo, ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, ambaye aliionya Serikali kuhusu tume inazounda kuchunguza matukio ya kigaidi dhidi ya raia.
Shekh Salum alisema tume zote za uchunguzi zinazoundwa kuchunguza matukio ya kihalifu yenye sura ya kigaidi, hazitoi majibu ya uchunguzi huku zikiwa zimetumia gharama kubwa ambayo ni kodi ya wananchi.
"Wananchi wanapata wasiwasi kwamba, kwanini tume hizi hazileti mrejesho, Serikali inatakiwa kuhakikisha mambo haya yanawekwa sawa ili kuondoa mawazo mabaya kuwa labda matukio haya yanatokana na mgongano wa kiimani," alisema.
Kauli ya Sheikh Salum kuhusu wasiwasi wa utendaji wa tume zinazoundwa na Serikali kuchunguza matukio mbalimbali ya kigaidi dhidi ya raia ambayo pia imezungumzwa na watu mbalimbali waliohojiwa na MTANZANIA Jumatano, inaibua upya kumbukumbu ya tume kadhaa zilizopata kuundwa kuchunguza vitendo vya uhalifu dhidi ya raia ambazo hadi sasa hazijatoa majibu ya uchunguzi wake.
Miongoni mwa tume hizo ni ile iliyoundwa kuchunguza tukio la kuvamiwa, kujeruhiwa na kupigwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania na Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, mwezi Machi mwaka huu.
Kibanda alitendewa vitendo vyenye sura ya kigaidi, huku wakati akiwa na mgogoro na Serikali kutokana na mitizamo na misimamo yake ya kazi ya uandishi wa habari.
Siku chache baada ya kuteswa, iliundwa tume iliyokuwa na makachero wenye ujuzi na uzoefu wa kazi ya kikachero kuchunguza tukio hilo, lakini hadi sasa ikiwa ni zaidi ya miezi sita tangu alipopatwa na mkasa huo, taarifa ya tume iliyoundwa haijawahi kutoka na kumekuwa na tetesi nyingi kuwa huenda shambulio hilo lilitekelezwa na wanataaluma ya utesaji ambao aghalabu wanapatikana katika vyombo vya dola.
Tume nyingine ambayo inachukua mwelekeo unaofanana na iliyoundwa katika sakata la Kibanda, ni ile iliyopewa jukumu la kuchunguza sakata ka kutekwa na kuteswa kinyama kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
Dk. Ulimboka aliteswa kinyama na kabla ya kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande ulio nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ambako aliokotwa baadaye na wasamaria wema waliomfikisha Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu.
Saa chache baada ya kuokotwa, alieleza kuwatambua waliomteka na kumtesa na alimtaja mmoja wa wanausalama kuhusika na tukio lake, lakini tume iliyoundwa kuchunguza ukweli wa tukio lake ambayo pia ilikuwa na makachero wenye ujuzi na uzoefu wa kazi ya ukachero, hadi sasa ikiwa ni takribani zaidi ya mwaka mmoja, haijawahi kutoa majibu wala tamko lolote la uchunguzi wake.
Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo Bisimba, ambaye alihusika kwa karibu kumsaidia Dk. Ulimboka, baada ya kuteswa, kiuhalisi matukio yote ya kigaidi yanayotokea sasa nchini yanaonekana kuwa na mkono wa Serikali na ndio maana hakuna hatua stahiki inazochukua kukabiliana nayo.
Bisimba alisema yapo baadhi ya matukio ambayo yaliigusa Serikali moja kwa moja na kuchukuliwa hatua za haraka kwa watuhumiwa kukamatwa, lakini mengine imekuwa ikizungusha.
"Matukio yasiyoigusa Serikali hawahangaiki nayo wanabaki kutubabaisha tu, kwa mfano lile la mauaji ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, pamoja na lile la askari mmoja wa usalama barabarani aliyegongwa, tuliona mara moja watuhumiwa walikamatwa ndani ya muda mfupi na kuchukuliwa hatua," alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali inatakiwa kuweka pembeni unafiki na kutekeleza wajibu wake ili kujinasua na harufu ya damu ya watu wake inayotoa sasa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama, ambaye pia alizungumza kuhusu mwenendo wa sasa wa usalama wa raia, yeye alilitaka Jeshi la Polisi likatae kuwekwa mfukoni na CCM pamoja na wanasiasa na badala yake lifanye kazi yake kwa kuzingatia taratibu na maadili ya kazi zake.
Alisema asilimia kubwa ya matukio ya kigaidi yanayoendelea kutokea yanaigusa Serikali na Jeshi la Polisi.
"Kila tukio utasikia ni ugaidi, udini, Muungano, haya ni mambo ambayo chanzo chake ni siasa, tuache siasa tufanye kazi, tukiendelea hivi tutafikia pabaya," alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba, alilitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuwakamata wahusika wanaomwagia raia tindikali.
Lipumba alisema kuwa uwepo wa matukio ya kigaidi nchini ni matokeo ya kuwa na Jeshi la Polisi lililotawaliwa na tatizo la ukosefu wa weledi na intelijensia ya uhakika, ambayo ingeweza kuyamaliza matatizo yote ya kinyama yanayotokea sasa.
Alisema Zanzibar ni nchi ndogo, ambayo haiwezi kulifanya Jeshi la Polisi kushindwa kuwakamata wahusika wanaomwagia watu tindikali, lakini kwa sababu jeshi hilo limetawaliwa na siasa, limekuwa likiishia kutoa matamko yasiyo na tija kwa Taifa.
Mwanasiasa mwingine aliyezungumza na kutoa maoni yake kuhusu usalama wa raia nchini iwapo unaridhisha, ni aliyewahi kuwa mgombea urais wa Chama cha NCCR-Mageuzi, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe ambaye alisema Serikali haiwezi kukwepa lawama za matukio ya kigaidi, kwa sababu kwa kiasi kikubwa wasaidizi wa rais wameshindwa kumsaidia kupambana nayo.
"Rais Kikwete amejitahidi kutaka kutekeleza mikakati yake, lakini baadhi ya viongozi aliowateua wamekuwa hawana msaada kwake na ndio wao wanakuwa chanzo cha vurugu hizi, kutokana na kushindwa kwao kuwa na mikakati imara ya kupunguza tatizo la ajira.
"Ugumu wa maisha unachangia kuibuka kwa matukio ya kikatili kama haya, ni jambo rahisi kumnunua mtu fukara kwa vijisenti kidogo ili afanye unyama, lakini haiwezekani kufanya hivyo kwa mtu mwenye shughuli ya kumuingizia kipato.
Alipoulizwa Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, kuhusu mtizamo huo ilionao jamii kwa sasa kuhusu taswira ya Serikali katika kushughulikia vitendo vya kigaidi, alijibu kwa ufupi kuwa hawezi kutoa jibu la jambo hilo na baadaye aliliomba gazeti hili kutafuta muda wa kufanya naye mahojiano ofisini kwake.
"Nakuomba uje ofisini, hili suala ni pana sana, njoo tufanye mazungumzo ya kina, naomba uje ofisini tulizungumze kwa kina," alisema Senzo.
SOURCE: Mtanzania
EmoticonEmoticon