SAKATA LA WAHAMIAJI HARAMU: SITTA AWATETEA




Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta, akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) Dar es Salaam jana kuhusu kutengwa kwa Tanzania katika nchi za Afrika Mashariki pamoja na ‘Operesheni Kimbunga’ inayoendelea hapa nchini. Kulia ni Katibu mkuu wa wizara hiyo Joyce Mapunjo.

·         APINGA VIKALI UTARATIBU UNAOTUMIKA KUWAONDOA·         ASEMA UNAKIUKA HAKI ZA BINADAMU, UTAWALA BORA·         AHOJI KWA MIAKA YOTE SERIKALI ILIKUWA WAPI WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amekosoa utaratibu unaotumika kuwaondoa wahamiaji haramu nchini kupitia Operesheni Kimbunga, akisema ni kinyume cha haki za binadamu.Waziri Sitta amekuwa kiongozi wa kwanza nchini kukosoa utaratibu unaotumika kuondoa wahamiaji hao tangu Rais Jakaya Kikwete, aagize wawe wameondoka nchini ndani ya siku 14, vinginevyo wataondolewa kwa nguvu. Rais Kikwete alitoa agizo hilo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kagera.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Sitta aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya, jeshi la polisi na uhamiaji kuwapa muda wa kutosha wahamiaji hao ili waweze kujiandaa kuondoka na mali zao ambazo walichuma kwa muda mrefu walioishi nchini kuliko kuwaswagaswaga. "Haifai kwa hawa ndugu zetu ambao tumeishi nao kwa muda mrefu leo hii wanaswagwaswagwa jambo ambalo ni kinyume cha haki za binadamu pamoja na utawala bora," alisema na kuongeza;"Je, Watanzania waliopo nje ya nchi wakiondolewa kwa nguvu kama hawa wenzetu wanavyofanyiwa tutafurahi?" Alisema kwa jambo hili Tanzania isionekane ina nongwa na nchi fulani kwani hata Rais Kikwete, wakati anatoa agizo hilo hakusema utaratibu huo utumike. Alitoa mfano kuwa kuna mwanamke ambaye amefukuzwa nchini ambaye ni raia wa Rwanda akisema aliishi kwa zaidi ya miaka 30 nchini Tanzania na mtoto wake amesomea nchini na kuajiriwa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)."Mtu kama huyu hakutendewa haki...mtu unamfukuza anaondoka na begi lake moja wakati ana mali zake nyingi...huyo ni lazima arudishwe ili ahakiki mali zake," alisema. Alisema walioondolewa na kuacha mali zao nyingi pamoja na watoto watarudishwa nchini kufanyiwa uhakiki kama inavyofanyika kwa raia wa Malawi. Alishauri wahamiaji hao watakaorudi kufuata mali zao wapewe makazi ya muda na mali zao zisiporwe kwani watu hao hawakuwa majambazi. "Kama umemuacha mtu ameishi nchini kwako kwa muda wa miaka 30 halafu leo unamfukuza kwa kumswagaswaga nani mwenye kosa? Na muda wote ulikuwa wapi?" Alihoji Sitta na kusisitiza kuwa; "Ndiyo maana tunasema aondolewe kwa utaratibu."Aliongeza kuwa miongoni mwa wahamiaji haramu waliofukuzwa baadhi yao waliwahi kuwa viongozi wa Serikali za vijiji na mitaa katika maeneo waliyokutwa wakiishi. Waziri Sitta alisema tayari amepokea barua kutoka nchi za Burundi na Rwanda zikilalamikia utaratibu unaotumika kuwaondoa wahamiaji haramu hao."Oktoba 1 mimi na Waziri wa Mambo ya Ndani tutakuwa mpakani mwa Burundi na Rwanda ili kuangalia jinsi operesheni hiyo inavyotekelezwa na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hizo ili Tanzania isionekane ina malengo mabaya," alisema Sitta. Alisema endapo utaratibu unaotumika wa kuwaondoa ukiendelea maadui wa Tanzania wataona njia hiyo inalenga kuwakomoa, jambo ambalo si la kweli.

Previous
Next Post »