Katika
maisha ya kila siku ya binadamu suala la ulinzi na usalama wa mali na maisha ni
muhimu sana. Binadamu huishi kwa kutegemeana basi ndivyo ilivyo hata katika
suala la ulinzi wa mali na maisha yetu. Unaweza kujiuliza je,ni nani mwenye
jukumu la ulinzi?je,ni mimi au wewe? Au ni sisi sote?
Basi katika
miaka ya hivi karibuni Jeshi la Polisi Nchini limeendeleza dhana ya ulinzi
shirikishi na ulinzi jirani kwa lengo la kushirikisha jamii kwa karibu zaidi
katika suala zima la ulinzi na usalama. Zana hii imekuwa ikitoa fursa kwa jamii
na wadau mbalimbali kutoa taarifa za kuzuia uharifu hali inayofanikisha
kudhibiti vitendo hivyo.
Ni wazi
kabisa kuwa kila mmoja wetu ana jukumu la kushiriki katika ulinzi.Ushirikishwaji
huu wa wananchi katika kuzuia na kudhibiti vitendo vya uharifu ni mpana zaidi,
kwani vitendo vya uvunjifu wa amani na utovu wa nidhamu si vya kuvumilika
katika jamii. Kila mmoja wetu anapaswa kujua nini cha kufanya pale anapoona
vitendo ambavyo si vya kiungwana vikitendeka.
Katika siku
za hivi karibuni hususani katika mechi
za ligi kuu Tanzania bara kumekuwa kukitokea vitendo ambavyo si vya kiungwana
wala kinidhamu katika mchezo wa mpira wa miguu. Vurugu mbalimbali kutoka
mashabiki wa timu zinazoshiriki ligi kuu zimevuka mipaka kwani imefikia hatua
hata ya kurushiana mawe.Katika mechi ya hivi karibuni kati ya Mbeya City dhidi
ya Yanga mechi iliyofanyika uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine kulitokea vitendo
visivyo vya kiungwana katika medani ya michezo.
Ikumbukwe
kuwa suala la ulinzi katika sehemu mbalimbali ni jukumu letu sote. Kila mmoja
wetu awe mlinzi wa mwenzake katika kuhakikisha amani na utulivu vinachukua
nafasi yake katika michezo ili kwa ujumla wananchi wapate burudani.
Vurugu na
vitendo visivyo vya kimichezo vina athari kubwa si tu kwa timu bali hata kwa
mashabiki na wananchi wa mkoa husika kwani inapotokea timu kufungiwa kutofanya
michezo yake katika uwanja wa nyumbani ni athari hata katika shughuli za
kiuchumi pamoja na kuua mapato ya mlangoni. Pia vurugu kama hizi ni athari pia
katika shughuli za uwekezaji na kuzuia upatikanaji wa fursa ya ajira kwa
wananchi.
Yapo
mapendekezo mbalimbali ya wananchi juu ya suala hili la kudhibiti vurugu katika
michezo. Itambulike kuwa ni suala la kila mwananchi kwani kama kila mmoja wetu
ataona umuhimu wa kutoa taarifa pale anapotilia mashaka mtu/watu kwa vyombo vya
ulinzi na usalama, basi suala hili tunao uwezo wa kulidhibiti na kulimaliza
kabisa.Kila mwananchi atoe ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kufanikisha
kudhibiti na kutokomeza vitendo vya vurugu uwanjani na katika michezo kwa
ujumla.
Pengine kwa
sasa ni muda muafaka kwa uongozi wa timu pamoja na shirikisho la soka nchini ni
kuliangalia suala hili kwa kina zaidi ili kujiepusha na madhara makubwa zaidi. Kuwepo
na adhabu kali zaidi kwa timu itakayo shindwa kuwadhibiti mashabiki wake dhidi
ya vitendo visivyo vya kimichezo.
Ni imani
yangu kuwa kila mwanamichezo na wadau wote wa michezo watashiriki kikamilifu
kuzuia na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pale waonapo dalili za vurugu
kutoka kwa mtu au kikundi cha watu
kikipanga njama za uvunjifu wa amani katika michezo hasa mechi za ligi kuu
zinazoendelea.
Kamanda wa
Polisi mkoa wa Mbeya Kamishina msaidizi, DIWANI ATHUMANI anawakumbusha
mashabiki na wadau wote wa michezo kuwa “michezo ni uchumi, michezo ni
burudani, michezo ni upendo/amani na kila mmoja wetu aone kuwa ana kila sababu
ya kutekeleza hili”
Imetolewa
na:
[DIWANI
ATHUMANI – ACP]
KAMANDA WA
POLISI MKOA WA MBEYA.
EmoticonEmoticon