WAZIRI
Mkuu Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, amewataka
Watanzania kutambua kwamba hakuna mtu tajiri anayetoa fedha na mali zake
bila masharti; na kuwa iwapo Watanzania watawaweka madarakani viongozi
kwa rushwa, wasitegemee Katiba Mpya itajibu matatizo yao ndani ya jamii.
"Tukumbuke
kuwa anayekuhonga ili umpigie kura akishaingia madarakani mkataba wake
na wewe uliishia pale ulipomuuzia kura yako na yeye kazi atakayofanya
akipata hiyo ofisi au madaraka ni kusaka rushwa na kufisadi mali za umma
ili arudishe fedha zake alizotumia kukununua wewe na wenzako," alisema
Sumaye.
Sumaye
alitoa kauli hiyo mjini Morogoro jana wakati akifungua maadhimisho ya 20
ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA).
Alisisitiza
kuwa; "Kama huamini wewe nenda ukamwombe fedha iwapo hana kura
anayokuomba halafu usikie jibu atakalokupa."Alisisitiza kuwa kiongozi wa
aina hiyo ataongeza nyingine (fedha) nyingi zaidi za kukununua tena
safari ijayo. "Mtu wa aina hiyo kipaumbele chake si jamii na umma, bali
ubinafsi wake na wale marafiki zake waliomfadhili wakampa zile
fedha,"alisema Sumaye.
Sumaye
alisema hata katiba iwe nzuri namna gani na ikatamka kuwa rushwa ni adui
wa haki na hata ikatoa adhabu kali sana kwa kosa hilo, kama tutaweka
viongozi madarakani kwa rushwa, hiyo katiba wala haitasaidia.Kiongozi
huyo mstaafu alisema ni lazima katiba nzuri mpya iambatane na serikali
safi yenye kusimamia masilahi ya umma.
"Huwezi
kumweka madarakani mwenyekiti wa kijiji au diwani au mbunge au hata rais
kwa rushwa ya kuwanunua wapigakura halafu utegemee katiba mpya itajibu
matatizo ya jamii," alisisitiza Sumaye.Alisema yeye ukimuuliza kuhusu
katiba tuliyonayo sasa atasema ni ni nzuri tu na tungeweza kufanya
marekebisho katika maeneo machache kama pana haja ya kufanya hivyo.
"Tatizo
letu liko katika kutekeleza na kusimamia sheria zetu tulizozitunga
kutokana na maelekezo ya jumla ya katiba yetu. Baada ya katiba Bunge
hutunga sheria mbali mbali kukidhi matakwa fulani fulani katika jamii,"
alisema na kuongeza;
"Kwa hiyo
pamoja na kutengeneza katiba mpya, jambo muhimu sana ni kuwa na
serikali itakayosimamia na kutekeleza sheria zetu ili kulinda yale
yaliyoelekezwa katika katiba."
Alisema
kuwa katiba itatamka haki ya mtu kuwa na mali na itatamka wajibu wa
serikali kulinda mali ya mtu. Alisema katiba haiwezi kumzuia mwizi
kwenda kuiba na sheria haitamzuia mwizi kwenda kuiba ila itatamka adhabu
ya kupewa huyo mwizi.
Alisema
kuwa ili vyote hivyo viwe na maana ni lazima awepo mtu au chombo cha
kumkamata mwizi na kumfikisha katika mikono ya sheria na chombo hicho ni
serikali.Alisema kama serikali haiwezi kufanya hiyo kazi kwa ukamilifu,
tutaishia kulalamika tu maonevu na maumivu yataendelea kuumiza jamii. Alisema
Katiba Mpya bila kuwa na watu madhubuti, watu waadilifu, wanaochukia
rushwa na ufisadi kwa dhati kuongoza nchi yetu haitakuwa na msaada
wowote katika kuboresha maisha ya Watanzania."Nataka nieleweke vizuri
kuwa mimi sizungumzii serikali yangu iliyoko madarakani, bali
nazungumzia Katiba Mpya na serikali itakayozaliwa baada ya hapo, alisema
Sumaye na kuongeza; "Nazungumzia
uchaguzi ulioko mbele yetu mwakani na mwaka 2015, simzunguzii mtu
yeyote bali naizungumzia tabia mbaya. Najua hata hapa wapo watu
wametumwa nendeni mkamsikilize huyo Sumaye leo (jana) atasema
nini.Hakuna haja ya kutafiti nitakachosema maana kinaeleweka. Nimesema
mimi sitanyamaza kupambana na rushwa na ufisadi na maovu mengine hata
siku moja. Wala sitaacha kukemea tabia hizi mbaya zinazoangamiza jamii
yetu na taifa letu."
Sumaye
alisisitiza; "Kama wewe ni mhusika una tabia zinazofanana na hizo dawa
ni kuziacha au uvumilie tu haya maneno yaendelee kukuchoma
moyoni."Aliwataka Watanzania wote kupitia wakati huu wa kutengeneza
Katiba Mpya waanze kutengeneza v i c hwa n i mwa o s e r i k a l i
itakayosimamia utekelezaji wa katiba hiyo kwa masilahi ya umma, yenye
uwezo na yenye uadilifu usiotiliwa shaka.
Alisema,
kazi ya kukemea uovu na hasa uovu wa rushwa za uchaguzi lazima ifanywe
na kila Mtanzania mwadilifu ili waovu hao wasipate uongozi wa kununua
maana wataifanya kazi ya kutunga Katiba Mpya ambayo ni kazi ya gharama
kubwa iwe imepotea bure.
Dawa za kulevya
Akizungumzia
dawa za kulevya, Sumaye alisema tatizo hilo kwa sasa ni kubwa ndani na
nje ya nchi na vijana wengi wameathirika.Alisema biashara hiyo ni haramu
inayohusisha fedha nyingi na mitandao mipana. Alibainisha kwamba katika
baadhi ya nchi duniani, biashara hiyo hukithiri mpaka wahusika huweza
kujenga majeshi ya kupambana na majeshi ya serikali ana kwa ana.
"Nchini
mwetu hatujafikia hatua hiyo, lakini ikiachiwa ikaendelea yaweza kufika
huko. Biashara hii huharibu sana vijana wetu na kugeuka zezeta au wakawa
wahalifu wa kutisha," alisema Sumaye na kuongeza; "Kama mtu anaweza
kuhonga sehemu kubwa ya wapigakura katika jimbo la uchaguzi au hata
katika nchi kama nafasi anayosaka ni urais, tumeshajiuliza hizo fedha
nyingi hivyo anapata wapi?
Kama
anajihusisha na biashara hizo chafu akipata nafasi hiyo watoto wetu
watapona? Haya ni maswali muhimu ya kujiuliza tunapoelekea mwaka kesho
kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na mwaka 2015 wakati wa uchaguzi
mkuu.
EmoticonEmoticon