Mabomba ya kusafirisha gesi yatua Mtwara

Mabomba maalu kwa ajili ya kusafirisha gesi  

 Mtwara. Meli kubwa kutoka China tayari imetua katika Bandari ya Mtwara kwa ajili ya kushusha mizigo ya mabomba ya gesi ili kuanza kwa kazi ya ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Mmoja wa watumishi ndani ya Bandari ya Mtwara ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema zaidi ya magari 20 yanatakiwa kupakua mzigo wa mabomba zaidi ya 4,000 kutoka bandarini hapo na kusafirishwa kwenda Kiranjeranje Lindi kwa ajili ya zoezi zima la ujenzi wa bomba hilo.
“Hayo magari mliyoyaona ni miongoni mwa zaidi ya magari 20 yanayokuja kupakua mzigo wa mabomba ambayo ni zaidiya 4,000 kwa ajili ya kuyapeleka maeneo mbalimbali ikiwemo Kiranjeranje Lindi kwa ajili ya kufanikisha zoezi la ujenzi wa njia ya kusafirisha gesi, upakiaji unaendelea hapa Mtwara na Dar meli inapakuwa mzigo ili kupelekwa kwenye maeneo husika na upakuaji kwa mikoa yote unaendelea kwa amani,” alisema.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa madereva wa magari maalumu kwa ajili ya kupakua mzigo wa mabomba,alisema wametokea Dar es Salaam na hii ni zabuni maalumu waliyoipata kwa ajili ya maandalizi ya kupokea mizigo na kupeleka yanakotakiwa hapo baadaye baadaye baada ya kukabidhiwa kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
“Hivi sasa tunaenda kupakiza mzigo kwa ajili ya maandalizi tukisubiri siku ambayo wahusika wakuu watakaokabidhiwa,ili na sisi tuanze zabuni yetu ya usafirishaji kuyapeleka yanakohitajika, “ alisema
Akizungumzia tukio hilo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo Muhongo alisema tayari meli ilitua katika bandari ya Dar es Salaam na meli kubwa imetua Mtwara kwa ajili ya kushusha mzigo wa mabomba na watakapomaliza yatakabidhiwa na kupokewa kwa heshima kama alivyofanya waziri mkuu jijini Dar es Salaam juzi (Jumapili)
“ Kwa mtu anayejua uchumi kitu kitakachotutolea umaskini ni hii gesi, mimi ninashangaa watu wa Mtwara wahoji kwa nini mizigo mingine ishushwe Dare es Salaam badala ya Bandari yaMtwara, hata kwa barabara wengine wanaanzia Dar na wengine wanaanzia Mtwara halafu wanakutana, hivyo sioni sababu ya kusafirisha kwa magari baada ya kushusha mizigo yote Mtwara ni kwa nini tuharibu barabara ?” alihoji Profesa Muhongo.
Sudi Mohammedi alisema kitendo cha serikali kwenda kushusha mizigo mingine katika Bandari ya Dar es Salaam ni kuonyesha ni kwa kiasi gani viongozi wasivyoithamini Mtwara kwa kuiacha bandari hiiyo.
Kabla ya kupita kwa magari hayo ya kubeba mizigo maeneo ya Bima, vilianza vifaru vikifuatiwa na gari kubwa lililobeba wanajeshi lililokuwa likizunguka katika baadhi ya maeneo mbalimbali mkoani hapa.
Previous
Next Post »