KODI YA SIMU KURUDI BUNGENI AGOSTI MWAKA HUU KWA AJILI YA KUJADILIWA UPYA


SAKATA la kodi ya simu ya Sh 1,000 kwa kila laini ya simu kwa mwezi, inayolipwa na watumiaji wa simu, litamalizwa bungeni kisheria. 


Waziri wa Fedha, William Mgimwa, amesema wameanza kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete, la kuitaka Wizara ya Fedha kukutana na wadau wengine, kuangalia namna ya kupata vyanzo vingine vya mapato mbadala wa kodi hiyo.


Alisema hayo alipozungumza jana na Habari leo, baada ya kusaini mkataba wa msaada wa zaidi ya Sh bilioni 344, kutoka Benki ya Dunia, ili isaidie masuala mbalimbali katika sekta ya usafirishaji. 
 
Mgimwa alisema katika suala hilo, masuala ya kisheria yatafikishwa bungeni mwezi ujao, ili kumaliza utata wa kodi hiyo.



Alisema uamuzi wa kushughulikia suala hilo, ulifikiwa kutokana na agizo la Rais Kikwete la hivi karibuni, kutaka wizara hiyo na ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kukaa na kampuni za simu kumaliza utata uliojitokeza kuhusu kodi hiyo.



Awali Umoja wa Wamiliki wa Kampuni za Simu (MOAT), ulitoa maoni kutaka kufutwa kwa kodi hiyo, kutokana na kulalamikiwa na wadau wa sekta ya mawasiliano.



Mbali na Moat, pia baadhi ya viongozi wa Serikali, wabunge na wananchi, walipinga kodi hiyo kwa walichokieleza kuwa itaongeza mzigo wa ugumu wa maisha kwa mtumiaji, hususan wa kipato cha chini.


Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, alipozungumza na gazeti hili jana, alisema mara baada ya Rais kutoa agizo, wizara husika zilikutana kufanyia kazi agizo hilo.


"Rais akishaagiza kinachofuata ni utekelezaji na sisi kesho yake tulianza vikao na ninachoweza kukwambia tuko pazuri na tukikamilisha majadiliano yetu, tutatoa taarifa," alisema Makamba.



Alisema lengo ni kuangalia kama Serikali inaweza kupata Sh bilioni 178 kutoka vyanzo vingine, iwapo itaamua kufuta kodi inayotokana na tozo ya Sh 1,000 kutoka kwenye laini za simu.



Hivi karibuni, Rais Kikwete aliagiza Wizara za Serikali zinahusika na kodi na mawasiliano na kampuni za simu za mikononi nchini, kukutana kutafuta jinsi ya kumaliza mvutano wa kodi hiyo.



Alitoa maelekezo hayo baada ya kukutana na viongozi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na wawakilishi wa kampuni za simu za TTCL, Airtel, Vodacom, Tigo na Zantel. 


Rais alisema lengo kuu la mkutano huo, liwe kupendekeza jinsi ya kuziba pengo la Sh bilioni 178 ambazo zitapotea katika bajeti, iwapo kodi hiyo itafutwa na Serikali kupitia marekebisho kwenye Muswada wa Fedha wa Bajeti ya Mwaka 2013/14.



Aliwaambia wawakilishi wa pande hizo mbili kuwa hawezi kuifuta moja kwa moja kodi hiyo, bila kutafuta njia nyingine za kupata fedha za kujaza pengo litakalotokeza, huku tayari Bunge limezipangia matumizi.



“Nakuombeni kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili yenu pamoja tutafute namna gani tutajaza pengo hili la Sh bilioni 178, endapo tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha wananchi mzigo mzito na kuwa pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu,” alisema Rais Kikwete.
Source:Habari Leo
Previous
Next Post »