MAKOSA ATANGAZA KUJINYONGA KWA KIINGILIO, ALIKUWA MFANYABIASHARA MAARUFU SANA MJINI IRINGA


















Katika mazingira ya kutatanisha Makosa ametangaza kujinyonga katika tukio atakalolifanya hadharani.  Kwanini anataka kulifanya tukio hili hadharani? Hili ni swali ambalo kila mtu anaweza kujiuliza lakini jibu lake anataka iwe hivyo kwa kuwa atajinyonga katika tukio ambalo mashuhuda watalazimika kulipa kiingilio.  Kwanini anataka kufanya tukio hilo kwa kiingilio? Kila mtu anaweza kujiuliza swali hili. Katika majibu yake kupitia mtandao huu, MAKOSA anasema amefikia uamuzi huo ili zikusanywe fedha zikazosaidia kuendesha familia yake, watoto yatima na sehemu kuchonga madawati kwa shule zenye upungufu wa madawati mjini Iringa. Alipoulizwa kama ana ufahamu wa sheria na kwamba kujaribu au kufanya hivyo ni kosa la jinai, katika majibu yake anasema litakuwa kosa la jinai mpaka pale atakapofanya hivyo na kwa kuwa atakufa hana cha kuhofia. Lakini MAKOSA ni nani? Kwa wakazi wa mjini Iringa MAKOSA ni mtu maarufu sana, alifahamika zaidi kwa biashara zake nyingi alizoanza kuzifanya mwanzoni mwa miaka ya tisini baada ya kuacha shughuli yake ya ubaharia. Wakati akifika mjini Iringa, MAKOSA akiwa na itikadi za rasta, alikuwa hanywi pombe, mnyenyekevu na alijikita katika kuisaidia jamii ya watu wa Iringa kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti. Miti ya aina mbalimbali inayonekana mjini Iringa, sehemu yake kubwa ilipandwa na MAKOSA. Hata hivyo pamoja na kuupendezesha mji kwa miti hiyo, historia ya MAKOSA katika uhifadhi wa mazingira ni kama vile imesahaulika kwasababu hakuna anayemuenzi kwa kazi kubwa aliyoifanya. Pamoja na harakati hizo MAKOSA ndio mtu wa kwanza mjini Iringa kuingiza magari aina ya Coaster zilizokuwa zikifanya kazi ya kusafirisha abiria katika maeneo mbalimbali ya mjini Iringa. Pamoja na biashara ya usafirishaji, MAKOSA alikuwa anaendesha biashara ya hoteli. Kabla ya kuanza kuendeshwa na MAKOSA, hoteli hiyo ilikuwa ikijulikana Cats Hotel (ipo jirani na Maktaba ya Mkoa wa Iringa) na akaibadilisha jina na kuiita MAKOSA CATS Hotel.  Katika hoteli hiyo bendi nyingi zimepiga muziki na kwa mara ya mwisho, mwanamuziki Macay Fanta alikuwa akifanya shoo zake mpaka pale MAKOSA aliposhindwa kuiendesha mwanzoni mwa miaka ya 2000. Lakini mtandao wa biashara za makosa haukuishia hapo, alikuwa pia akimiliki hospitali maarufu sana iliyopo jirani kabisa na soko kuu la mjini Iringa, hii nayo iliitwa MAKOSA hospital. Taarifa kutoka kwake mwenyewe biashara zote hizo haziko tena mikononi mwake na ugumu wa maisha unazidi kumuandama. Japokuwa hajasema hivyo, huenda kuteteleka kwa hayo yote ndio sababu ya MAKOSA kutaka kujiua.  Tafsiri ya jina la MAKOSA imeendelea kuwa siri yake na amekataa kutoa maana ya kuacha majina yake halisi ya Ramadhani Mrisho na kujiita MAKOSA.
Previous
Next Post »