Mama wa marehemu Kanumba Flora Mtegoa amesema anampenda msanii Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu, licha ya matatizo yote yaliyotokea na kwamba anamwachia Mungu katika yote.
Akizungumza na Mwananchi katika makaburi ya Kinondoni mara baada ya misa maalum ya kumuombea marehemu na kuweka mashada ya maua Mtegoa alisema yeye ni mkristo hivyo hana kinyongo na mwigizaji huyo.
"Mimi ni mkristo tumeambiwa samehe mara saba sabini, binafsi sina kinyongo chochote na ninampenda kama ilivyokuwa kwa mwanangu, ila kila ninapomuona siachi kumkumbuka mwanangu," alisema Mtegoa.
Alisema Kanumba alikuwa ni kama mtoto, mume, kaka na kama rafiki yake, alimfanya kuwa mtu wa karibu yake na anashukuru mwanaye pia alimfanya ajisikie furaha muda wote.
"Mara ya mwisho kuongea naye ilikuwa ni Aprili 6 usiku, siku moja kabla ya kifo chake, tulizungumza mengi kwa njia ya simu aliniahidi mengi na kunieleza kuhusu safari yake ya Marekani, nammisi kwa kweli," alisema.
Akizungumzia suala ya ushiriki wake katika filamu ya Without Daddy Mtegoa alisema "Nilikuwa naigiza tangu nasoma sekondari lakini sanaa hapo nyuma haikulipa hivyo sikuendelea na sanaa, baada ya kufariki Kanumba niliombwa nicheze filamu ya Without Daddy, nilikubali na ikawa filamu yangu ya kwanza," alisema.
Alisema kwa sasa yeye anafanya kazi chini ya Kampuni ya Kanumba The Great, hivyo itakapotokea filamu nyingine yupo tayari kuicheza.
EmoticonEmoticon