‘Maninja’ wamkata albino mkono


Mkuu wa Majeshi ya Polisi Tanzania,IGP Said Mwema.

MTOTO wa mwenye ulemavu wa ngozi, Mwigulu Magessa (7) ameshambuliwa na vijana watatu wanaodaiwa kuvaa nguzo vilizoficha nguso zao na kumkata mkono wake wa kushoto.
Akizungumza kwa simu juzi, Diwani wa Kata ya Milepa, Apolinari Macheta alisema tukio hilo lilitokea saa 11:00 wakati Magesa anayesoma darasa la kwanza Shule ya Msingi Msia, Kata ya Milepa, Bonde la Ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga akirejea nyumbani.
Macheta alisema Magesa alikuwa ameongozana na kundi la wanafunzi wenzake.
Alisema mtoto huyo amelazwa Zahanati ya Mtowisa, Bonde la Ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga kwa matibabu na kwamba, hali yake inaelezwa siyo nzuri kwani alifikishwa akiwa amepoteza fahamu.
Akisimulia kisa hicho, Macheta alisema Kijiji cha Msia kimegawanyika sehemu mbili; Msia Center na Msia mashambani.
Alisema Magesa akiwa ameongozana na kundi la wanafunzi wenzake wakirejea nyumbani Msia Mashambani, ghafla vijana watatu wanaodaiwa kuvaa kininja waliwashtua, huku mmoja wao anadaiwa kumkimbiza albino huyo na wengine kuwafukuza wanafunzi wengine.
“Licha ya wanafunzi hao kupiga kelele zao haziweza kusikika kijijini, kwani walikuwa mbali na makazi ya watu... yule kijana mmoja aliyekuwa akimfukuza albino akiwa na panga aliukata mkono wake na kutokomea nao kusikojulikana,” alisema.
Alisema watoto walipofika kwa wazazi, waliwasimulia na kuanza msako mkali kumtafuta Magesa baadaye walimkuta akiwa mashambani huku mkono wake mmoja ukiwa umenyofolewa.
Jitihada za kumpata Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Peter Ngusa hazikufanikiwa baada ya simu zake za mkononi kuita bila kupokelewa. Wimbi la mauaji ya albino yalikuwa yamepungua kufuatia serikali kuamua kupambana nayo.
Hata hivyo, kwa wiki mbili zilizopita mkoani Rukwa yametokea matukio mawili ya kukatwa mikono kwa walemavu wa ngozi, hali inayoashiria mauaji hayo kurejea kwa kasi.
Watu wanaojishughulisha na mauaji hayo wanadaiwa kutumwa na waganga wa kienyeji kwa ajili ya biashara zao au kuwasaidia wachimbaji madini kupata madini mengi, dhana ambayo ni potofu inayotakiwa kupigwa vita na kila mwananchi.
Previous
Next Post »