Mabaraza ya Katiba kuanza Juni mwaka huu


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba

MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema kazi inayofuata kwa tume hiyo ni kuunda mabaraza ya Katiba katika kila wilaya nchini, ambayo yatakuwa na wajumbe kuanzia ngazi ya Kata na watachaguliwa na wananchi wa maeneo husika.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alisema mikutano ya mabaraza hayo itaanza mwezi Juni hadi Agosti mwaka huu, huku akisisitiza kuwa katika mikutano hiyo, wajumbe hao watatakiwa kuwasilisha maoni ya wananchi tu.
“Hivi sasa Tume inakamilisha utaratibu wa namna bora ya kidemokrasia ya kuwapata wajumbe wa mabaraza ya Katiba, ambao utasambazwa nchini kote na kutangazwa katika vyombo vya habari ili wananchi wafahamu” alisema Warioba.
Alisema wajumbe wa mabaraza hayo watakuwa na jukumu la kujadili rasimu ya Katiba itakayowasilishwa na tume kabla ya rasimu hiyo kuwasilishwa katika Bunge maalum la Katiba litakaloketi Oktoba mwaka huu, ili kujadiliwa na kupitishwa.
“Hadi mwezi Agosti mabaraza ya Katiba yatakuwa yamemaliza kazi yake na hivyo Tume ya Katiba itakaa tena kuandaa rasimu nyingine ambayo itakwenda katika Bunge maalum la Katiba” alisema Warioba na kuongeza;
“Baada ya Rasimu kupitishwa na bunge hili, wananchi watapata fursa ya kupiga kura ya ndiyo au hapana ili kuidhinisha Katiba” alisema Warioba.
Alisema kuanzia kesho hadi Januari 25 mwaka huu, tume hiyo itaanza kukusanya maoni ya makundi mbalimbali ili kukamilisha hatua ya kwanza ya kukusanya maoni, ikiwa ni baada ya kumaliza mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi katika mikoa yote nchini, ulioanza Juni mwaka huu.
“Baada ya kumaliza hatua hii ya kukusanya maoni ya makundi kama, vyama vya siasa, taasisi za kidini, asasi za kiraia, makundi maalum pamoja na viongozi wa kitaifa, tutaanza kuandaa rasimu ya Katiba” alisema Warioba na kuongeza;
“Rasimu ya Katiba itakayoandaliwa itachapishwa katika magazeti ili wananchi wapate fursa ya kuisoma kabla ya kuwasilishwa rasmi katika mabaraza ya Katiba.”
Alisema mikutano ya mabaraza ya Katiba haitahusu kupiga kura, bali itakuwa ni kwa ajili ya kujadili rasimu ya Katiba itakayowasilishwa na tume.
“Nawaomba wananchi kushiriki kikamilifu katika kuwapata wajumbe watakaoshiriki katika mabaraza ya Katiba. Tume itatangaza vizuri utaratibu wa kuwapata wajumbe hawa hapo baadaye” alisema Warioba.
Idadi ya waliotoa maoni
Alisema watu 318,223 walitoa maoni yao katika awamu nne ambazo Tume hiyo ilikuwa ikikusanya maoni ya wananchi nchi nzima.
Previous
Next Post »