Chadema kwachafuka, vijana wake watimuana


Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana. Kuhusu masuala mbali mbali yanayohutu tume ya Katiba.

HALI si shwari katika Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), baada ya kuelezwa kuwa limemvua uongozi na kumfukuza uanachama Makamu Mwenyekiti wake, Juliana Shonza.
Habari zilizopatikana jana jioni zilieleza kuwa mbali na Shonza, baraza hilo pia limewafukuza uanachama aliyekuwa mgombea wa ubunge Jimbo la Kibaha Mjini, Habib Mchange na aliyekuwa akigombea ubunge Jimbo la Mbozi Mashariki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Mtella Mwampamba.
Habari kutoka ndani ya baraza hilo zimeeleza kuwa mbali ya viongozi hao, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya, Gwakisa Mwakasendo naye amepewa onyo kali.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya Bavicha kilichofanyika Mbezi, Dar es Salaam juzi.
Habari hizo zimeeleza kwamba viongozi hao wamefukuzwa kwa tuhuma mbalimbali. Hata hivyo, Shonza hakuwapo katika kikao hicho.
Akizungumzia madai hayo, Shonza alisema jana kwamba hata yeye amesikia taarifa hizo katika mitandao ya kijamii, lakini hana taarifa kwa kuwa hajapata barua yoyote.
“Mimi sikuwepo kwenye kikao lakini nimezisikia taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii na hata barua yenyewe ya kufukuzwa sijaipata, hivyo siwezi kusema chochote juu ya hilo,” alisema Shonza.
Kwa upande wake, Mchange alisema kwamba alihojiwa juzi katika kikao hicho na kuelezwa kuwa anakivuruga chama.
Alisema baada ya kuelezwa hivyo aliomba mwongozo wa Chadema, lakini hakupewa na baada ya kuhojiwa aliamuriwa kutoka nje ya kikao hicho.
“Baada ya kutolewa niliondoka lakini niliomba nisomewe katiba, lakini sikukubaliwa na hivyo tumesikia tu baada ya kuondoka kwamba uamuzi wa kutufukuza ulifikiwa,” alisema Mchange.
Alisema aliitwa kwenye kikao hicho akiwa mjumbe wa Bavicha, lakini alipofika ndipo akakutana na suala hilo la kuhojiwa kuhusu mambo ya chama.
“Hizo taarifa za kufukuzwa nimezisikia, lakini nikwambie tu Heche (John, Mwenyekiti wa Bavicha), hawezi kunifukuza uanachama kwa kuwa mimi si mwanachama wa Bavicha, bali ni mwanachama wa Chadema,” alisema Mchange.
Akizungumzia suala hilo, Mwampamba alisema kwamba aliitwa kwenye kikao hicho baada ya kutumiwa ujumbe wa kualikwa, lakini alipofika alitakiwa kusubiri nje ya ukumbi na baadaye aliitwa ndani.
“Ilipofika saa nne usiku niliitwa na kuelezwa kuwa kuna tuhuma ambazo natakiwa kujibu. Nilikataa na kuwaeleza kuwa sina imani na mwenyekiti pamoja na katibu, hivyo mabaunsa wakanitoa nje,” alisema Mwampamba.
Alisema amesikia taarifa za kufukuzwa kwenye mitandao ya kijamii, lakini hajashtushwa kwa kuwa kuna utaratibu ambazo lazima zifuatwe kabla ya hatua hiyo.
Alipotakiwa kuthibitisha habari hizo jana, Heche alisema amejipanga kutoa ufafanuzi leo katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Previous
Next Post »