Kituo cha polisi chavamia na watu 4 kuuawa

 
 
Polisi wa Nigeria wakishika doria baada ya shambulio
Watu wanne wameuawa nchini Nigeria, wakati kituo cha polisi na ofisi ya serikali ya mtaa ilipovamiwa na watu wenye bunduki Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa polisi nchini humo mashambulizi hayo yamefanywa katika mji wa Song, uliopo karibu na mpaka wa nchi hiyo na Cameroon.
Msemaji wa polisi wa jimbo la Adamawa, amesema polisi mmoja, mwanajeshi na raia mmoja na mjukuu wake ndio waliofariki.
Ingawa msemaji huyo wa polisi hakulilaumu kundi lolote kwa mashambulizi hayo, katika siku za hivi karibuni wapiganaji wa kundi la Boko Haram wamekuwa wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara Kaskazini mwa Nigeria.
Wakazi wa eneo hilo wanasema baadhi ya waliokufa miili yao ilikuwa imeteketezwa kwa moto.
Msemaji wa polisi Mohammed Ibrahim, ameiambia idhaa ya BBC ya lughya ya Hausa kwamba vikosi vya usalama tayari vimepelekwa katika eneo hilo.
Ameendelea kusema kwamba mpaka sasa hakuna mshukiwa yeyote aliyetiwa mbaroni.
Wiki iliyopita, kumekuwa na tukio kama hilo katika eneo la Maiha lililopo katika jimbo hilo hilo la Adamawa.
Mashambulizi yanayohusishwa na kundi la Boko Haram, ambalo linataka sheria za Kiislamu maarufu kama Sharia kuanza kutumika nchini humo, yashasababisha vifo vya zaidi watu elfu tatu katika miaka ya hivi karibuni.
 
Previous
Next Post »